WASHITAKIWA KESI YA 'MTOTO WA BOKSI' KUHOJIWA UPYA POLISI



Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Morogoro, imekubali ombi la upande wa mashitaka, katika kesi ya kula njama na kufanya ukatili dhidi ya mtoto Nasra Mvungi (4), kutaka washitakiwa wahojiwe upya Polisi, ili mashitaka yanayowakabili yabadilishwe baada ya kifo cha muathirika.
Mwendesha Mashitaka na Wakili wa Serikali, Sundy Hyera, kwa kushirikiana na jopo la mawakili wenzake akiwemo Mwendesha Mashitaka wa Polisi, Anganile Msiani, aliwasilisha ombi hilo jana Mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mkoa wa Morogoro, Mary Moyo.
Awali washitakiwa hao, baba mzazi Nasra, Rashid Mvungi (47), mkazi wa Lukobe na mtumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro na wanandoa Mariam Said (38) na mumewe Mtonga Omar (30), wakazi  wa Mtaa wa Azimio, Kata ya Kiwanja cha Ndege, Manispaa ya Morogoro, walifikishwa mahakamani hapo jana kujibu mashitaka yanayowakabili.
Wakili Hyera alidai muathirika Nasra alifariki dunia Juni mosi mwaka huu, kwa hiyo ipo haja ya kusikiliza ombi hilo, ili mahojiano hayo yafanyike upya na kuwezesha mabadiliko ya mashitaka kwa washitakiwa wote watatu.
Pia aliomba mahakama ipange tarehe nyingine ya karibu kwa mwezi huu, ili kesi hiyo ifikishwe mahakamani hapo kutaja baada ya kufanyika mahojiano mapya na washitakiwa Polisi.
Baada ya hoja hizo, Hakimu Moyo aliridhia ombi hilo na kutoa ruhusa washitakiwa wote watatu wafikishwe Polisi kuhojiwa na kuandikisha maelezo mengine,  kwa kuwa  mtoto Nasra ameshafariki.
Hakimu huyo aliiahirisha kesi hiyo hadi Juni 12, mwaka huu itakapofikishwa mahakamani hapo kutajwa tena, pia aliamuru  washitakiwa waliopo rumade, waendelee kubakia rumande.
Awali wakazi wa Manispaa ya Morogoro  walifurika kwenye viwanja vya mahakama hiyo, kusikiliza kesi inayowakabili washitakiwa hao.
Wananchi wa rika mbalimbali walianza kumiminika mahakamani hapo kuanzia saa mbili asubuhi, wakiwa na nia ya kuona  hao wanaodaiwa kumfanyia katili mtoto huyo, kwa kumfungia ndani ya boksi kwa miaka zaidi ya mitatu.
Mshitakiwa wa kwanza kufika mahakamani hapo saa nne asubuhi, alikuwa Mvungi ambaye yupo nje kwa dhamana na wenzake waliletwa kwa gari la Polisi, lililokuwa pia na  mahabusu wengine wanaokabiliwa na mashitaka ya aina mbalimbali mahakamani hapo.
Washitakiwa hao waliposhuka kwenye gari, wananchi waliokuwepo mahakamani hapo waliwazomea huku wakitoa kauli za mashinikizo kwa mahakama, kwamba itoe adhabu kali ili iwe ni fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama hiyo.
Mkazi mmoja wa mtaa wa Boma aliyekuwepo mahakamani hapo, aliamua kuangua kilio baada ya kuwaona washitakiwa hao, huku akisema wamemkosea Mungu pamoja na kiumbe huyo asiye na hatia hapa duniani.
Hali hiyo ya nje ya Mahakama, ikiwemo pia heka heka za baadhi ya wananchi waliokuwa na simu zenye
kamera  kutaka kupinga picha washitakiwa, ilisababisha mashauri mengine yasitishwe kwa muda, ili kupisha kesi hiyo kwanza.
Ndani ya chumba cha wazi cha mahakama, kulifurika watu na kuwapa wakati ngumu askari Polisi kuhakikisha ulinzi na amani wakati wote wa shauri hilo.
Baada ya kesi kuahirishwa, watu hao walizingira gari dogo lililofika mahakamani hapo kuwachukua washitakiwa na kuwapeleka Kituo Kikuu cha Polisi, ambapo waliamua kusukuma kwa nyuma huku
wanawake wa wanaume wakiendelea kuzomea washitakiwa hao.

No comments: