Gaudentia Kabaka. |
Hatimaye Serikali imetimiza ahadi yake ya kuongeza kima cha chini cha mishahara kama ilivyotolewa na Rais Jakaya Kikwete katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani Mei Mosi.
Akihutubia Taifa kutoka uwanja wa Sokoine Mbeya siku hiyo, Rais Kikwete aliahidi unafuu wa maisha kwa wafanyakazi kwa kuangalia uwezekano pia wa kupunguza kodi kwenye mishahara (PAYE).
Kuhusu kuongeza mishahara, Rais aliahidi wafanyakazi wote kwamba Serikali itaendelea kuiongeza kulingana na hali ya uchumi wa nchi.
Akifafanua, alisema pamoja na Serikali kupenda kuongeza mishahara kwa wafanyakazi kwa kiwango cha kuridhisha, lakini lazima izingatie hali ya mapato yake.
Jana, Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudentia Kabaka, aliliambia Bunge, kwamba Serikali imekamilisha majadiliano ya kuongeza kima cha chini cha mshahara katika sekta 12 binafsi, kitakachoanza kutumika rasmi Julai mosi.
Waziri Kabaka alitaja sekta hizo kuwa ni ya Ujenzi, Shule Binafsi, Nishati, Viwanda na Biashara, Hoteli na Huduma za Majumbani, Ulinzi Binafsi, Madini, Afya, Uvuvi na Huduma za Majini, Usafirishaji, Mawasiliano na Kilimo.
“Napenda kulitaarifu Bunge lako tukufu, wafanyakazi na waajiri wote nchini, kuwa kima cha chini cha mshahara katika sekta zote 12 kimeongezeka kwa viwango tofauti,” alisema Waziri Kabaka alipowasilisha hotuba ya makadirio ya matumizi ya wizara yake bungeni jana.
Kwa mujibu wa Kabaka, mishahara imepanda kwa kiwango cha asilimia kati ya 21 na 65 huku Afya ikiongoza kwa kuongezwa ikifuatiwa na sekta ya hoteli na huduma za majumbani yenye asilimia 55.
Akitaja mishahara hiyo mipya, Waziri alisema kima cha chini kwa sekta ya Viwanda na Biashara kimeongezeka kwa asilimia 43.8, Hoteli na Huduma za Majumbani kwa asilimia 55.2, Ulinzi Binafsi asilimia 46.4, Madini asilimia 25.2, Afya asilimia 65, Uvuvi na Huduma za Majini asilimia 21.2, Usafirishaji asilimia 49 na Kilimo asilimia 42.9.
“Aidha sekta nne mpya zilizoanzishwa ambazo ni Ujenzi, Shule Binafsi, Nishati na Mawasiliano nazo vima vya chini vya mishahara vimeongezwa. Viwango hivyo vipya vya kima cha chini vitaanza kutumika Julai na vitatangazwa rasmi katika Gazeti la Serikali,” alisema Waziri.
Alisema nyongeza hizo za mishahara zimezingatia tija na hali ya uzalishaji na utoaji huduma nchini, uwezo wa waajiri na wazalishaji katika kila sekta, mfumuko wa bei na kulinda ajira ili wafanyakazi wasipunguzwe kazi au uwekezaji kuhamishiwa nchi nyingine zenye gharama nafuu ya uzalishaji.
Katika hatua nyingine, Waziri Kabaka alisema Wizara inaendelea na mchakato wa kuanzisha Mfuko wa Fidia kwa wafanyakazi wanaoumia au kupata maradhi wakiwa kazini.
Alisema hatua za kupata watendaji wakuu wa Mfuko huo zinaendelea na unatarajiwa kuanza kazi mwaka wa fedha wa 2013/14.
Kwa upande wake, Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Maendeleo ya Jamii imeshauri kuongeza kiwango cha mishahara kwa kuzingatia hali halisi ya ugumu wa maisha uliopo.
Akiwasilisha maoni ya Kamati hiyo, Mwenyekiti Jenister Mhagama, alisema pamoja na kuongeza viwango vya mishahara, Serikali iangalie pia uwezekano wa kuondoa au kupunguza kodi kwenye mishahara (PAYE) na kuboresha mazingira ya kazi vikiwamo vitendea kazi.
Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni kwa Wizara hiyo, Cecilia Paresso (Viti Maalumu- Chadema) alisema pamoja na ugumu wa mazingira ya kazi, mishahara duni na hali ngumu ya maisha bado mfanyakazi ameendelea kunyonywa kwa kiwango kikubwa cha PAYE.
Aliitaka Serikali ibuni njia nyingine mbadala ya kukusanya mapato ili kuondoa PAYE, ikiwamo kufuta misamaha ya kodi isiyo na tija kwa uchumi wa nchi. Bajeti hiyo ilitarajiwa kupitishwa jana huku Wizara hiyo ikiwa imeomba Bunge kuiidhinishia Sh bilioni 14.9 kwa shughuli zake.
No comments:
Post a Comment