Bandari ya Dar es Salaam. |
Nafasi za kazi zilizotangazwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPR) kwa ajili ya viongozi wa juu wa Mamlaka hiyo, zimedaiwa kuibua vita kubwa ya ajira, imeelezwa.
Habari za uhakika ambazo gazeti hili linazo zinasema wengi wa waliojitokeza kuomba nafasi hizo katika mamlaka hiyo yenye nguvu kubwa kiuchumi ni pamoja na waliokuwa viongozi wa mashirika ya umma, binafsi, serikalini na hata waliopata kuongoza baadhi ya wakala za Serikali.
Lakini kutokana na ushindani kuonekana kuwa mzito, imeelezwa baadhi ya wajumbe wa Bodi ya PTA wamekuwa wakidaiwa kuhusika kuwatengenezea waombaji hao mazingira mazuri ya kupata ajira.
Kutokana na baadhi ya wajumbe wa Bodi kudaiwa kuwatafutia wagombea njia za mkato, Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Profesa Joseph Msambichaka licha ya kushangazwa, alisema kama kuna wanaojaribu kutumia hila, wanajisumbua kwa kuwa mchakato wa mwisho utafanywa na kampuni binafsi, tena za nje ya nchi.
“Nami ndiyo nasikia, lakini pia inawezekana, maana kuna watu kila kukicha wanahaha kushika nafasi nzito nzito na bandari ni nzito…sasa kwa kulitambua hilo na ili kuzuia mianya ya kuchomekeana watu, sisi tunapitia maombi yao, kisha tutakabidhi kwa kampuni huru kabisa, tena za kimataifa.
“Wajue Bodi haitahusika na hatua za mwisho za kumpata kiongozi wa TPA, wataalamu ndio watakaoangalia uwezo na sifa za kila anayeomba kazi katika Mamlaka. Narudia, kama wanajipitisha na kutumia hila kupitia Bodi, wanajisumbua,” alisisitiza Profesa Msambichaka.
Mbali ya Profesa, wajumbe wengine wa Bodi ya TPA ni Julius Mamiro, Jaffa Machano, Caroline Kavishe, Asha Nassoro, Dk Kuwe Bakari, Dk Hildabrand Shayo, Abdul Sauko na John Ulanga.
Kwa mujibu wa nyaraka kuhusu mchakato huo, mchakato wa kupitia majina na kutoa mapendekezo unaanza hivi karibuni kabla ya Bodi ya TPA kufanya uamuzi wa mwisho ifikapo mwisho wa mwezi huu.
Nafasi zilizotangazwa ni za Mkurugenzi Mkuu, Naibu Mkurugenzi Mkuu (Miundombinu), Naibu Mkurugenzi Mkuu (Huduma), Meneja wa Bandari ya Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala, Mkurugenzi Huduma za Sheria, Meneja Uhusiano, Meneja Kitengo cha Mafuta, Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Huduma na Mkurugenzi wa Teknohama.
Kutangazwa kwa nafasi za kazi katika ngazi ndani ya TPA mwishoni mwa Aprili mwaka huu kunatokana na kuondolewa na kusimamishwa kazi kwa baadhi ya watendaji waandamizi wa Mamlaka hiyo.
Hivi karibuni, Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe alitangaza kutimua kazi wakurugenzi watatu na mameneja wawili wa TPA.
Wakurugenzi hao walitimuliwa kazi kwa nyakati tofauti baada ya uchunguzi wa tuhuma zilizokuwa zikiwakabili kukamilika na watuhumiwa hao kuhojiwa.
Miongoni mwa tuhuma zilizosababisha vigogo hao kuondolewa ni matumizi mabaya ya madaraka na ubadhirifu wa mali ya umma na kuitia hasara Serikali.
Waliotimuliwa ni aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Ephraim Mgawe, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Huduma, Hamadi Koshuma, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Miundombinu, Julius Mfuko, Meneja wa Bandari ya Dar es Salaam, Cassian Ngamilo, Meneja Kituo cha Kupakulia Mafuta (KOJ), Tumaini Massaro.
Baada ya kuondolewa kwa viongozi hao na wengine kusimamishwa, Madeni Kipande aliteuliwa kukaimu nafasi ya Mkurugenzi Mkuu wa TPA.
No comments:
Post a Comment