MAGUFULI AFIKIRIA KUYAONDOA MALORI YOTE DAR

Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli amesema anafikiria namna ya kuondoa malori ya mizigo katikati ya Jiji la Dar es Salaam, ili kupunguza tatizo la foleni na kuzuia uharibifu wa barabara.
Magufuli alisema kazi ya kuondoa malori hayo katikati ya mji, si ya Wizara moja, bali ya Serikali nzima pamoja na ushiriki wa wadau mbalimbali ili kulinda barabara zote.
Alisema hakuna sababu ya kuendelea kuingiza malori ya mizigo katikati ya mji, na kusababisha foleni ya magari na uharibifu wa barabara, wakati kuna reli yenye uwezo wa kupeleka mizigo hadi Kibaha na malori yakachukua mizigo hiyo huko.
Magufuli aliyasema hayo juzi wakati akizungumza katika Kijiji cha Vigwaza, mkoani Pwani, wakati akikagua ujenzi wa mizani ya kisasa ya magari.
“Hakuna sababu ya kuingiza magari mjini na kuharibu barabara na kuweka foleni, kuna reli inayopita hapa Ruvu na kuna eneo kubwa tu pale pembezoni mwa daraja la Ruvu, kwa maana hiyo kuna uwezekano wa kuweka bandari kavu pale na malori yakachukua mizigo pale.
“Hili jambo ni la kusaidia wote,hata nyinyi waandishi mtusaidie pia, mizigo ikichukuliwa pale tutaokoa fedha nyingi zinazopotea katika foleni za jijini Dar es Salaam na zinazotumika kutengeneza barabara zinazoharibika kutokana na uzito wa haya malori na kuzifanyia maendeleo mengine,” alisema.
 “Hii ni mizani ya kwanza ya kisasa hapa nchini ambayo kulingana na teknolojia iliyotumika, itasaidia katika kuondoa yale malalamiko mbalimbali ya wasafirishaji, ikiwemo ucheleweshwaji na rushwa,” alisema Magufuli.
Alisema kwa mujibu wa Sheria ya Usafirishaji, barabara za mikoa zinaruhusiwa kupitisha mizigo yenye uzito wa tani 56, lakini kinyume chake wasafirishaji wamekuwa wakipitisha magari mpaka yenye uzito wa tani 100.
Hali hiyo amesema imekuwa ikichangia barabara hizo kuharibika na kuonekana kama ziko chini ya kiwango wakati si kweli.
Akizungumzia mzani huo, alisema utakuwa msaada katika kupunguza foleni wakati wa upimaji, kwani kutakuwa na kifaa maalumu kitakachopima gari umbali wa meta 200, na endapo gari linalopimwa litakuwa halijazidisha uzito, litaruhusiwa kupita na kama uzito umezidi litatozwa faini.
Alisema mizani hiyo inatarajiwa kukamilika ndani ya miezi miwili ijayo na kuwataka wakandarasi kama kuna uwezekano, mzani huo ukamilike ndani ya mwezi mmoja, ili kuharakisha alichokiita mwarobaini wa wasafirishaji wabishi.
“Wale wasafirishaji waungwana wenye kufuata sheria hii itawapitia mbali, ni dawa ya ubishi wa wasafirishaji wanaozidisha uzito na baadaye kulalamika wanacheleshwa au kuombwa rushwa,” alisema.
Akikagua ujenzi wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili (MUHAS), Kampasi ya Mloganzila nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, Magufuli aliwataka wakazi wa eneo hilo kutokubali kurubuniwa na baadhi ya watu wasiotaka maendeleo.
Aidha, aliwaonya kutokubali kurubuniwa na wawekezaji wachache watakaokuja kutaka kuuziwa maeneo yao yaliyo jirani na chuo hicho, kitakachounganishwa na Hospitali ya Kisasa ya Kimataifa.
“Kuna watu wasiotaka maendeleo kwa manufaa wanayojua wenyewe, najua watakuwa wanapiga vita maendeleo haya, lakini hawajui kitakachotokea na msikubali kuwauzia wawekezaji maeneo yenu wakitaka labda muingie nao ubia ili mnufaike wote,” alisema.
Akijibu swali la mmoja wa wanakijiji aliyetaka kujua hatma ya waliobomolewa nyumba zao na kulipwa fedha kidogo, Magufuli alisema watu hao na waliojenga katika hifadhi ya barabara, hawatalipwa tena kwa kuwa sheria ya malipo inajulikana.
Aliwataka wakandarasi wanaojenga barabara ya kutoka Kibamba kwenda katika chuo hicho, kukabidhi barabara hiyo Novemba 30, mwaka huu ili wananchi wa eneo hilo waanze kutumia barabara hiyo.

No comments: