BUNDI AANZA KURANDA KWENYE PAA LA CHADEMA...

Ushahidi uliotolewa jana kwa wanahabari na aliyetangazwa kuvuliwa uanachama na umakamu Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Chadema (Bavicha) Juliana Shonza, unathibitisha mpasuko mkubwa ndani ya chama hicho cha upinzani.
Unazidi kukikandamiza chama hicho na tuhuma za ubaguzi wa kikabila na kikanda na ukiukwaji mkubwa wa Katiba yake, ukiwamo pia uthibitisho wa Baraza la Vijana kutokuwa na utambulisho miongoni mwa wanachama wake.
Lakini pia yanajitokeza madai, kwamba hata viongozi wa Baraza hilo hawana sifa za kuwa na nafasi hizo kutokana na kuwa na umri mkubwa kuliko kanuni zinavyotaka.
Shonza ambaye anapinga kuvuliwa uanachama na wadhifa sambamba na wanachama wenzake; Habibu Mchange, Mtela Mwampambwa na Grayson Nyakarungu, aliamua jana kupasua jipu ndani ya Chadema baada ya kuchukuliwa hatua hiyo Januari 5.
Makamu Mwenyekiti huyo anayepinga kuenguliwa, ameelekeza lawama zake kwa Mwenyekiti wake wa Baraza, anayemtaja kwa jina la Wegesa Suguta badala ya John Heche kama anavyofahamika ndani ya Chama hicho-alipoulizwa kiini cha jina hilo ‘jipya’ alisema ndilo linaloonekana katika vyeti vyake vyote vya taaluma.
“Kwanza kabisa naomba kuweka wazi kwamba sijawahi kupewa shutuma zozote au mashitaka yoyote yale yanayohusiana na hicho alichokiongea,” alisema Shonza huku akimjumuisha pia Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe kwa kushabikia hicho alichokiita kichefuchefu “kinachosambazwa kwa makusudi na virusi vichache vilivyojivika ngozi ya ukombozi”.
Baada ya kulalamika kutokana na taarifa zilizoandikwa katika baadhi ya magazeti yakifananisha kilio chake na utoto, Shonza alieleza kusikitishwa kwake na msimamo wa Mbowe kuhusu mtafaruku huo.
“Kitendo cha Mwenyekiti wangu,  Mbowe kujitokeza kupitia gazeti mojawapo na kudai madai yangu ni ya kitoto, kwanza kimenifedhehesha, ni dharau kwa vijana walioniona nina sifa na ukomavu na kunipa kura nyingi ili niwe Makamu Mwenyekiti wa Bavicha Taifa,” alilalamika Shonza jana.
Hata hivyo, alilalamikia kitendo cha Kamati ya Utendaji kushindwa kuwahoji  yeye na mwanachama mwenzake Exaud Mamuya, lakini yeye akachukuliwa hatua na Mamuya kuachwa.
“Hii ni ajabu sana katika kikao cha Kamati Tendaji batili, ambao hatukuhojiwa ni watu wawili, mimi Juliana Shonza na kijana mmoja anaitwa Exaud Mamuya. Lakini Juliana Shonza nimehukumiwa bila hata kusikilizwa, wala kupewa mashitaka na chombo chochote katika chama,” alisema na kuongeza kuwa huo ni mkakati wa kipuuzi ambao unaendeshwa na watu wapuuzi tena kwa misingi ya kikabila na kikanda.
“Taarifa zozote zile mlizozisikia kuhusu kuvuliwa kwangu uanachama, naomba kwa nguvu moja kupitia taaluma yenu muwaambie Watanzania wazipuuze. Ni taarifa zilizotolewa na kikundi cha kihuni kilicholenga kutimiza matakwa ya wakubwa wao. Kikundi hicho hakina mamlaka ya kikatiba yoyote yale ya kunivua uongozi huu nilionao,” Shonza aliwaambia waandishi wa habari.
Alidai pia kwamba  kibaraka wa kiongozi wa juu wa chama aliyetumika kutoa shutuma chafu dhidi ya Naibu Katibu Mkuu (Kabwe Zitto), ameachwa kwa madai yeye alikiri mbele ya Kamati Tendaji kwamba ni kweli alinuia kumchafua na kuvuruga chama. “Wakati tuhuma zake zinafanana na za Mchange na Mwampamba”.
Alisema ukanda huo  unajidhihirisha  kwenye kutoa hukumu batili kwa wanaotoka Mbeya, Mbozi na Kibaha wakati vijana wa Kilimanjaro wakiachwa, kwa madai walitoa ushirikiano. Shonza aliwataja wahusika hao kuwa ni Mwampamba (Mbozi), Mchange (Kibaha), Shonza (Mbozi), Joseph Kasambala (Mbeya Mjini-kasimamishwa) na Gwakisa Mwakasendo (Rungwe-kasimamishwa).
Waliosamehewa kwa mujibu wa Shonza ni Ben Saanane na Mamuya wote wa Kilimanjaro. Alisema hiyo ni dhamira ya wazi, kwamba Chadema sasa ni chama cha kikanda, viongozi wa Chadema wanatumika kutangaza ukanda kwa Watanzania. “Kwa maana hiyo wale wote wasio wa Kaskazini ndani ya Chadema tusitarajie kutendewa haki”.
Shonza alimtaka Mwenyekiti Mbowe kuacha kujenga makundi ndani ya chama hicho yanayoweza kugeuka mwiba siku za usoni.
Katika hatua nyingine Shonza alidai kuwa amekuwa akishauri masuala mbalimbali ndani ya chama hicho lakini ushauri wake umekuwa ukipuuzwa akisema:
“ Uanzishwaji wa chuo cha mafunzo ya uongozi kwa makada wa Chadema , badala yake ni matumizi mabaya ya fedha za ufadhili wa wadau tofauti na hasa mfadhili mkuu, Sabodo (Mustapha). Hii ingesaidia pia kulea kimfumo wa maadili ya uongozi kwa vijana wa umoja wa wanafunzi wa Chadema wa vyuo vikuu –CHASO, ambapo mimi ni muasisi wa mkakati huu nchini.
“Chama kwa ujumla kutokuwa na jengo letu na hasa makao makuu yetu. Ni aibu kwa chama kikubwa kama Chadema kuwa na ofisi tulizopanga na kulipa mamilioni ya fedha za ruzuku na misaada, kwa manufaa ya Mwenyekiti Mbowe na Mkurugenzi wa Fedha, wanaomjua mmiliki wa jengo la makao makuu. Kimsingi mimi natambua chama kina uwezo mkubwa wa kuwa na majengo yetu.
“Kupunguza mshahara wa Katibu Mkuu, Dk Slaa (Willibrod), ambao ni zaidi ya Sh milioni saba kwa mwezi na marupurupu kibao ili pesa hizo zielekezwe kujenga chama mikoani kama kweli tunataka 2015 tuingie Ikulu.
“Kuhakikisha pesa zilizochangishwa kwenye M4C zinatumika ipasavyo na si kama zitumikavyo kipindi hiki ambapo ni kama tumelewa wingi wa watu kwenye mikutano ya hadhara.
“Kitendo cha Mwenyekiti wa Chama kufumbia macho hatua ya Slaa-Katibu Mkuu kujikopesha pesa ya ruzuku ya Watanzania zaidi ya Sh milioni 140.
“Hatua ya Mwenyekiti Heche kulipwa mshahara na marupurupu hali kanuni za chama haziruhusu huku Mbowe akifumbia macho wakati viongozi wa mikoa na wilaya hawapewi pesa na vifaa vya uenezi na,
“kitendo cha mchumba wa Dk Slaa; Josephine Mushumbusi kuzunguka mikoani na kulazimisha kupokewa kama mke wa mfalme na kuendesha vikao vya ndani na vya hadhara vyenye kulenga kuwajenga wagombea ubunge anaowataka yeye na Katibu Mkuu kwa mwaka 2015,” alisema Shonza.
“Je hizi ndizo hoja za kitoto anazodai Mbowe? Hivyo basi namtaka Mbowe sasa asikimbilie kujibu hoja kishabiki. Ajitahidi kuwa na fikra na busara ili kukisaidia chama kuvuka kwenye daraja la sasa la pepo wa kufukuzana,” aliongeza.
 Kuhusu uhalali wa Bavicha, Shonza alisema siku zote amekuwa akishauri kuhusu utengenezaji ahadi za Baraza hilo na kusajili wanachama katika mfumo mzuri, ili kuweka kumbukumbu lakini imeshindikana.
“Mara nyingi nimeshauri kwa ajili ya maendeleo ya Baraza … nimekuwa nakwamishwa na Mwenyekiti na Katibu na hata leo sisi wote ni wanachama wa kufikirika tu,  kwa kuwa bado hatuna kadi za uanachama kwa vijana wa Bavicha zaidi ya kutambuliwa na Katiba ya Chama,” alilalamika Shonza ambaye bado anajitambulisha kama Makamu Mwenyekiti.
Kuhusu umri wa viongozi wa Bavicha, Shonza alidai kuwa wapo wanaopindukia miaka 35 na hivyo kunyenyekea kwa Heche ambaye alidai ana uwezo wa kuamua lolote bila kukemewa kutokana na udhaifu wa viongozi hao.
“Wajumbe wa Kamati Tendaji kikatiba ni makatibu wa kamati za uratibu za mikoa, lakini badala yake, Suguta amekuwa akiwaita wenyeviti wa mikoa na sababu kubwa ikiwa ni kwamba wengi wao hawastahili kuwa Bavicha kutokana na umri wao kuwa zaidi ya miaka 35 hivyo kupoteza sifa.
“Katiba inamtaka mwana Bavicha kuwa na miaka 18-35, hivyo kwa kuhofia kupoteza nafasi zao hulazimika kukubaliana na lolote ambalo Suguta analitaka, hata kama wakijua kwamba ni kinyume na matakwa ya Katiba na Mwongozo wa Baraza,” alisema.
Alitoa ushauri kwa vijana kuacha kugeuza siasa kuwa ajira au chombo cha kuendeshea maisha, kwani hatua hiyo ni kikwazo katika kukuza demokrasia ya kweli “maana wengi wanaendekeza njaa na mahitaji ya maisha yao ili kupindisha ukweli.”
Ili kupata haki, alisema yuko kwenye mchakato na wanasheria wake kushughulikia suala la kumpeleka mahakamani Heche na gazeti la Tanzania Daima, kwa kumwita msaliti wa Chadema, anatumiwa na CCM na kuwa ana uhusiano na Wasira (Stephen) tena bila kumhoji. “Kwa maana hiyo wamenichafua na kunidhalilisha mbele ya umma wa Watanzania”.
Pia kwa kutumia wadhifa wake wa Makamu Mwenyekiti akionesha wazi kupuuza hatua ya Chadema, alitangaza rasmi kuwa Mwampamba na Mchange ni wanachama hai na halali wa Chadema na kuwataka waendelee na kazi kama kawaida. 
Akizungumza kwa simu, Heche alisema hana muda wa kulumbana na Shonza kwa kuwa vikao vya kikatiba vya Chadema vimeshachukua hatua.
Akifafanua, alisema Katiba ya Chadema imetoa nafasi ya vikao vya juu ambavyo Shonza anaweza kukata rufaa yake kama hakuridhika na uamuzi huo.
Alihoji kama Shonza si msaliti na kama ana nidhamu, kwa nini hatumii vikao vya kikatiba na badala yake anakimbilia kukata rufaa katika vyombo vya habari.
Kuhusu jina lake, alikiri kuwa jina la Wegesa Charles Suguta ni lake na kufafanua kuwa Wegesa ni jina la nyumbani kama ilivyo Suguta kwa baba yake.
Aliendelea kufafanua kuwa Charles ni jina la baba yake la kubatizwa kama ilivyo John ambalo ni jina lake la kubatizwa na Heche ndio ukoo wao. Alimtaka Shonza asimpangie wakati gani wa kutumia majina yake.

No comments: