VODACOM YATOA SHILINGI MILIONI 40 KWA USALAMA BARABARANI

Kampuni ya Mawasiliano  ya Vodacom Tanzania, imetoa msaada wa Sh milioni 40 kwa Serikali kupitia Baraza la Taifa la  Usalama Barabarani na Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani.
Hii ni kwa ajili ya kufanikisha wiki ya usalama barabarani mwaka huu inayotarajiwa kuzinduliwa hivi karibuni mkoani Arusha.
Hafla ya kukabidhi hundi ya fedha hizo ilifanyika jana katika Wizara ya Mambo ya Ndani ambapo waziri wake, Mathias Chikawe alikuwa mgeni rasmi akiongozana na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Ernest Mangu na Mkuu wa Kitengo cha Usalama Barabarani nchini, Kamanda Mohammed Mpinga.
Chikawe aliwashukuru Vodacom kudhamini kampeni ya usalama barabarani kwa mwaka huu kwa kutoa mchango wao  na kushirikiana na Polisi wa Usalama Barabarani kufikia malengo ya usalama wa raia na kupunguza ajali za barabarani.
Alisema ajali za barabarani zinaongezeka kwa kasi na kusababisha upotezaji wa nguvu kazi huku zikiacha maafa makubwa kwa taifa, hivyo ni jukumu la kila Mtanzania kuwa sehemu ya kusimamia na kuzingatia sheria za barabarani. Aliyataka makampuni mengine kuunga mkono jitihada hizi za kupunguza ajali nchini.
Naye Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano wa Vodacom, Georgia Mutagahywa alisema Vodacom Tanzania inajivunia kuwa sehemu ya juhudi za kuokoa maisha ya Watanzania na mali zao na ina dhamira ya kuhakikisha inashirikiana na wadau kusaidia usalama barabarani.
Aliongeza kuwa Vodacom imekuwa mstari wa mbele kusaidia shughuli mbalimbali za kijamii katika sekta ya elimu, afya, kupambana na umaskini.

No comments: