"CONFUCIUS" WA UDOM WATOA MISAADA KWA YATIMA


Taasisi ya 'Confucius' ya Chuo Kikuu cha Dodoma kimetoa misaada ya huduma za utafiti wa afya na dawa zenye thamani ya Shilingi milioni moja kwa Kituo cha watoto yatima cha Matumaini kilichopo mjini hapa kama sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Watoto Duniani inayoadhimishwa kila Juni mosi. 
Mkurugenzi Mkazi wa taasisi hiyo ambayo hutoa mafunzo ya lugha na utamaduni wa Kichina Zheng Xueyu alisema kwa kutambua siku ya maadhimisho ya siku ya mtoto wamekitembelea kituo hicho ambapo pamoja na mambo mengine wametoa msaada wa vipimo vya afya kwa watoto wanaoishi hapo. 
Pia wametembelea wagonjwa wanaoishi na maambukizi ya Ukimwi kituoni hapo na taasisi hiyo imetoa dawa zenye thamani ya Shilingi milioni moja. 
Mkurugenzi huyo alisema pia mafunzo ya kusoma na kuhesabu kwa lugha ya Kichina yalitolewa kwa watoto wenye umri kati ya miaka mitatu  hadi sita na mafunzo ya kuimarisha afya ya mchezo wa kung fu  yalitolewa kwa vijana wenye umri kati ya miaka sita  hadi 12 wanaoishi katika kituo hicho. 
Katika ziara hiyo kikundi hicho kilifuatana pia na madaktari wa tiba ya afya wanaotoa huduma katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma na kusaidia kutoa vipimo na ushauri wa kiafya kwa watoto hao kwa ushirikiano na madaktari kutoka China ambapo kwa ujumla waliwapima watoto hao na kutoa ushauri kwa walezi wa kituo hicho ambapo matibabu zaidi ya kina yatafanyika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma hapo baadaye. 
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kituo hicho Padre Vicent Boseri alisema ziara hiyo imetimiza matakwa ya maandiko matakatifu ya kuwajali wenye shida na uhitaji. 
Alisema kituo hicho kina jumla ya wanafunzi yatima 140 wanaofadhiliwa na kituo hicho ambapo 60 wanasoma elimu ya chekechea, 100 elimu ya msingi na 10 elimu ya sekondari.

No comments: