Benki nne nchini zimeingia mkataba wa kukopesha nyumba zinazojengwa na kuuzwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) hivyo kufanya idadi ya benki zinazotoa huduma hiyo kufikia 12.
Pia Kampuni ya Bima ya MGen Tanzania, imeingia mkataba na NHC ili kuzipa benki hizo, uhakika wa fedha zao kurejeshwa hasa kutoka kwa Watanzania wa kipato cha chini.
“Tunajua benki hizi nyingi zinatoa riba kubwa, kiasi kwamba Mtanzania wa kawaida anashindwa kumudu, sisi kampuni ya bima, kazi yetu ni kumwekea bima Mtanzania huyu wa chini kiwango ambacho hatashindwa kukilipa kwa muda tutakaokubaliana, ili aweze naye kumudu kununua nyumba hizi,” alisema Mkurugenzi Mkuu wa MGen Tanzania, Charles Sumbwe.
Benki zilizoingia mkataba huo jana Dar es Salaam ni DCB, CRDB, ABC na NIC chini ya mradi wa kujenga na kukopesha nyumba. Benki nane ambazo tangu awali ziliingia mkataba huo na NHC ni NMB, NBC, KBC, Exim, CBA, BOA na Azania.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Felix Maagi, alisema kutokana na mafanikio iliyopata katika mradi wa ujenzi wa nyumba, shirika linatarajia ifikapo Desemba, itajenga nyumba za bei nafuu katika mikoa yote nchini.
Maagi, alisema kuongezeka kwa benki hizo kunatoa fursa na wigo mpana kwa Watanzania kupata kirahisi mkopo wa nyumba hizo.
“Awali tuliingia mkataba na benki nane ambazo tumefanya nazo kazi kwa kipindi kirefu tangu mradi huu uanze, kuongezeka kwa benki hizi nne kunafanya tuwe na benki 12, ambazo zitafanya kazi kwa ushindani na kuweka wigo mpana kwa Watanzania wengi kupata mikopo ya nyumba,” alisisitiza Maagi.
Maagi ambaye pia ni Mkurugenzi wa Fedha wa Shirika hilo, alisema kwa sasa shirika linaendelea kutekeleza miradi ya ujenzi na mingi iko katika hatua za mwisho ikiwamo ya Dodoma, Kibada, Ubungo, Mchikichini na Upanga (Dar es Salaam).
Aidha, alisema ipo miradi mingine inaendelea katika mikoa 14 iliyo katika hatua mbalimbali za kukamilika na ikikamilika mchakato wa mikopo na ununuzi itaanza kupitia benki hizo.
Alisema hadi sasa shirika limepokea maombi ya Watanzania 125 wanaotaka kukopeshwa nyumba na kati yao 37 wameshapatiwa mikopo yenye thamani ya Sh bilioni 6.3 na waliobaki, bado wako kwenye mchakato.
Akizungumzia ujenzi wa nyumba za bei nafuu, Maagi alisema shirika linatambua uwezo tofauti wa kifedha walionao Watanzania na kwa sasa wanajenga nyumba zenye gharama tofauti, ambapo ya bei ya juu inaanzia Sh milioni 300 na ya gharama nafuu inafikia Sh milioni 40.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka akiwasilisha bajeti ya Wizara yake jana bungeni alisema ili kuwezesha upatikanaji wa mikopo ya nyumba, taasisi ya Tanzania Mortgage Refinancing itaanza kukopesha benki hata kabla benki hizo hazijatoa mikopo.
“Lengo ni kuzipatia benki mtaji wa kukopesha kwa muda mrefu. Ninatoa mwito kwa benki za biashara ambazo hazijaanza kutumia chombo hiki, zikitumie na kutoa mikopo ya nyumba yenye riba nafuu kwa wananchi.”
Kuhusu hati za kimila, Waziri alitoa mwito kwa wananchi kushirikiana na halmashauri zao kuhakiki na kupima maeneo yao na kuzipata, akisema zina manufaa ikiwamo kuwawezesha kuzitumia kama dhamana ya mikopo benki na kuepusha migogoro ya ardhi.
“Sina budi kuzishukuru benki ambazo zimetambua kwamba hati za kimila zinaweza kutumika kuchukua mikopo. Hapo hapo ninazihimiza benki na taasisi nyingine za fedha kutoa ushirikiano na kutambua kuwa hati za kimila zina nguvu za kisheria kutumika kama dhamana,” alisema Waziri Tibaijuka.
Katika hatua nyingine, wageni kutoka nchi jirani wanadaiwa kujipenyeza nchini na kumiliki ardhi kwa njia za udanganyifu wakisaidiwa na wananchi na viongozi wasio na maadili, jambo ambalo Serikali imesema haitalivumilia.
Waziri Tibaijuka alisema ni dhahiri kwamba kuwapo kwa ardhi ya kutosha Tanzania kumezusha changamoto hiyo ya kufanya wageni kujipenyeza na kumiliki ardhi kinyemela.
“Nasisitiza, kwamba wenye tabia hiyo waache mara moja maana wakibainika, hawatavumiliwa kamwe na sheria itafuata mkondo wake,“ alisema Waziri Tibaijuka.
Alisema zipo njia sahihi za kuhudumia wageni wenye nia ya kupata ardhi nchini na kwamba viongozi wanaowasaidia kupindisha sheria hiyo ili kujipatia ardhi hawatavumiliwa.
Kuhusu kuanzishwa kwa Hazina ya Ardhi, Waziri alisema kwa mwaka 2012/13, wizara iliahidi kuanzisha chombo cha kusimamia hazina ya ardhi na kuanzisha Mfuko wa Fidia ya Ardhi.
Alisema wizara kwa kushirikiana na wadau wengine inaendelea kutekeleza ahadi hiyo na taratibu zitakapokamilika itawasilisha muswada wa sheria ya kuanzishwa rasmi vyombo hivyo.
“Ninarudia kuliomba Bunge lako tukufu kuendelea kuunga mkono utaratibu mpya wa kutoa ardhi kwa wawekezaji kwa msingi wa kugawana hisa utakaofuata taratibu zinazotumiwa na halmashauri na vijiji kwa sasa za kupewa gawiwo lisilozingatia misingi ya kiuchumi,” alisema na kutolea mfano wa wawekezaji kutoa zawadi ndogo kama visima vya maji, madarasa, barabara za vumbi na zahanati.
Akisoma maoni ya Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, Mjumbe wa Kamati hiyo, Dk Mary Mwanjelwa (Viti Maalumu – CCM) alisema Kamati inaishauri Serikali kutatua migogoro kwa kuendelea kuelimisha wananchi kuhusu maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya uwekezaji.
“Sambamba na hilo, Kamati inaishauri Serikali kuhakikisha mchakato wa kuanzisha utaratibu wa kuwa na ardhi huru kwa ajili ya matumizi ya Serikali na ardhi ya akiba kwa ajili ya matumizi ya wawekezaji wa ndani na nje ya nchi,” alisema Dk Mwanjelwa.
Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Halima Mdee (Kawe – Chadema), alisema ingawa karibu kila eneo limevutia wawekezaji wa aina fulani katika ardhi, lakini maeneo ya uchimbaji madini, shughuli za wanyama pori kama vile uwindaji, hoteli na utalii na maeneo ya kilimo, zimeonekana kukimbiliwa zaidi na wawekezaji na kuitaka Serikali kuwa makini.
No comments:
Post a Comment