WATAKA FAO LA KUJITOA MIFUKO YA HIFADHI YA JAMII LISAIDIE WANACHAMA...

Jenister Mhagama.
Bunge limeibana Serikali likiitaka kuifanyia marekebisho sheria ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, ili pamoja na kuruhusu Fao la Kujitoa pia iruhusu mwanachama kuchukua sehemu ya mafao yake kulipia mkopo wa nyumba na sehemu nyingine kuandaa maisha yake baada ya kustaafu.

Akisoma taarifa ya Kamati ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii kuhusu utekelezaji wa bajeti ya Wizara ya Kazi na Ajira kwa mwaka ujao wa fedha, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mbunge wa Peramiho, Jenister Mhagama (CCM) alisema lengo la mpango huo ni kusaidia wanachama wa mifuko hiyo walio kazini sasa.
Pamoja na hayo, Mhagama alisema Kamati inaishauri Serikali kupitia sheria hiyo itengeneze mfumo mzuri utakaowezesha kuwapo Fao la Kujitoa bila kuathiri anguko la mifuko ili kukidhi hifadhi ya uzeeni.
“Mwanachama aruhusiwe kutumia sehemu ya mafao yake ya uzeeni kulipia mkopo wa nyumba na aruhusiwe kutumia sehemu ya mafao yake ya uzeeni kugharimia mambo mengine kwa lengo la kuandaa mazingira mazuri ya maisha baada ya kustaafu,” alisema Mhagama kwa niaba ya Kamati hiyo.
Mhagama alisema Kamati inaipongeza Serikali kwa kuandaa Muswada ulioliwezesha Bunge kutunga Sheria Namba 8 ya mwaka 2008, ambayo ilianzisha Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Hifadhi ya Jamii (SSRA).
“Sheria hiyo pamoja na zote za hifadhi ya jamii zilifanyiwa marekebisho mwaka wa fedha unaoishia sasa kupitia Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, Sheria Namba 5 ya mwaka 2012 ili kuondoa kukinzana.
"Hata hivyo tangu kufanyika kwa marekebisho hayo ya sheria kumekuwa na migogoro baina ya SSRA na baadhi ya wanachama wa mifuko ya hifadhi ya jamii nchini ambao wanadai marekebisho hayo ya sheria yatawaumiza kutokana na kuondoa fao la kujitoa. Kutokana na hali hii Kamati inashauri kufanyike marekebisho katika sheria hiyo,” alisema Mhagama.
Alisema baadhi ya madai ambayo yanatolewa na wafanyakazi wanaopinga utekelezwaji wa sheria hiyo ni pamoja na baadhi ya sekta kama ya madini ambayo inahusisha matumizi ya dawa na mionzi ambapo watumishi wake hawana uhakika wa kufanya kazi mpaka miaka 55 au 60 hivyo kuondoa Fao la Kujitoa ni kuwanyima haki.
Madai mengine kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo wa Kamati ya Bunge ni watumishi wa sekta binafsi kukosa uhakika na ajira zao na hasa ikizingatiwa kuwa Tanzania haina utaratibu wa kisheria wa malipo ya watu wasio na kazi.
Alisema pia kuwa takwimu zinaonesha kuwa wastani wa umri wa kuishi wa Mtanzania ni kati ya miaka 47 na 53 hivyokukosekana Fao la Kujitoa ni kuwanyima haki zao.
“Hata hivyo baada mkinzano wa matumizi ya Sheria hiyo na hali halisi ya mahitaji ya wafanyakazi, Kamati inaona upo umuhimu wa kupitiwa haraka na kufanyiwa marekebisho kwa sheria hiyo,” alisema Mhagama.
Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni, Cecilia Paresso (Viti Maalumu- Chadema) alisema kambi hiyo inaitaka Serikali kuwa makini katika kuendelea kutumia fedha za wafanyakazi kwenye mifuko ya hifadhi hizo kuwekeza katika miradi ambayo haina manufaa  kwa wafanyakazi.
“Tulifanya rejea pana ya taarifa kuu ya mwaka ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kuhusu hesabu za Mashirika ya Umma na taasisi zingine kwa mwaka 2010/11, iliyoonesha kwamba kuna udhaifu mkubwa katika vitega uchumi vinavyosimamiwa na mifuko hiyo,” alisema Paresso.
Akisoma hotuba yake ya bajeti, Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudentia Kabaka alisema katika mwaka wa fedha wa 2012/13 SSRA imefanya tathmini na uwezo wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), kufanya ukaguzi katika mifuko sita ya hifadhi ya jamii kwa lengo la kuhakikisha kuwa inatekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria.

No comments: