KAKA SASA AWEKA SOKONI BARUA ALIZOTUMIWA NA RAIS BARACK OBAMA...

KUSHOTO: Moja ya barua hizo. KULIA: Malik Obama.
Mmoja wa kaka aliyechangia baba na Rais Obama sasa anauza karatasi mbili za barua alizopokea kutoka kwa ndugu yake huyo maarufu na kuziuza kwa Dola za Marekani 15,000 kila kimoja.

Karatasi hizo mbili zote zimeandikwa kwa kutumia karatasi za kiofisi za Ikulu ya Marekani na vina ujumbe unaofanana japo zimetumwa kwa makundi mawili ya watu tofauti.
"Thanks for your prayers and support," (Yaani nashukuru kwa sala zenu na ushirikiano wenu), barua hizo zilisomeka, huku akisaini kwa vifupisho vya majina yake 'B.O.'
Barua hizo zilitumwa na Rais huyo muda mfupi baada ya wakenya wenzake kusafiri kutoka Afrika kwenda Washington D.C. Januari 2009 kuhudhuria kuapishwa kwake.
Imeripotiwa kwamba kaka wa Barack, Malik Abongo Obama, ambaye amechangia baba na rais huyo, alifuatwa na Gary Zimet, mkusanyaji wa Marekani, ambaye alitaka kuona kama Malik alikuwa na barua yoyote inayoweza kupigwa mnada.
Zimet alituma barua kwa malik, bila kufahamu kama angepata majibu yoyote kutoka kwake.
"Nilishangazwa pale nilipopata majibu. Nilituma barua kwenye ofisi ya posta nchini Kenya," alieleza Zimet.
"Nilimuuliza kama alikuwa na barua yoyote kutoka kwa kaka yake. Sikutarajia hata kidogo kupata majibu kutoka kwake, lakini aliniandikia kunijibu na alisema, "Ninazo barua mbili."
Moja ya barua hizo ilitumwa kwa watu wa K'Obama, ambao wanajumuisha familia kubwa ya Obama, na nyingine kwa K'Olego, ambayo Malik anaelezea kuwa ni wanafamilia wa ukoo wao.
Zimet alieleza kwamba alituma barua hizo kwa ajili ya kuuzwa katika mtandao mapema Jumatano asubuhi hivyo bado anasubiria majibu kutoka kwa yeyote mwenye nia ya kuzinunua, lakini anatarajia barua hizo zitauzika kwa haraka zaidi.
"Nina hakika siku chache zijazo zitatoa mwanga wingi wa maombi ya kununua," alisema, akirejea 'uhaba wa barua alizoandika Obama kwa mkono wake' kuwa ni kivutio kikubwa.
Hapo kabla aliuza barua nyingine 13 zilizoandikwa na Rais huyo wakati akiwa Ikulu, na hivi sasa anayo moja sokoni ambapo Obama anamwandikia mwanamke kuhusu mpango wake wa afya, inayoitwa 'Obamacare'.
Malik alieleza kwamba yeye na kaka yake huyo mashuhuri wanaonana zaidi kuliko ilivyodhaniwa hapo awali.
"Namwona kaka yangu faragha walau mara moja kwa mwaka, wakati ninapokwenda kumtembelea katika Ikulu na kumsalimia.
Ni kama vile kutembelea makumbusho ya taifa, kama vile Smithsonian au Buckingham Palace," alisema mwezi Machi.
"Mara ya mwisho nilimwona Novemba 19, mwaka jana, muda mfupi baada ya uchaguzi wa Marekani. Nilikwenda Ikulu na kumpa pongezi zangu.
"Tuko karibu lakini hatuishi mifukoni mwa kila mmoja. Sihitaji kuwapo kwenye kila sherehe kubwa. Sijaonana na Michelle kwa kipindi kirefu. Siwezi kusema nina mahusiano na watoto wa ndugu yangu huyo."

No comments: