COMORO YAOMBA WALIMU KUTOKA ZANZIBAR

Serikali ya Comoro imeiomba Zanzibar kuwapatia walimu watakaofundisha masomo ya
kiswahili katika shule na vyuo nchini humo.
Hayo yalisemwa na Balozi wa Comoro nchini, Dk Ahmad Badrual-Ahmad, Mazizini alipokutana na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Ali Juma Shamuhuna.
Alisema licha ya wananchi wa Comoro kwa asilimia 90 kuzungumza Kiswahili cha kawaida, lakini bado wanahitaji mafunzo zaidi ikiwemo wanafunzi waliopo katika shule na vyuo vya elimu ya juu yatakayowajenga kuzungumza kwa ufasaha kiswahili.
“Tunaiomba Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali ya Zanzibar kutupatia walimu watakaofundisha lugha ya kiswahili kwa wanafunzi wetu kuanzia msingi, sekondari na vyuo vikuu,” alisema Dk Badrual-Ahmad.
Alisema Comoro ipo tayari kutoa walimu wa masomo ya Kifaransa. Wananchi wa Comoro huzungumza kwa ufasaha Kifaransa na lugha hiyo hufundishia katika shule za huko.
Balozi huyo alisifu uhusiano wa kindugu uliopo kati ya wananchi wa Zanzibar na
Comoro ambao ni wa asili.
Awali, Shamuhuna alisema milango ipo wazi kwa Comoro kuomba msaada wa kupatiwa walimu wenye sifa watakaofundisha Kiswahili. Alisema Zanzibar ni miongoni mwa nchi zenye sifa ya kuzungumza kiswahili kwa ufasaha mkubwa si Afrika Mashariki pekee bali duniani kwa ujumla.
Aidha alisema wapo walimu wa kutosha wenye uwezo wa kufundisha Kiswahili na Zanzibar ipo tayari kuwatoa bila ya kikwazo.

No comments: