NOAH MARUFUKU, COASTER RUKSA KUBEBA ABIRIA KWENDA MIKOANI...

Magari ya aina hii sasa ni marufuku kubeba abiria wa kwenda mikoani kwa mujibu wa agizo la Sumatra.
Serikali imeruhusu mabasi aina ya Toyota Double Coaster kusafirisha abiria kwenda mikoa ya Kaskazini mwa nchi, ili kupunguza tatizo la usafiri wakati huu wa msimu wa sikukuu, lakini ikazikataa Noah.
Akizungumza jana, Ofisa Mfawidhi Kanda ya Mashariki wa Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra), Conrad Shio alisema lengo la uamuzi huo ni kuondokana na tatizo la usafiri.
Shio alisema mabasi ambayo yalikuwa tayari kufanya shughuli hiyo, yalitakiwa kupakia abiria wake kwenye Kituo cha Mabasi  ya Mikoani cha Ubungo chini ya usimamizi wa Sumatra na Polisi kwa kutumia bei halali iliyopangwa na Serikali.
“Kabla ya kuanza safari, mabasi haya yalitakiwa kuja Ubungo na kupakia abiria chini ya usimamizi wa Polisi na Sumatra na baada ya hapo tunawaandikia kibali na wanaanza safari yao,” alisema Shio.
Aidha, alisema katika operesheni waliyoianza ya kukagua mabasi yaendayo mikoani na kudhibiti upandaji wa nauli kiholela kuanzia Novemba mpaka Jumamosi iliyopita, mabasi 87 yalikamatwa kwa kosa la kupandisha nauli na asilimia kubwa yalikuwa aina ya Toyota Double Coaster.
“Katika mabasi tuliyokamata ni yale yanayofanya safari zake Dar es Salaam-Moshi-Arusha, Dar es Salaam-Mwanza na Dar es Salaam-Bukoba.
“Lakini kwa asilimia kubwa ni mabasi ya Toyota Double Coaster badala ya kufuata utaratibu tuliouweka na kuwa na vibali, waliweka vituo vyao Ubungo Maziwa, Mwenge na maeneo mengi na hao ndio tuliowakuta na kosa la kupandisha nauli hadi Sh 45,000,” alisema Ofisa huyo wa Sumatra.
Alisema pia mabasi manne yanayofanya safari zake kutoka Dar es Salaam kwenda Mwanza, yamekamatwa kutokana na ubovu, na mengine zaidi yako katika orodha hasa baada ya kufuatiliwa mwenendo.
“Utakuta mabasi ya kampuni fulani, leo limeharibika hili, kesho lingine na siku inayofuata lile la kwanza linaharibika, hii inaonesha kuwa kampuni hiyo haiyafanyii matengenezo. Majina ya kampuni hizo tutayataja baada ya kuyafikisha makao makuu,” alisema.
Shio alikana kuruhusu magari madogo aina ya Noah kusafirisha abiria na kuonya kuwa magari hayo yatakuwa yakifanya hivyo kinyume cha sheria na kwa kificho.
Kutokana na watu wengi kutaka kusafiri wakati huu wa msimu wa sikukuu za mwishoni mwa mwaka, bei za nauli za kwenda mikoani zimepanda zaidi huku baadhi ya abiria wakishindwa kusafiri kutokana na ongezeko la nauli na mabasi kujaa.
Uchunguzi ulibaini kuwa bei ya kutoka Dar es Salaam kwenda Arusha ilipanda hadi kufikia Sh 50,000 kwa abiria mmoja ikiwa ni tofauti na bei ya Serikali ya Sh 16,400 kwa mabasi ya kawaida; Semi-Luxury Sh 25,100 na Luxury Sh 28,600.
Ilibainika pia kuwa magari binafsi aina ya Noah juzi yalisafirisha abiria kwenda Moshi na Arusha kutoka Dar es Salaam.
Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani Tanzania, Pereira Ame Silima amesema kamwe Polisi haitaruhusu gari bovu kutembea barabarani hasa mabasi wakati huu wa msimu wa sikukuu.
Akizungumza jana na waandishi wa habari, Silima ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, alisema hatua hiyo inafanyika lengo likiwa ni kupunguza ajali za barabarani.
“Unaweza kukagua basi leo, dakika chache likaharibika, lakini Jeshi la Polisi limekuwa likiendelea na ukaguzi wa magari nchi nzima, na sasa ukaguzi huo hautakuwa ni hiari ila ni lazima, kwani hatutaki kuona mabasi mabovu yakitembea barabarani hasa kipindi hiki,” alisema Silima.
Akijibu swali la kuwa askari wa Usalama Barabarani ambao wanajificha nao huchangia ajali za barabarani, Silima alisema ingawa ajali nyingi zinatokana na makosa ya madereva, lakini Polisi ina mpango wa kupunguza vizuizi barabarani ili kuondoa tatizo hili.
Aidha, aliwataka madereva nchini kuhakikisha wanazingatia alama na sheria za Barabarani ili kupunguza ajali ambazo kati ya Novemba hadi Desemba kila mwaka,  ni kipindi cha ajali nyingi.
Akitolea mfano, Silima alisema kati ya Novemba hadi Desemba mwaka 2010, ajali 3,965 zilizotokea na kusababisha vifo vya watu 559 na majeruhi 3,377 na kipindi kama hicho kwa mwaka jana, ajali zilizotokea ni 3,326 zilizosababisha vifo vya watu 594 na majeruhi 3,034.
Alisema eneo lingine linaloongoza kwa ajali ni kwa waendesha pikipiki ambapo tangu Januari hadi Novemba 2012, ajali 4,637 zimetokea na kusababisha vifo vya watu 771 na majeruhi 4,562.
Aliwakumbusha na kuwataka watumiaji wote wa barabara kuzingatia sheria na kanuni za Usalama Barabarani na kubainisha chanzo cha ajali kuwa ni mwendokasi, ulevi, uendeshaji wa hatari, ujazaji wa abiria na mizigo na kutofuata michoro na alama za barabarani na ubovu wa magari.

No comments: