KIKOSI MAALUMU CHAUNDWA KUPAMBANA NA WACHOCHEA VURUGU...

Advera Senso.
Polisi imetangaza kwamba imeunda kikosi maalumu kutoka Makao Makuu kwenda mikoani kushirikiana na makamanda kukamata watu wanaotuhumiwa kuchochea vurugu ikiwemo kutumia ujumbe mfupi wa simu za mkononi.

Jeshi hilo kupitia kwa Msemaji wake, Advera Senso limesema linakamilisha ukusanyaji wa ushahidi wa watu wanaofadhili, wanaosaidia na wanaoshawishi vitendo hivyo wafikishwe mahakamani mapema.
Katika utekelezaji wa azma hiyo, jeshi hilo limeendelea kukamata watu wanaodaiwa kuchochea vurugu kupitia ujumbe mfupi wa simu (sms) baada ya mtu mwingine kukamatwa mkoani Lindi.
Mtu huyo ambaye jina lake halikutajwa, amekamatwa siku chache baada ya mwingine kukamatwa jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki kwa tuhuma za kutuma meseji za uchochezi na kuhamasisha vurugu. Senso alisema mtu huyo atafikishwa mahakamani leo.
Kwa mujibu wa Senso, Polisi inaendelea kukamilisha ukusanyaji wa ushahidi wa watu wanaofadhili, wanaosaidia na wanaoshawishi vitendo hivyo kutekelezwa ili na wao wafikishwe mahakamani mapema.
“Katika kuhakikisha kwamba vitendo hivyo vinakomeshwa na kudhibitiwa hapa nchini, Jeshi la Polisi limeunda kikosi maalum kutoka makao makuu kwenda kusaidiana na makamanda wa mikoa ili kwa kusaidiana na wananchi kuweza kuharakisha ukamataji na watu wote wanaojihusisha na uchochezi wa vurugu na fujo kwa njia ya sms na kwa njia nyingine yeyote ile popote walipo ili waweze kufikishwa mahakamani haraka,” alisema Senso.
Akishukuru wananchi kwa ushirikiano mkubwa wa kutoa taarifa zinazofanikisha operesheni hiyo, ameomba waendelee kuipatia polisi taarifa zaidi na hata za watu wanaofadhili kwa njia ya fedha ama ushauri wachukuliwe hatua.
Alisisitiza, “Jeshi la Polisi linatoa onyo kali kwa mtu yeyote ama kikundi cha watu wanaojihusisha na vitendo hivyo vya uchochezi kuacha mara moja. Aidha, litamkamata mtu yeyote anayejihusisha na vitendo hivyo vya uchochezi bila woga ama upendeleo pasipo kujali cheo, wadhifa, rangi ama umaarufu wa mtu huyo.”
Idadi ya majeruhi waliofikishwa katika Hospitali ya Rufaa ya Ligula kutokana na vurugu za wiki iliyopita, imeongezeka kutoka watu 17 hadi kufikia 30 jana.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Saduni Kabuma aliwaambia waandishi wa habari kuwa majeruhi 13 wameongezeka kati ya juzi na jana.
Kabuma alisema siku ya kwanza ya tukio, hospitali yake ilipokea majeruhi 17, siku iliyofuata waliongezeka tisa na jana wamepokea majeruhi wengine wanne ambao walikuwa wanatibiwa katika zahanati mbalimbali vijijini kabla ya kuhamishiwa hospitalini hapo.
“Baada ya uchunguzi tumebaini baadhi watu majeraha yao yametokana na kupigwa na risasi  na wengine ni wale ambao walipata mshituko kutokana na mabomu,” alisema Kabuma.
Aliwataja baadhi ya majeruhi wa risasi ni Henry Focus (16) anayesoma Darasa la Sita katika Shule ya Msingi Mikindani na kaka yake, Sharks Focus (25) ambao wote wamejeruhiwa miguuni. Mwingine ni Fadina Nahimu (34) ambaye amejerujiwa kifuani.
Kabuma alisema baadhi ya majeruhi hao wametibiwa na kuruhusiwa kurudi majumbani na wengine wameendelea kulazwa wakipatiwa matibabu.
Wiki iliyopita kuzulizuka vurugu kubwa mara baada ya kusomwa kwa Bajeti ya Nishati na Madini. Vurugu hizo ziliazishwa na watu wanaopinga uamuzi wa serikali wa kujenga bomba la gesi kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam, licha ya serikali mara kadhaa kuelezea umuhimu na faida ya bomba hilo kwa uchumi wa Tanzania kwa ujumla.
