BAJETI YA SERIKALI 2014/2015 YAFYEKA MISAMAHA YOTE YA KODI

Bajeti Kuu ya Serikali ya Sh trilioni 19.87, imewasilishwa jana bungeni na Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum, huku ikiwabana wananchi katika bidhaa na huduma za starehe, na   kipaumbele kikubwa kikiwa elimu.
Aidha, katika Bajeti hiyo, badala ya Serikali kupata fedha kutoza kodi bidhaa za muhimu kwa wananchi kama mafuta, safari hii, wananchi hawajaguswa katika huduma na bidhaa muhimu kwao, na badala yake fedha nyingi zinatarajiwa kukusanywa baada ya kufuta misamaha ya kodi.
Akiwasilisha bajeti hiyo bungeni jana, Waziri Saada, aliweka wazi kuwa ni Bajeti ya ‘lala salama’, pale aliposema kuwa ndiyo Bajeti ya mwisho, katika utekelezaji wa Awamu ya Pili ya Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini (MKUKUTA II).
“Mheshimiwa Spika, Awamu ya Pili ya Mkukuta inafikia tamati Juni 2015, hivyo Bajeti hii ni ya mwisho katika utekelezaji wa Mkukuta II. Aidha, Malengo ya Maendeleo ya Milenia ambayo yametumika kama sehemu ya mikakati yetu ya kupunguza umasikini yanafikia tamati mwaka 2015,” alisema Waziri Mkuya.
Ingawa Waziri Mkuya hakuweka wazi, lakini Bajeti hiyo pia ndiyo ya mwisho itakayotekelezwa kikamilifu na Serikali ya Awamu ya Nne ya Rais Jakaya Kikwete.
Bajeti ijayo ya 2015/16, Serikali iliyopo madarakani itapata fursa ndogo ya kutekeleza sehemu tu ya bajeti hiyo, na sehemu itakayobakia, itatekelezwa baada ya kupatikana kwa Rais wa Awamu ya Tano, baada ya kukamilika kwa Uchaguzi Mkuu wa 2015.
Mipango mingine inayopaswa kumalizika kabisa au kwa sehemu kubwa wakati wa utekelezaji wa Bajeti hiyo, ni Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2010-2015 na Mpango wa Kwanza wa Maendeleo wa Miaka Mitano katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 utafikia tamati Juni 2016.
“Kazi iliyo mbele yetu ni kutafuta jinsi masuala ya kupunguza umasikini, yatakavyooanishwa katika mikakati na mipango yetu baada ya Juni 2015, wakati tunaelekea kuhitimisha Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano mwaka 2016,” alisema Mkuya.
Alisema Serikali itaongeza ushuru wa vinywaji baridi kutoka Sh 91 kwa lita hadi Sh 100 kwa lita, ikiwa ni ongezeko la Sh 9 kwa kila lita.
Pia itaongeza ushuru wa bidhaa kwenye juisi iliyotengenezwa kwa matunda yaliyozalishwa hapa nchini kutoka Sh 9 kwa lita hadi Sh 10 kwa lita, ikiwa ni ongezeko la Sh moja tu kwa lita.
Pia itaongeza ushuru wa bidhaa kwenye juisi iliyotengenezwa kwa matunda ambayo hayazalishwi hapa nchini kutoka Sh 110 kwa lita hadi Sh 121 kwa lita, sawa na ongezeko la Sh 11 kwa lita.
“Ushuru wa bidhaa kwenye maji yanayozalishwa viwandani, hautaongezeka,” alisema Mkuya.
Kwa upande wa bia, ushuru wa bia inayotengenezwa kwa nafaka ya hapa nchini na ambayo haijaoteshwa mfano kibuku, utaongezeka kutoka Sh 341 kwa lita hadi Sh 375 kwa lita, ikiwa ni ongezeko la Sh 34 kwa lita.
Ushuru wa bia nyingine zote, utaongezeka kutoka Sh 578 kwa lita hadi Sh 635 kwa lita, ikiwa ni ongezeko la Sh 57 kwa lita.
Ushuru wa mvinyo uliotengenezwa kwa zabibu inayozalishwa ndani ya nchi, kwa kiwango kinachozidi asilimia 75, utaongezeka kutoka Sh 160 kwa lita hadi Sh 176 kwa lita, ikiwa ni ongezeko la Sh 16.
Ushuru wa mvinyo uliotengenezwa kwa zabibu inayozalishwa nje ya nchi, kwa kiwango kinachozidi asilimia 25, utaongezeka kutoka Sh 1,775 kwa lita hadi Sh 1,953 kwa lita, ikiwa ni ongezeko la Sh 178 kwa lita.
Ushuru wa vinywaji vikali, utaongezeka kutoka Sh 2,631 kwa lita hadi Sh 2,894 kwa lita, ikiwa ni ongezeko la Sh 263 kwa lita.
“Marekebisho ya viwango vya ushuru wa bidhaa kwenye sigara ni kama ifuatavyo: Sigara zisizokuwa na kichungi, zinazotengenezwa kutokana na tumbaku inayozalishwa hapa nchini, kwa kiwango cha angalau asilimia 75, utaongezeka kutoka Sh 9,031 hadi Sh 11,289 kwa sigara 1,000. Hiyo ni sawa na ongezeko la Sh 2.25 kwa sigara moja,” alisema.
Sigara zenye kichungi zinazotengenezwa kutokana na tumbaku inayozalishwa hapa nchini kwa kiwango cha angalau asilimia 75, ushuru wake utaongezeka kutoka Sh 21,351 hadi Sh 26,689 kwa sigara 1,000 ikiwa ni ongezeko la Sh 5.30 kwa sigara moja.
Ushuru kwa sigara nyingine, zenye sifa tofauti  na zilizotajwa hapo juu, kwa mujibu wa Waziri Saada, utaongezeka kutoka Sh 38,628 hadi Sh 48,285 kwa sigara 1,000, sawa na Sh 9.65 kwa sigara moja.
“Ushuru wa sigara aina ya ‘cigar’ unabaki kuwa asilimia 30,” alisema.
Katika moja ya nafuu iliyotangazwa na Serikali, imepunguza kiwango cha chini cha Kodi ya Mapato ya Mishahara (PAYE) hadi asilimia 12 kutoka asilimia 13. Pia imeahidi kuongeza kima cha chini cha mishahara, ambacho hata hivyo hakikutajwa.
Waziri Mkuya alisema katika Bajeti hiyo ya Sh trilioni 19.8, Serikali inalenga kukusanya mapato ya kodi na yasiyo ya kodi ya Sh trilioni 12,18, kati ya hizo, mapato ya kodi ni Sh bilioni 11.31 na mapato yasiyo ya kodi, ni Sh bilioni 859.8. Aidha, mapato yanayotokana na vyanzo vya halmashauri ni Sh bilioni 458.5.
Waziri Mkuya alisema Serikali inaendelea na jitihada za kupata misaada na mikopo ya masharti nafuu, ambapo inatarajia kupokea Sh trilioni 2.94. Kati ya fedha hizo misaada na mikopo ya kibajeti ni Sh bilioni 922.1, Mifuko ya Kisekta Sh bilioni 274.1 na miradi ya maendeleo Sh trilioni 1.75.
Waziri Mkuya alisema kwa nia ya kuendeleza miradi ya miundombinu nchini, Serikali itakopa katika soko la ndani Sh trilioni 3.  Kati ya hizo,  Sh bilioni 689.56  ni za kugharimia miradi ya maendeleo na Sh trilioni 2.3 ni kwa ajili ya kulipia hatifungani na dhamana za Serikali zinazoiva.
Pia itakopa Sh trilioni 1.3 kutoka masoko ya fedha ya nje kwa masharti ya kibiashara kwa ajili ya kugharimia miradi ya maendeleo.  
Akizungumzia mgawanyo wa fedha, Mkuya alitaja Sekta ya Elimu kuwa ndiyo iliyotengewa fedha nyingi kuliko sekta yoyote katika sekta za kipaumbele zilizoteuliwa katika Mpango wa Tekeleza kwa Matokeo Makubwa Sasa (BRN).
Sekta hiyo kwa mujibu wa Mkuya, imetengewa Sh trilioni 3.466, ambapo kati ya hizo Sh bilioni 307.3 zimetengwa kugharimia mikopo ya elimu ya juu.
Fedha zilizobakia zimepangwa kutumika kuimarisha ubora wa elimu ikijumuisha miundombinu ya elimu, ambapo Waziri Mkuya alisema lengo ni kusaidia upatikanaji wa vifaa vya kujifunzia na kufundishia, kuimarisha na kujenga madarasa na maabara.
Pia Serikali katika sekta hiyo, imekusudia kuhakikisha vijana  wanapata fursa za ajira, hivyo juhudi zimewekwa kuimarisha vyuo vya ufundi stadi vilivyo chini ya Mamlaka ya Elimu ya Ufundi Stadi  (VETA).
Sekta ya pili kwa kupewa mgawo mkubwa ni Miundombinu ya usafirishaji, ambapo Sh trilioni 2.1 zimetengwa na kati ya hizo,  Sh bilioni 179.0 ni kwa ajili ya ununuzi wa mabehewa na ukarabati wa Reli ya Kati.
Aidha Waziri Mkuya alisema Sh trilioni 1.4 ni kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa barabara na madaraja.  “Azma hii inalenga kupunguza msongamano wa magari mijini, gharama za usafiri na usafirishaji wa bidhaa na huduma, na hivyo kupunguza mfumuko wa bei.”
Sekta inayofuata kwa kutengewa kitita kikubwa cha fedha ni Afya, ambayo Waziri Mkuya alisema Sh trilioni 1.59, zimetengwa kwa ajili ya ununuzi wa dawa, kuzuia magonjwa ya mlipuko, chanjo za watoto, ujenzi wa zahanati na kudhibiti maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi na malaria.
Sekta ya Kilimo, imetengewa Sh trilioni 1,08, kwa ajili ya kuimarisha miundombinu ya umwagiliaji katika maeneo mbalimbali yakiwemo ya Ukanda  Maalumu wa Kilimo wa Kusini mwa Tanzania  (SAGCOT).
Pia fedha hizo zimelenga kutumika kwa ajili ya ujenzi wa maghala na masoko; na upatikanaji wa mikopo kwa ajili ya kukuza uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara.
Waziri  alisema Serikali itaendelea kuwekeza kwenye ugani kwa kuimarisha vyuo vya utafiti katika kilimo na kuhakikisha kunakuwa na maofisa ugani wa kutosha na mbegu bora.
“Hatua hii itaimarisha uzalishaji wa mazao, usalama wa chakula na kuhakikisha upatikanaji wa masoko ya uhakika,” alisema.
Kwa upande wa Nishati na Madini, Serikali imetenga Sh trilioni 1,09, kati ya hizo Sh bilioni 290.2 zimetengwa kwa ajili ya Wakala wa Umeme Vijijini (REA), ili kusambaza umeme vijijini.
Aidha, Sh bilioni 151 zimetengwa kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam na Sh  bilioni 90 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa mtambo wa kufua umeme kwa kutumia gesi wa Kinyerezi I.
“Hatua hii inalenga kuhakikisha upatikanaji wa umeme wa uhakika na kupunguza gharama zake na hivyo kuvutia uwekezaji na kuongeza ajira,” alisema.
Sekta ya Maji imetengewa Sh bilioni 665.1  kwa ajili ya kuimarisha miundombinu ya maji mijini na vijijini ikiwa ni pamoja na  kuendelea na ujenzi wa visima katika vijiji 10 kwa kila halmashauri na kukamilisha ujenzi wa bomba la maji kutoka Ruvu Chini hadi Dar es Salaam. 
Katika Utawala Bora, Serikali imetenga Sh bilioni 579.4 kwa ajili ya kuimarisha utawala bora, ikiwa ni pamoja na kugharimia Bunge Maalumu la Katiba;  vitambulisho vya Taifa; Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2014; kuhuisha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura; maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015; mapambano dhidi ya rushwa na utoaji wa haki kwa wakati.
Katika jitihada za kuongeza mapato zaidi, Waziri wa Fedha ameondolewa mamlaka ya kusamehe kodi katika maeneo muhimu, ambapo Waziri Mkuya aliwaomba wabunge waiunge mkono Serikali,   katika hilo ili kurahisisha usimamizi wa kodi nchini na hivyo kutoa unafuu kwa walipa kodi, na kuongeza mapato ya Serikali.
“Serikali itachukua hatua kuu mbili muhimu. Kwanza, kutoa taarifa ya misamaha ya kodi kila robo mwaka kwa kuwatangaza walionufaika na misamaha kwenye Tovuti ya Wizara ya Fedha.
“Hatua hii itasaidia kuleta uwazi na uwajibikaji katika suala la misamaha ya kodi na kuwafanya wananchi wajue ni nani anayenufaika na misamaha hiyo,” alisema.
Pili, alisema Serikali itatoa taarifa ya kina ya misamaha yote ya kodi iliyotolewa na kuiwasilisha bungeni kila mwaka, ili  wabunge mpate nafasi ya kujadili na kutoa maoni yenu.

No comments: