Moja ya ndege za Qatar Airways ikiwa safarini. |
Watu kadhaa wametapeliwa na wanaojiita maofisa wa shirika la ndege la Qatar nchini, kwa kisingizio cha kuwapatia ajira ya uhudumu wa ndani ya ndege.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti la HABARILEO, umebaini kuwapo kwa watu wanaojitambulisha kuwa maofisa wa Qatar Airways ambao walipenyeza tangazo katika gazeti hilo kualika maombi ya watumishi hao bila hata kueleza sifa zao.
Hadi jana, zaidi ya watu 20 kutoka mikoa ya Arusha, Dar es Salaam, Dodoma na Morogoro, walikuwa wametapeliwa kati ya Sh 200,000 na Sh 500,000 kila mmoja huku wengine wakiombwa fedha za kigeni zikiwamo dola za Marekani zisizopungua 300.
“Fedha hizo zinaombwa na maofisa hao wanaojitambulisha kwa majina ya Salum Balhabou na Mariam Hussein, wanaotumia namba 0656274439 na 0765166185 zilizosajiliwa Tigo na Vodacom,” alisema mmoja wa watu walionusurika kutapeliwa.
"Wanafanya utapeli wao kwa kushirikiana ambapo ukizungumza na mmoja anakupa maelekezo na kukushawishi uzungumze na mwenzake kwa ajili ya maelezo zaidi," alisema mwingine ambaye alitapeliwa na kuongeza kuwa mbinu wanayotumia si rahisi kubainika na mtu mwenye shida ya kazi.
Hata hivyo, pamoja na kutapeli watu fedha, watu hao wanaodhaniwa kuwa huenda hata majina waliyotumia kujisajili si yao wanapotezea watu nauli na muda kwa kuwadanganya, kuwa waende ukumbi wa usaili Diamond Jubilee na Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere, Dar es Salaam, huku wakijua hakuna usaili unaoendeshwa na kampuni hiyo.
"Baada ya kutuma Sh 200,000 kwa Mariam, nilitumiwa ujumbe mfupi wa maandishi ukinielekeza niandike maombi ya ajira kwenda kwa Meneja Uajiri wa Qatar Airways kwa kutumia S.L.P. 4244, Dar es Salaam, halafu nifike kwenye usaili Diamond Jubilee kesho yake nikiwa na barua yangu...".
"Nilifanya hivyo siku ilipofika, lakini sikukuta usaili wowote, nikampigia simu huyo Balhabou, akaniambia usaili umehamishiwa katika ukumbi wa Uwanja wa Ndege ambako pia nilikwenda na kukuta kimya. Kuona hivyo nilimpigia tena simu, lakini iliita bila majibu na siku ikaisha nikajua nimetapeliwa," alisema mkazi wa Ukonga, Dar es Salaam, aliyefanyiwa utapeli huo.
Mbali na kutumia ukumbi wa Diamond Jubilee kama chambo, wapo waliotakiwa kuchagua wakafanye kazi Doha, Qatar; Amsterdam, Uholanzi na Johannesburg, Afrika Kusini na wapo walioambiwa wachague nafasi kulingana na kiasi cha fedha walichokituma kwa matapeli hao.
“Kwanza waliniambia nafasi zipo na nitume dola 300 niingizwe katika orodha ya waliopita usaili na kisha kesho yake nipande ndege nianze kazi, huku nikiulizwa ningependa nianzie wapi,” alisema mmoja wa waathirika ambaye hata hivyo hakutoa fedha hizo, licha ya kubembelezwa.
Baada ya Mhariri Mkuu wa gazeti la HABARILEO kupata taarifa za kuwapo kwa aina hiyo ya usaili, aliwapigia simu wahusika hao akijifanya ni mmoja wa wazazi wa mwombaji nafasi hiyo ya ajira ambaye aliombwa awapelekee dola 300 za Marekani.
Naye alipewa maelekezo hayo, huku Balhabou na Mariam kwa kujiamini, wakisisitiza watumiwe shilingi za Tanzania kwa Tigo Pesa na iwe jioni ya juzi, kwani jana ndio ulikuwa mwisho wa kuwasilisha majina ngazi za juu na kupitishwa tayari kuanza kazi.
“Ajitahidi atume hizo Sh 200,000 za kuanzia jioni hii hii (juzi saa moja usiku), kwa kuwa nina watu wanne hapa ili niwaweke sawa kwa hamsini hamsini (Sh 50,000), ili jina lake lipitishwe, kwa kesho atakuwa amechelewa…,” alijinasibu Mariam.
Habari kutoka ndani ya shirika hilo la kimataifa la ndege, zilisema utapeli huo ulianza baada ya gazeti la HABARILEO kutoa tangazo dogo la kazi likionesha kuwa kampuni hiyo ilikuwa ikihitaji wahudumu ndani ya ndege zake, ilhali haikuwa kweli.
"Namba zinazotumika kuiba fedha za watu ndizo zinazoonekana kwenye tangazo hilo dogo, sasa tunaamini wahusika wa utapeli walilitangaza kwa makusudi na kuweka namba hizo ili wahitaji wa kazi wawapigie, kusikiliza maelezo yao na kuwatumia fedha.
"Hadi leo asubuhi tumefuatwa na watu wengine wakiwa na fedha mkononi wakitaka kulipa ili waingizwe kwenye orodha. Kwa ufupi, huo ni utapeli na sisi Qatar hatutafuti wafanyakazi kwa mtindo huo … hatuuzi kazi," mmoja wa maofisa waandamizi katika ofisi za ndege hizo alisema na kukataa kutajwa kwa kuwa si msemaji.
Kwa maelezo yake, walianza kupokea watu waliotapeliwa Mei 19, lakini kutokana na ukweli kwamba hawahusiki na utapeli huo wala kuhitaji watu, walishindwa kuwasaidia na badala yake kuanza taratibu za ndani za kisheria ili kuchukua hatua ambazo hata hivyo, hawakuzifafanua.
"Wamekuwa wakilalamika na kutuonesha jinsi walivyohamisha fedha kutoka kwenye simu zao kwenda kwa matapeli hao. Kweli wameibiwa fedha nyingi. Kampuni yetu imetumika tu...Watanzania wanapaswa kutokuwa wepesi kukubali kutuma fedha kwa wasiowajua na kilichotokea kiwe funzo kwao," alisema.
Alieleza ni kwa nini Qatar haihusiki na kusema kwanza haitangazi kazi kwa mtindo uliotumika kwa lugha ya Kiswahili na hata kuweka namba za simu.
Vilevile alisema, ikitokea ajira, usaili utafanywa na wahusika watakaotoka makao makuu Doha ambao huja nchini siku ya usaili na kuondoka jioni siku hiyo hiyo.
“Hawa wameibiwa na hatuna namna ya kuwasaidia, kwa sababu unapowasiliana na Vodacom na Tigo unaambiwa akaunti za wahusika hazina fedha, ikimaanisha wamekwishazihamisha," alisema Ofisa huyo wa Qatar Airways.
1 comment:
Jamani ilo swala limetokea tena mwezi Hui march 16/2015 wamebandika nafasi A kazi name pia nilivyo pig a nimeambiwa nitumw 300$ kwa supervisor ili anisajili leo sababu kesho ndio wanaanza kushughurikia maswala ya visa alafu mshahala ni sh 1000$ je walofanya ivyo wamefanikiwa?
Post a Comment