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda yuko mkoani Mtwara ambako pamoja na kuhudhuria ibada jana ya kumweka wakfu Askofu Mteule wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kusini Mashariki, Lucas Mbedule, leo  anaweka jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa Kiwanda cha Saruji kitakachozalisha mamia ya ajira kwa wakazi wa mkoa huo.
Kiwanda hicho ni cha  Kampuni ya Dangote Industries ya Alhaj Dangote wa Nigeria kitakachokuwa na uwezo wa kuzalisha tani milioni tatu za saruji kwa mwaka au mifuko 150,000. Kitaajiri wafanyakazi 1,000 ndani ya kiwanda na wengine 9,000 wa nje wakiwa ni wakala, wasafirishaji, wajenzi na wauzaji rejareja.
Kuna viwanda vinne vya saruji nchini hivi sasa vyenye uwezo wa kuzalisha tani 3,000 kwa mwaka, ila vinazalisha tani milioni 1.2.
Akizungumza katika ibada hiyo ya kumweka wakfu askofu, Waziri Mkuu aliomba viongozi wa dini zote kuendelea kuhubiri amani, mshikamano na upendo miongoni mwa waumini wa dini zao ili kwa pamoja washirikiane kufanya shughuli za kuwaletea maendeleo.
Alisema ni jukumu la viongozi wa dini kuhakikisha wanahubiri amani kwa waumini wao wakati wote. Alisema  Serikali inatambua mchango wa taasisi za dini katika kuimaisha afya za wananchi kupitia zahanati, hospitali na vituo vya afya wanavyojenga na kuhudumia watu wote bila kujali dini zao.
Alisema kusimikwa kwa Askofu Mbedule kuna maana kubwa ukihusishwa na maendeleo ya kasi yanayotazamiwa katika mikoa ya Lindi na Mtwara kutokana na kugundulika kwa gesi asilia ambayo itawafanya wawekezaji na watu wengine kuvutika kuja Mtwara.
Pinda alisema ni vyema Dayosisi ikajiandaa kuhudumia watu wengi zaidi wanaotazamiwa kuongezeka katika miaka michahe ijayo .
Kwa mujibu wa Pinda, wawekezaji zaidi ya 45 wameomba kuwekeza Mtwara kupitia Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), hivyo ujio huo utazalisha ajira kwa wakazi wa Mtwara na maeneo jirani.
Alisema mbali na hilo, serikali pia inakusudia kuweka kituo cha kuzalisha umeme ambacho kitaajiri wataalamu mbalimbali wapatao 100,000 na hivyo kuongeza idadi ya watu katika Manispaa ya Mtwara ambao kwa sasa hawazidi 150,000 .
 “Kesho(leo) natarajia kuweka jiwe la msingi kwa ajili ya kiwanda cha saruji hapa Mtwara ambapo kitakapokamilika kitazalisha mifuko 150,000 ya saruji kwa siku, ikiwa ni sawa na tani milioni tatu kwa mwaka na kiwanda kitaajiri wafanyakazi elfu moja na watu elfu tisa wataajiriwa kwenye sekta binafsi kutokana na saruji itakayozalisha,” alisisitiza..
Pinda alisema waajiriwa hao ni pamoja na mawakala, wasarifirishaji, wajenzi, wauzaji rejareja na jumla.
Alisema mbali na kiwanda cha saruji pia kutajengwa kiwanda cha mbolea, kiwanda cha bidhaa za plastiki ambavyo vitasaidia kukuza uchumi wa Mkoa wa Mtwara na wanamtwara wenyewe ambao wataweza kujipatia ajira za moja kwa moja lakini pia kwa kufanya shughuli za uzalishaji mashambani watakazoziuza kwa watu walioajiriwa.
Aidha, alisema serikali inafahamu kuwa upo umuhimu mkubwa wa kuleta maendeleo ya nchi kwa uwiano bila kubagua kwa misingi ya jinsia, rangi, kabila, dini, mikoa au ukanda kwani maendeleo ya nchi kwa uwiano ni nguzo muhimu kwa umoja na mshkamano wa wananchi wa taifa kama Tanzania.
Kuhusu tatizo la maji mkoani Mtwara, Waziri Mkuu alisema amemwagiza Waziri wa Maji kuleta wataalamu mkoani humo kuona uwezekano wa kupata maji kutoka mto Ruvuna unaotengaisha Tanzania na Msumbiji.
Aliliahidi kushughulikia maombi ya KKKT kupata ardhi  ekari 30 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha elimu katika wilaya Masasi.

No comments: