POLISI WA TANZANIA AFARIKI DUNIA DARFUR...

SSP Hawa Luzy akiwa katika picha ya pamoja na askari anaowaongoza baada ya kukabidhiwa bendera muda mfupi kabla ya safari ya kwenda Darfur, Sudan.
Ofisa wa Jeshi la Polisi, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP), Hawa Luzy aliyekuwa katika Operesheni ya Ulinzi wa Amani katika Jimbo la Darfur nchini Sudan, amefariki dunia.
Taarifa iliyotolewa jana Dar es Salaam na Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Paul Chagonja, ilisema ofisa huyo alifariki katika Hospitali ya Al-Fidelis mjini Khartoum, Desemba 22, mwaka huu ambako alikuwa amelazwa kwa matibabu ya maradhi ya tumbo.
Kamishna Chagonja alisema taratibu za kusafirisha mwili wa marehemu Luzy kutoka Khartoum kuja nchini zinafanywa kwa ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi na Umoja wa Mataifa (UN) ambao ndio waratibu wa Operesheni ya Ulinzi wa Amani katika Jimbo la Darfur.
Alisema ofisa huyo aliondoka nchini Machi, 2010 akiongoza kundi la askari wanawake 25 kwenda Darfur na alitarajiwa kumaliza mkataba wake wa ulinzi wa amani katika jimbo hilo Machi mwakani.
Aidha, akiwa Darfur alishika nafasi mbalimbali za uongozi kama vile Kamanda wa Polisi kwa Askari waliopo Darfur kwa mwaka 2010 hadi mwaka 2011, Kamanda wa Teknohama, Jinsia na Mkuu wa Huduma za Jamii.
Mpaka hivi sasa, Jeshi la Polisi lina maofisa na askari wapatao 262 waliopo katika Operesheni ya Ulinzi wa Amani katika Jimbo la Darfur.

No comments: