KODI YA SIMU YAFUTWA, RAIS ASAINI HATI YA DHARURA...


Rais Jakaya Kikwete.

Rais Jakaya Kikwete, amesaini hati ya dharura kufuta kodi ya Sh 1,000 kwa mwezi kwa kila kadi ya simu, iliyowekwa katika Bajeti ya Serikali ya 2013/14.

Kutokana na hatua hiyo, Bunge limepelekewa taarifa ya kuweka suala hilo kwa dharura katika ajenda zake, ili yafanyike marekebisho katika Sheria ya Fedha ya 2013, kufuta kodi hiyo haraka.
Taarifa zilizofikia gazeti hili jana na kuthibitishwa na Ofisa Mwandamizi wa Serikali ambaye hakutaka kutajwa jina, zilibainisha hatua hiyo ya Rais, ingawa hazikuweka wazi marekebisho yatakayofanyika katika sheria hiyo, kama yameongeza kodi mpya itakayofidia pengo litakalotokea katika Bajeti baada ya kufutwa kwa kodi hiyo.
Hata katika mtandao wake,  Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, ameweka wazi kuhusu hatua hiyo ya Rais na kumshukuru.
“Mheshimiwa Rais ametia saini hati ya dharura kufanyika marekebisho kwa Muswada wa Fedha wa mwaka 2013 kuondoa tozo ya kodi kwa laini za simu…ahsante Mheshimiwa Rais,” alisema Makamba.
Kabla ya hatua hiyo, Julai 23 Rais Kikwete alikutana na kampuni za simu nchini, Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), Airtel, Vodacom, Tigo na Zantel na Wizara ya Fedha na Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia kujadili malalamiko yaliyotokea kupinga kodi hiyo.
Baada ya kikao hicho, Rais aliagiza wizara na kampuni hizo za simu za mkononi nchini, kukutana mara moja kutafuta jinsi ya kumaliza mvutano wa kodi hiyo.
Katika mkutano huo, Rais alitaka wahusika; kampuni za simu na wizara, kupendekeza jinsi ya kuziba pengo la Sh bilioni 178 ambazo zitapotea katika Bajeti ya Serikali, iwapo kodi hiyo itafutwa na Serikali.
Rais Kikwete aliweka wazi kuwa hawezi kuifuta moja kwa moja kodi hiyo, bila kutafuta njia nyingine za kupata fedha za kujaza pengo hilo la Sh bilioni 178 ambazo tayari Bunge limezipangia matumizi.
“Nakuombeni kaeni pamoja, wekeni bongo zenu pamoja, wekeni akili yenu pamoja mtafute namna gani tunaweza kujaza pengo hili la Sh bilioni 178, endapo tutakubaliana kuwa kodi hii inabebesha wananchi mzigo mzito na kuwa pengine menejimenti ya kodi yenyewe ni ngumu,” alisema Rais Kikwete alipokuwa akitoa agizo hilo.
Kodi hiyo ya Sh 1,000 kwa mwezi kwa kila kadi ya simu,  iliwekwa katika Bajeti ya Serikali ya 2013/14 ambapo ilitarajiwa kuingiza Sh bilioni 178.
Baada ya uamuzi huo wa Bunge, Umoja wa Wamiliki wa Kampuni za Simu Tanzania (MOAT), ulitoa tamko la pamoja kwamba  uamuzi huo utalazimisha kampuni hizo kupandisha gharama za simu kwa watumiaji.
Kampuni hizo pia zilidai kuwa eneo mojawapo litakaloathirika, ni huduma za intaneti  ambazo zinahitaji kuwekewa mikakati ya kukuzwa kutokana na umuhimu wake katika maisha ya sasa kiuchumi na kijamii.
Kwa ongezeko hilo, kampuni hizo zilidai kuwa huduma hizo za intaneti zingezorota kutokana na ongezeko la gharama na hivyo Watanzania wangeendelea kuwa na kiwango cha chini cha matumizi ya intaneti, ikilinganishwa na baadhi ya nchi zingine zikiwamo za Afrika Mashariki.
“Hatua hii ya kuongeza kodi itakwenda kinyume na mipango iliyopo yenye lengo la kuibadili jamii kwa kuipa maarifa ya msingi kupitia huduma ya intaneti sambamba na mawasiliano ya simu,” ilisema sehemu ya tamko hilo.
Mbali na tamko hilo, Chama cha Kutetea Walaji kiliwaburuta mahakamani Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Wizara ya Fedha, kikitaka wapewe amri ya kusimamisha kodi hiyo kwa watumiaji wa simu kila mwezi.Wakati kesi hiyo ikiendelea mahakamani, Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, iliruhusu kampuni za simu za Vodacom, Airtel, Mic Tanzania Ltd, TTCL na Zantel Tanzania, kujiunga katika kesi hiyo kupinga kodi hiyo.

No comments: