Kikao cha Bunge kikiendelea mjini Dodoma. |
Mjadala mkali umeibuka miongoni mwa wabunge wakati wa kujadili Sera ya Taifa ya Elimu na Mafunzo iliyowasilishwa na Serikali baada ya kupinga tamko la kutaka umri wa kuanza elimu ya awali uwe miaka mitatu huku wengine wakiunga mkono.
Wakati baadhi ya wabunge akiwemo Mbunge wa Viti Maalumu, Suzane Lyimo (Chadema) wameiunga mkono wakisema ni nzuri , wengine hususan Mbunge wa Viti Maalumu, Hilda Ngoye (CCM) akisema umri huo ni mdogo kwa mtoto kuanza kufundishwa masomo ya darasani.
Ngoye aliungwa mkono na Mbunge wa Tarime, Nyambari Nyangwine (CCM) aliyesema sera hiyo imezingatia zaidi maeneo ya mijini kwani ni vigumu kwa watoto wa vijijini wenye umri huo kutembea umbali mrefu kwenda shule.
Aidha Mbunge wa Muleba Kaskazini, Charles Mwijage (CCM) naye alisema sera hiyo imejumuisha mazingira ya mijini na vijijini wakati ukweli ni kwamba maeneo hayo ni tofauti.
Hoja hizo zilitolewa baada ya mtoa mada, Katibu Mtendaji wa Shirikisho la Vyuo Vikuu nchini, Profesa Sifuni Mchome kueleza masuala mbalimbali yaliyomo ndani ya Sera hiyo. Mchome ndiye Mwenyekiti wa Kamati iliyotunga Sera hiyo.
Semina hiyo iliyohudhuriwa na viongozi wa juu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, wakiongozwa na Waziri, Dk. Shukuru Kawambwa na Naibu wake, Philipo Mulugo.
Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudentia Kabaka pamoja na kusifu sera hiyo lakini alisema lazima baadhi ya vipengele viangaliwe kwa kina kwa vile umri wa mtoto kuanza shule ya awali akiwa na miaka mitatu na ule wa miaka minne kwa mtoto kuanza shule ya msingi ni mdogo sana kwa kuanza kumjaza mtoto masomo ya shule.
Mbunge wa Viti Maalum, Suzan Lyimo (Chadema) alisema sera hiyo ni nzuri na akidai serikali imeamua kuja na sera hiyo ambayo iliasisiwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo.
Kwa mujibu wa Lyimo, walisisitiza elimu ya msingi na sekondari kuunganishwa kwa miaka 10 na kutolewa bure.
Kwa upande wake, Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango Malecela (CCM) alisema ameridhishwa kwa sera hiyo kuagiza watoto kuanza shule ya awali na msingi wakiwa na umri mdogo kwa vile hatua hiyo itawezesha watoto kuanza kujifunza katika umri mdogo na kuwa rahisi kwao kupokea maarifa mapya.
Alisema hata hivyo ni lazima Sera hiyo ikarejesha Mpango wa Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) kwa vile kuondolewa kwa Mpango huo ndiko kulikofanya watoto sasa kumaliza darasa la saba na kuingia kidato cha kwanza wakiwa hawajui kusoma na kuandika.
Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Ummi Mwalimu alisema Sera inapaswa kuboresha mazingira ya mtoto wa kike awapo shuleni akisema hivi sasa watoto wa kike 8,000 wanakatisha masomo kila mwaka kutokana na mimba huku watoto wengine wa kike wakikosa masomo kwa siku saba kutokana na kufuata maji ya kutumia shuleni.
Mbunge wa Peramiho, Jenister Mhagama (CCM) pamoja na kukubaliana na vipengele vya Sera hiyo, lakini alitaka Serikali kutilia mkazo suala la utapiamlo.
Alisema tatizo hilo linasababisha wanafunzi kushindwa kujifunza huku akisema hata kama sera hiyo itakuwa nzuri lakini kama suala la lishe bora halitasisitizwa kwenye sera itakuwa ni kazi bure.
Akitoa majumuisho, Profesa Mchome alisema ufahamu wa lugha kwa wanafunzi wa shule ya msingi, sekondari na vyuo vikuu ni mdogo hivi sasa na kwamba ni wakati muafaka sasa kwa serikali kuwataka watoto kuanza shule wakiwa na umri mdogo ili waweze kuwa na muda mrefu zaidi na mazingira bora ya kujifunza Kiswahili, Kiingereza na nyinginezo na kuboresha elimu.
Masuala mengine yaliyo katika rasimu ya Sera hiyo ya Elimu na Mafunzo ni pamoja na mapendekezo ya kuunganisha elimu ya msingi na sekondari ya kawaida ya sasa ili kuunda elimu-msingi itakayotolewa kwa kipindi cha miaka 10 .
Mambo mengine yanayotarajiwa kutekelezwa na Sera ni kuhuisha mitaala ya sasa ya elimu ili ikidhi muundo mpya wa elimu na mafunzo, kuhuisha sheria na taratibu mbalimbali za utoaji elimu ili ziendane na muundo mpya wa elimu-msingi.
Kuimarisha mfumo wa usimamizi, ithibati na udhibiti wa utoaji wa elimu na mafunzo katika ngazi mbalimbali ili kukidhi malengo na muundo mpya wa elimu-msingi.
Nyingine ni kuongeza ubora wa miundombinu katika shule za sasa za msingi ili kukidhi mahitaji na malengo ya elimu-msingi ikiwa ni pamoja na kuongeza madarasa ya elimu-msingi katika kila shule ya msingi ya sasa, kujenga maabara za sayansi na maktaba katika kila shule ya elimu-msingi.
Kuweka utaratibu utakaohakikisha kuwa wanafunzi wanaomaliza elimu na mafunzo ngazi husika kwa ufanisi na wale wanaokatisha masomo au mafunzo yao kwa sababu mbalimbali, wanaendelea na kuhitimu masomo au mafunzo yao katika mfumo rasmi wa elimu na mafunzo. Jambo jingine litakalotekelezwa ni kutoa elimu kwa umma kuhusu madhumuni, malengo na matarajio ya Sera mpya ya Masuala mengine ndani ya sera ni Kuimarisha matumizi ya Kiswahili na Kiingereza katika ngazi ya elimu – msingi kama lugha za kujifunzia na kuwasiliana.
Rasimu ilieleza kuwa mambo chanja yanayotarajiwa kupatikana baada ya mkakati kutekelezwa ni kuwepo kwa elimu ya awali ya lazima kwa kipindi kisichopungua mwaka mmoja kabla ya kujiunga na elimu msingi, kuwepo kwa elimu msingi ya miaka 10 kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne cha sasa kwa watoto wote wenye rika la kwenda shule.
Matokeo mengine ni kuwepo kwa mfumo nyumbufu, miundo na taratibu za kujiendeleza katika mikondo anuai ya kitaalamu na kitaaluma, kuwepo kwa elimu na mafunzo yenye viwango, ubora na sifa zinazotambulika kitaifa, kikanda na kimataifa.
Kuhusu elimu ya awali, ilieleza kuwa mkakati ni kuweka vigezo, viwango na taratibu ili elimu ya awali iwe ya lazima na itolewe katika kila shule ya elimu – msingi, na kuwa sheria, miongozo na taratibu kuhusu elimu hiyo lazima kuwekwa na kutekelezwa ifikapo mwaka 2018.
Katika elimu msingi, ni kuwa ya lazima kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne, na kutolewa kwa miaka 10 na umri wa kuanza darasa la kwanza kuwa kati ya miaka minne hadi sita kulingana na uwezo wa mtoto kumudu masomo katika ngazi husika.
Rasimu hiyo iliyoandaliwa kwa miaka mitatu, inapendekeza pia Kiswahili kutumika kufundishia katika ngazi zote za elimu na mafunzo nchini. Rasimu ya kwanza imekamilika Machi mwaka huu
Imepita kwa wadau mbalimbali, mashuleni, vyuoni na katika taasisi mbalimbali nchini ambao wametoa maoni yao kabla ya wabunge pia kuipitia jana na kutoa maoni yao.
Baada ya maoni hao ya wabunge, itapelekwa kwa mamlaka husika kwa ajili ya andiko la mwisho kabla ya kupelekwa katika Bunge lijalo ili itungwe sheria kuhusu Sera ya Elimu na Mafunzo.
Mkakati mwingine ni kuweka utaratibu utakaowezesha lugha ya Kiingereza kama lugha ya mawasiliano kikanda na kimataifa kufundishwa kwa ufasaha katika ngazi zote za elimu na mafunzo.
No comments:
Post a Comment