Profesa Anne Tibaijuka. |
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anne Tibaijuka, leo anawasilisha hotuba yake ya bajeti kwa mwaka ujao wa fedha huku akikabiliwa na kibarua kizito cha kujibu hoja kuhusiana na migogoro ya ardhi, ubora wa majengo na masuala ya makazi.
Kwa mujibu wa ratiba mpya ya Bunge, bajeti ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, ambayo ilikuwa iwasilishwe leo imesogezwa mbele hadi Juni 4 mwaka huu.
Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imepewa siku mbili ikifuatiwa na Wizara ya Kazi na Ajira ambayo imepewa siku moja ya Jumatano.
Migogoro ya ardhi ni miongoni mwa maeneo ambayo yamekuwa yakichomoza sana kwenye hotuba ya bajeti ya wizara hiyo kila mwaka yakiwemo pia masuala ya ujenzi wa maeneo yaliyotengwa kwa shughuli mbalimbali za kijamii, ikiwemo maeneo ya wazi.
Suala la wapangaji mijini kulazimishwa na wenye nyumba kulipa kodi ya mwaka mzima iliyowasilishwa na Mbunge wa Bumbuli, Januari Makamba (CCM), kwenye bajeti ya mwaka jana pia linategemewa kuibuliwa mwaka huu ili kufahamu hatua zilizochukuliwa katika utekelezaji wake.
Ubora wa majengo ikiwemo kuporomoka kwa majengo katika Jiji la Dar es Salaam kutokana na ubora hafifu pia linatarajiwa kuibuliwa katika mijadala ya hotuba hiyo.
Ghorofa lililoporomoka katika Mtaa wa Indira Ghandhi na kusababisha vifo vya watu wapatao 20, linatarajiwa kuibua mjadala upya.
Miongoni mwa mambo ambayo Waziri Tibaijuka anatarajiwa kubanwa na wabunge, ni kuhusu amri yake ya kutaka jengo pacha na hilo lililoporomoka libomolewe ambayo hadi sasa haijatekelezwa.
Hata hivyo hivi karibuni, Waziri Tibaijuka alipoulizwa mjini hapa na waandishi juu ya kupita kwa siku 30 alizotoa kwa jengo hilo kubomolewa, alisisitiza kwamba agizo lake liko pale pale na akasema wanaopaswa kutekeleza hilo ni Halmashauri ya Manispaa ya Ilala.
Kwa mujibu wa Tibaijuka, aliamuru jengo hilo libomolewe si kwa sababu ya ubora kwa kuwa mamlaka zinazopaswa kuthibitisha ubora ni nyingine; isipokuwa aliamuru kwa kuwa ujenzi wake ulikiuka kanuni kutokana na kuongeza idadi ya ghorofa kinyemela licha ya eneo hilo kutostahili kujengwa ghorofa 10.
Wakati huo huo Wizara ya Kazi na Ajira, inatarajiwa kubeba hoja nyingi zikiwemo za ukosefu wa ajira kwa vijana wengi huku mifuko ya hifadhi ya jamii nayo ikikabiliwa na maswali juu ya kwanini haiwekezi katika miradi mikubwa ili kukuza uchumi wa nchi.
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa itawasilisha hotuba yake ya bajeti Alhamisi ambapo bila shaka hoja ya mgogoro wa Malawi na Tanzania utakuwa ni miongoni mwa hoja zitakazoibuka.
Hoja nyingine zitakuwa ni ushirikiano na uhusiano baina ya Tanzania na mataifa mengine.
Suala la ubora wa Balozi za Tanzania katika nchi mbalimbali ambalo limekuwa likilalamikiwa na wabunge wengi ikiwemo Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, linatarajiwa kujitokeza katika mjadala wa wizara hiyo.
Wizara ya Mifugo na Uvuvi ambayo wafugaji wamekuwa wakilalamikia kufukuzwa katika maeneo mbalimbali ikiwemo Loliondo unatarajiwa kuliteka Bunge wakati Wizara hiyo itakapowasilisha hotuba yake ya bajeti kwa mwaka ujao wa fedha Ijumaa.
No comments:
Post a Comment