SERIKALI YARIDHISHWA NA KITENGO CHA USALAMA TPA


Serikali imeeleza kuridhishwa na utendaji kazi wa kitengo cha usalama cha Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kutokana na kilivyoimarisha ulinzi katika bandari na hivyo kuchangia kuongeza ufanisi. 
Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe, alitoa zawadi jana kwa askari wa mamlaka hiyo walioonesha moyo wa kujitolea na kufanya kazi kwa ufanisi. 
Akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika jana Dar es Salaam, Dk Mwakyembe alisema kazi yao nzuri imeongeza usalama na kuvutia zaidi wateja. “Nawasifu kwa kazi nzuri mnayofanya,” alisema. 
Alisema kujitolea kwao na weledi wao umesaidia kuokoa mamilioni ya Shilingi ambayo yangepotea kwa wizi katika bandari hiyo. 
Alisema kutokana na kuimarika kwa usalama bandarini hapo, nchi mbalimbali zinaanza kuonesha nia ya kutumia zaidi bandari hiyo kupitisha mizigo yao. 
Akitoa mfano, Waziri huyo alisema ujumbe wa maofisa wa Serikali ya Kongo na wafanyabiashara kutoka jimbo la Katanga waliotembelea bandari hiyo wiki hii ni ishara kubwa kuwa  bandari inaanza kurudisha heshima yake. 
Baadhi ya zawadi zilizotolewa ni pamoja na pikipiki, televisheni, simu za mkononi, pesa taslimu na kompyuta mpakato zilizochangiwa na wadau mbalimbali. 
Takwimu zinaonesha idadi ya meli zinazotumia bandari hiyo imeongezeka kutoka 1,236 mwaka 2011/12 hadi kufikia meli 1,301 mwaka 2012/13. 
Kwa upande wa shehena mwaka 2012/13 bandari ilihudumia tani milioni 12.5 ikilinganishwa na tani milioni 10.9 za mwaka 2011/12, ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 15. 
Pia kwa mwaka wa 2012/13 bandari ilihudumia nchi zinazotumia bandari hiyo shehena ya tani milioni nne ambayo ni sawa na asilimia 32 ya shehena yote. 
Mwaka 2012/13 wastani wa Sh bilioni 371.7 zilikusanywa, sawa na ongezeko la asilimia 14.3 ukilinganisha na Sh bilioni 325.3 mwaka 2011/12. 
Matukio ya uhalifu na wizi yamepungua kutoka matukio 21 mwaka 2011 hadi matukio saba mwaka 2012, na kufikia matukio 3 mwaka 2013. 
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Madeni Kipande alimshukuru Waziri Mwakyembe kwa kuweka suala la usalama katika vipaumbele vya wizara.  
Mkuu wa Kitengo cha Usalama cha TPA,  Lazaro Twanga alisema kutambuliwa huko kumewapatia motisha na nguvu ya kufanya kazi nzuri zaidi.

No comments: