Baada ya miaka 38 ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kada
wake maarufu,
Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa amejitoa na kujiunga na
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Kwa kujiunga na Chadema katika sherehe iliyofanyika
kwenye hoteli maarufu Kunduchi, Dar es Salaam, Lowassa anajisafishia njia ya
kuteuliwa kugombea urais kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) ambao juzi
ulimwalika kujiunga nao.
Waziri Mkuu huyo aliyejiuzulu mwaka 2008 kutokana na kashfa ya
Richmond, alithibitisha kuwa Safari ya Matumaini aliyoiasisi ndani ya CCM
inaendelea, akimaanisha nia yake ya kutaka kuwa Rais wa Tanzania.
“Kama Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere
alivyosema, CCM siyo baba yangu wala mama na kwamba kama Watanzania hawapati
mabadiliko ndani ya CCM watayatafuta nje ya CCM. Sasa tuyatafute
mabadiliko hayo nje ya CCM,” alisema Lowassa.
“Hivyo basi, baada ya kutafakari kwa kina nimeamua kuwa
kuanzia leo ninaondoka CCM na kuitikia wito wa Ukawa kupitia Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kuungana nao katika kuleta mabadiliko ya
kweli ya nchi yetu,” alisema mbunge huyo wa Monduli mkoani Arusha tangu mwaka
1995.
Akieleza sababu za kutoka CCM ambako aliwania urais mwaka huu
na kutemwa
katika vikao vya uteuzi, Lowassa alisema anaamini hakutendewa
haki katika mchakato mzima wa kupendekeza majina na kuteua
mgombea wa Urais kupitia chama hicho tawala.
Alisema mchakato huo uligubikwa na mizengwe, ukiukwaji wa
maadili, uvunjaji
wa Katiba na taratibu za uchaguzi za CCM, na dhahiri, alidai
uchaguzi ulisimamiwa
kwa upendeleo na chuki dhidi yake.
“Kwa mantiki hiyo, nitakuwa mnafiki kama nitaendelea
kujidanganya mimi mwenyewe na umma wa Watanzania kwa kusema kuwa bado nina
imani na CCM au kuwa CCM ni chama kitakachowaletea ukombozi wa kweli wa kiuchumi,
kisiasa na kijamii.
“CCM niliyoiona Dodoma siyo tena kile chama nilichokulia
na kilichonipa malezi na maadili ya siasa yaliyojengwa kwenye misingi ya haki,
usawa na uadilifu,” alisema Lowassa na kuongeza kuwa kama Mtanzania aliye na
uchungu na nchi yake, “nasema imetosha na sasa basi!”
Akielezea kuhusu kuendelea kwa falsafa yake aliyoitumia CCM
kuomba urais, Lowassa aliyefuatana na mkewe Regina na familia
yake, alisema: “Safari ya Matumaini inaendelea kupitia Ukawa, lakini
haitafanikiwa
iwapo sote hatutajiandikisha kupiga kura. Natoa wito kwa wakazi wa Dar es
Salaam kutumia fursa iliyopo kujiandikisha kwa wingi. Naiomba Tume ya Uchaguzi
iongeze siku za muda wa kujiandikisha kama ilivyofanya Njombe.”
Akizungumzia kuondoka kwake CCM aliyojiunga nayo ilipoasisiwa
mwaka 1977, Lowassa alisema hakufanya uamuzi huo kwa pupa, lakini
unafika wakati wa kuchukua maamuzi hata kama ni magumu kwa kuamini
fika kuwa ni kwa maslahi ya Taifa.
Chadema, CUF, NLD na NCCR-Mageuzi kwa mwaliko wao na imani yao
na kuthamini mchango anaouweza kutoa kufanikisha azma ya kuleta mabadiliko na
maendeleo.
Lowassa aliyevalia shati la maji bahari na suruali ya ‘dark
blue’ na viatu nyeusi, aliwasili kwenye ukumbi wa mkutano saa 10.19 akifuatana
na viongozi wa Ukawa.
Alizungumza kwa dakika 15 kuanzia saa 10.29 na ilipofika saa
10.51 alikabidhiwa kadi ya Chadema na Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho,
Freeman Mbowe, akitanguliwa na mkewe Regina. Mbali ya hao wawili, familia
yake ambayo inahusisha watoto watano, pia imeelezwa kujiunga na Chadema pamoja
na wafuasi wake kadhaa akiwamo Naibu Waziri wa zamani, Goodluck ole Medeye
ambaye alisema leo atazungumzia hatima yake kisiasa.
Akijibu maswali ya waandishi wa habari, Lowassa alisisitiza
hahusiki na kashfa ya Richmond na kwamba amechoshwa na tuhuma hizo.
“Nimechoka na suala hili, nimesema kama kuna mtu ana ushahidi
aende mahakamani. Kama huna ushahidi, please, shut up and keep quiet (kama huna
ushahidi nyamaza),” alisema Lowassa na kuongeza kuwa hatalipa kisasi na kuwa
wanaosema atalipa kisasi wanaogopa kwani wamefanya dhambi gani.
Kwa upande wao, Mwenyekiti wa NLD Taifa, Dk Emmanuel Makaidi
alimkaribisha kwa moyo mkunjufu Lowassa katika Ukawa na asahau mambo ya
CCM. Naye Makamu Mwenyekiti wa CUF Zanzibar, Dk Juma Duni Haji alisema
Lowassa ni jembe kwasababu wameongeza nguvu ya Ukawa ulioasisiwa wakati wa Bunge
la Katiba mwaka jana.
Mwenyekiti wa Taifa wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia
alisema Lowassa ni jasiri na kwamba Ukawa haitamwaga damu katika kuingia
madarakani.
Mbowe ambaye alikuwa mwenyeji wa Lowassa jana, alikiri kuwa
mchakato wa
kumwingiza mwanasiasa huyo ndani ya Chadema haukuwa
rahisi.
Alisema kulikuwa na hofu kubwa ndani ya chama chake na kudai
kuwa baadhi ya viongozi wa CCM walimpigia simu wakitaka asimpokee
mwanasiasa huyo.
Akitetea tuhuma zinazoelekezwa dhidi ya Lowassa, Mbowe alisema
hawawezi kuishi kwa mambo ya zamani na yasiyo na ushahidi, na chama hicho
hakiwezi kuwa chama cha kuhukumu watu.
Alisema wamekubali kumchukua Lowassa kwa sababu
ya rekodi yake ya utendaji na kwamba atakuwa na haki zote sawa na mwanachama
mwanzilishi
wa Chadema.
Lowassa aliyezaliwa Agosti 26, 1953, sasa anajiandaa
kupeperusha bendera ya Ukawa katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, baada ya vyama
hivyo vinne kufanya uteuzi wao wa ndani, lakini Chadema ikimsimamisha yeye na
vyama vingine vitamuunga mkono. Kwa mujibu wa wakuu hao wa Ukawa, mgombea
wao atapatikana mapema mwezi ujao kabla ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi kufanya
uteuzi wa wagombea Agosti 21, mwaka huu.
Licha ya kuwapo kwa viongozi wengi wa kitaifa wa Ukawa,
kiongozi wa juu
aliyekosekana jana alikuwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbrod
Slaa.
Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Zanzibar, Salum Mwalimu
alipoulizwa kuhusu kukosekana kwa Slaa, alisema ni vyema akatafutwa
mwenyewe. “Lakini kuna jambo gani kubwa kwani hata viongozi wengine hawapo
kama John Mnyika,” alieleza Salum, hata baada ya kueleza kuwapo kwa viongozi
wengine wa juu, bado alisema hakuna tatizo lolote.
Mkutano huo ulihudhuriwa na wabunge kadhaa wa Chadema na
wafuasi wao.
No comments:
Post a Comment