NYUMBU WAOMBA MSAADA WA KUIMARISHWA

Serikali imetakiwa kuiwezesha Taasisi ya Tanzania Automotive Technology Centre (TATC) maarufu kama Nyumbu ili waweze kutengeneza  magari na vifaa mbalimbali hapa nchini vyenye ubora unaokubalika.
Mkurugenzi wa Fedha na Utawala  wa taasisi hiyo, Kunonga Mezza, alisema hayo jana kwenye Maonesho ya 38 ya Biashara  Kimataifa  yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere barabara ya Kilwa  maarufu kama Sabasaba.
Alisema taasisi hiyo iko chini ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ambayo inashughulika na kutengeneza magari aina ya nyumbu yanayotumika jeshini pamoja na vipuri mbalimbali vya magari na  mashine za kufyatulia matofali mashine ya kusaga pamoja na vifaa vya maji.
Alisema wamekuwa wakifanya tafiti mbalimbali za kutengeneza vifaa, mitambo, mashine na viputi mbalimbali vya magari hivyo ni vema Serikali kuwasaidia kuwawezesha kutengeneza vifaa hivyo nchini  vyenye ubora unaokubalika.
“Utafiti wa utengenezaji wa magari aina ya nyumbu yanayotumika jeshini imefikia mwisho, hivyo tunaendelea na tafiti nyingine ili kutengeneza vifaa vingi zaidi vitakavyotumika hapa nchini,” alisema.
Hata hivyo alisema wanashughulika kwa kutengeneza magari aina ya tippa kutengeneza vipuri vya gari mosho, pampu za maji, gea za magari, mashine za kusaga unga, mashine za kufyatua matofali pamoja na mashine za kuchakata mkonge.
Pia alisema taasisi hiyo inahitaji kuwa na mitambo ya kisasa itakayowezesha kutengeneza bidhaa nyingi na zenye tija ili kuhudumia watu wengi zaidi kwa wakati mmoja.
Hata hivyo alisema bado wanahitaji kufanyiwa mafunzo mbalimbali ili kuweza kutumia mashine mpya za kiteknolojia pamoja na kujengewa uwezo waweze kujifunza zaidi kutoka kwa nchi nyingine zinazoendelea.
Vile vile walieleza kuwa wanaweza kufanya kazi na kampuni binafsi na mtu mmoja  kwa kutoa huduma hiyo yenye ubora zaidi.

No comments: