MUME AFICHUA SIRI OFISA WA TAKUKURU ALIVYOUAWA...

Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Dk Edward Hoseah.
Mume wa Ofisa Uchunguzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Bhoke Ryoba (34) aliyeuawa kwa kupigwa risasi na mfanyakazi mwenzake katika ufukwe wa Kigamboni jijini Dar es Salaam juzi, ameanika hadharani jinsi mkewe alivyouawa na kueleza kuwa alipigwa risasi ya kisogoni na siyo jichoni.
Aidha, mume huyo wa Bhoke, Charles Gibore ametaka vyombo vya Dola kuhakikisha haki inatendeka kuhusu kifo cha mkewe na ukweli usipotoshwe.
Mkewe aliuawa na mfanyakazi mwenzake, Mussa John (34), majira ya saa moja usiku wa Jumamosi katika ufukwe wa Kigamboni, ambako taarifa za awali zikimkariri Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Temeke, Engelbert Kiondo, zilidai kuwa Bhoke alipigwa risasi jichoni.
Lakini Gibore alisema jana kuwa mkewe aliuawa na mfanyakazi wenzake huyo kwa kupigwa risasi kisogoni na kutokea katika paji la uso tofauti na taarifa za awali kueleza kuwa alipigwa katika jicho la kushoto. Aliuawa katika eneo la ufukwe wa MO (Mohammed) Kigamboni katika Bahari ya Hindi.
Akizungumza nyumbani kwake Mji Mwema, Kigamboni wilayani Temeke, Dar es Salaam jana baada ya kutoa heshima za mwisho kwa mwili wa mkewe, Gibore alisema ana imani na vyombo vya Dola pamoja na Takukuru kuwa haki na ukweli wa mauaji hayo utabainishwa na jamii ijue.
Mwandishi alishuhudia mwili wa Bhoke ukiwa umefungwa kitambaa hadi kwenye paji la uso kuzuia jeraha hilo.
Mumewe alidai risasi iliyomuua mkewe ilitokana na mashindano ya wafanyakazi wenzake wa Takukuru na kwamba hakukuwa na uvamizi wowote wa majambazi eneo waliokuwa wakisherehekea kuwapongeza na kuwaaga wenzao waliofuzu mafunzo na kuhamishiwa vituo vingine mikoani.
Alisema amempoteza mtu muhimu katika maisha yake, ambaye saa tatu kabla ya kifo chake, alimpikia chakula na kula pamoja naye nyumbani na waliagana kuwa wataonana baadaye, lakini alishituka kuona anachelewa kurudi nyumbani isivyokuwa kawaida yake.
Akielezea mazingira ya kifo, Gibore alisema, “Mke wangu aliombwa na wenzake aandae chakula cha tafrija maana ana kampuni na mgahawa wa chakula…aliondoka nyumbani saa tisa alasiri, lakini alitanguliwa na mfanyakazi wake saa tano asubuhi ili aandae mazingira eneo la sherehe.”
Kwa mujibu wa mfanyakazi huyo wa mama Bhoke, mume huyo wa marehemu alisema alimueleza kuwa aliwakuta wafanyakazi hao wakiwa wanakunywa pombe katika ufukwe huo na baadaye wawili kati yao, walianza kushindana kupiga risasi kwa kutumia bastola zao.
“Baadaye waliingia baharini kuogelea na mke wangu akawa amefika, baada ya muda mmoja kati ya wale wawili alitoka majini na akachukua bastola na kuanza kupiga tena ovyo, mwenzake kuona hivyo, naye akatoka kwenye maji na kuanza kushindana kupiga ovyo ndipo akampiga mke wangu kisogoni na risasi ikatokea paji la uso,” alidai mume huyo wa marehemu Bhoke.
Alisema baada ya kuona mkewe anachelewa, alipiga simu yake ikawa haipatikani ndipo alipoamua kupiga ya mfanyakazi, ndio akamweleza kilichotokea kuwa mkewe amepigwa risasi na mfanyakazi mwenzake majira ya saa 12 jioni.
“Nilichukua usafiri wangu nikaelekea huko beach, niliwakuta baadhi wakikusanya vitu pamoja na wafanyakazi wetu wa chakula, nikawauliza watu wa Takukuru mke wangu yuko wapi, hawakunipa jibu? Baadaye wakanipa namba ya waliokuwa na mke wangu, nikawapigia kuwajulisha mimi mumewe wanieleze wako wapi, wakakata simu,” alisema Gibore.
Alisema aliamua kwenda Hospitali ya Vijibweni, lakini hakuwakuta na alipopiga simu, aliwapata na kumueleza wapo Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Kitengo cha Wagonjwa Mahututi (ICU), alipofika aliwakuta baadhi ya wafanyakazi wa Takukuru na daktari na muuguzi mmoja katika mapokezi ya ICU.
Alidai, daktari alimueleza hali ya mkewe walipompokea ilikuwa mbaya na kumtaka avute subira na baadaye alielezwa kuwa wamejitahidi kuokoa maisha yake, lakini imeshindikana.
Gibore alisema alimpigia simu Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Dk Edward Hoseah na kumweleza mkewe amefariki na Dk Hoseah alikuwa mtu wa kwanza kufika Muhimbili.
“Namshukuru sana Dk Hoseah, alifika Muhimbili hata kabla ya ndugu zangu, lakini vijana wake waliokuwa pale walimweleza kuwa walivamiwa na majambazi wakiwa ufukweni, jambo ambalo nilimweleza wazi kuwa vijana wake wanampotosha kwani walikuwa wakichezea silaha na mmoja alimpiga mke wangu kisogoni.
“Dk Hoseah alinihakikishia kuwa watafuatilia suala hilo kwa makini na kunitaka nivute subira, nina imani ingawa ndio nimepoteza mtu muhimu, sijui ni hila au bahati mbaya, lakini suala hili la kuchezea silaha namna hii linahitaji ufumbuzi,” alisema Gibore ambaye ni Meneja wa Mahusiano kwa Wateja Wakubwa katika Benki ya NBC.
Mkurugenzi wa Idara ya Elimu na Mafunzo kwa Umma wa Takukuru, Mary Mosha akitoa salamu za rambirambi, alisema kifo cha Bhoke kimeacha pengo maana kimetokea ghafla kwa kuuawa na mtumishi mwenzake na kuahidi uchunguzi unafanywa na Polisi.
Bhoke aliyezaliwa Juni 18, 1978, aliyekuwa pia mwanafunzi wa Shahada ya Uzamili katika Chuo Kikuu Mzumbe, aliajiriwa Takukuru mwaka 2008 katika Idara ya Uhasibu, lakini akiwa Ofisa Uchunguzi.
Ameacha mjane (Gibore) na watoto watatu (Doloresy Charles (10), Dolvin (4) na Dolrick mwaka mmoja na nusu). Anatarajiwa kusafirishwa kwa barabara leo saa 10 alfajiri kwenda Tarime mkoani Mara kwa maziko katika Kijiji cha Kirere yanayotarajiwa kufanyika kesho.
Mwili wake ulifikishwa nyumbani kwake saa 9.35 alasiri na vilio vilitanda kwa mamia ya wananchi waliojitokeza kumuaga Ofisa Uchunguzi huyo wa Takukuru.
Juzi, Kamanda Kiondo alisema mauaji ya Bhoke yalitokea kati ya saa moja na saa mbili usiku katika ufukwe wa Kigamboni ambako mtuhumiwa na marehemu walishiriki na wenzao kwenye masuala ya kijamii.
“Walikuwa kwenye kufurahi kijamii, si shughuli ya kiofisi, walikwenda kwa gari ndogo binafsi ambayo bado namba za usajili hatujazipata, katika kufurahi huko ndipo John alipiga risasi na kumpata Bhoke katika jicho la kushoto,” alisema Kamanda Kiondo.
Lakini akizungumza na gazeti hili jana usiku, Kamanda Kiondo alisema wanaendelea kumshikilia John na wanaendelea na uchunguzi, ingawa alibainisha kuwa mtuhumiwa huyo anaweza kufikishwa mahakamani baada ya sikukuu za Krismasi na Boxing Day.
“Huyu alijisalimisha mwenyewe hapa kwetu na tunaendelea kumshikilia huku tukiendelea na uchunguzi na pia kushirikiana na wenzetu wa Takukuru. Unajua Takukuru ni taasisi kubwa na hivyo tunataka kujua mazingira yote ya  mauaji hayo. Inaelezwa wote walikuwa wafanyakazi, je, katika nafasi gani? Je, huyu mwanamke alikuwa nani kwake, au shemeji yake?
“Tunaangalia pia ushahidi wa kifo kama ni ajali, kuua kwa kukusudia na alikuwa na nia ya kuua. Sote tunajua kuwa risasi ilifyatuliwa na kuua mtu, kwa hiyo, lazima tuangalie zaidi ya hapo. Uchunguzi unaendelea na unaweza kuchukua muda, lakini kwa kuwa amejisalimisha mwenyewe na kusema ameua, tunaweza kumfikisha mahakamani baada ya sikukuu,” alisema Kamanda Kiondo.
Awali, mtoa habari wetu juzi alidai wafanyakazi hao wakiwa katika ufukwe huo usiku saa tisa; baadhi  wakiwa wamelala na wengine wamekaa katika kusherehekea, walivamiwa na vibaka.
Mtoa taarifa huyo alidai baada ya kuvamiwa na vibaka, John alitoa bastola yake kwa nia ya kupiga juu ili kuwatawanya vibaka hao ambao haikufafanuliwa walikuwa wangapi, lakini kwa bahati mbaya Bhoke aliyekuwa amelala, aliamka ghafla na risasi ikampata kichwani.

No comments: