HALMASHAURI 80 KUVUNA SHILINGI BILIONI 40 KWA NYUMBA ZA WALIMU



Serikali inatarajiwa kutoa Sh bilioni 40 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za walimu katika halmashauri 80 nchini, sawa na Sh Sh milioni 500 kwa kila halmashauri.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Fedha, Saada  Salum Mkuya aliposoma Hotuba ya Serikali kwa mwaka wa fedha wa 2014/15.
Alisema hayo mjini hapa juzi, wakati akielezea matumizi ya fedha kwa makundi maalumu, hasa kuhusu ujenzi wa nyumba za walimu.
Waziri huyo alisema serikali inaendelea na utaratibu wa ujenzi wa nyumba za walimu kwa awamu.
Alisema katika mwaka wa fedha 2013/14, halmashauri 40 zilipewa kila moja Sh milioni 500 ili zianze ujenzi wa nyumba za walimu. Kiasi kama hicho, kitatolewa katika halmashauri hizo kwa mwaka 2014/15. 
“Aidha, Sh milioni 500 zitatolewa kwa halmashauri 80 zaidi, hivyo kufanya jumla ya halmashauri 120 kunufaika na utaratibu huo, lengo likiwa ni kuzifikia halmashauri zote mwaka 2015/16”, alisema.
Aliwahimiza viongozi wa Serikali katika ngazi za mikoa, wilaya na kata, kusimamia kikamilifu fedha hizo ili zitumike kwa malengo yaliyokusudiwa.
Kuhusu malipo ya madai ya walimu, alisema serikali inaendelea kulipa madai ya walimu yaliyohakikiwa, ambapo katika mwaka 2014/15 kiasi cha Sh bilioni 5.6 kimelipwa.
“Aidha, kwa mwaka 2014/15 madai ya walimu ambayo yatakuwa yamehakikiwa, yataendelea kulipwa.
Aidha, Waziri huyo alisema uwiano wa mwalimu kwa wanafunzi katika shule ya msingi, umeimarishwa kutoka 1:47 mwaka 2012 na kufikia 1:43 mwaka 2013, ikilinganishwa na lengo la uwiano wa 1:40. Katika elimu ya sekondari, uwiano wa mwalimu kwa mwanafunzi ulifikia lengo la MKUKUTA II la 1:28 mwaka 2013.

No comments: