MEJA JENERALI MAKAME RASHID WA JKT AFARIKI DUNIA...

Meja Jenerali Makame Rashid.
Aliyewahi kuwa Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Meja Jenerali mstaafu Rashid Makame (69), amefariki jana jijini Dar es Salaam, katika Hospitali ya Lugalo alikokuwa akipatiwa matibabu.

Msemaji wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Kanali Kapambala Mgawe, alithibitisha kuwepo kwa msiba huo na kuongeza kuwa alifariki saa 12:30 asubuhi hospitalini hapo.
Alisema msiba upo nyumbani kwa marehemu eneo la Mikocheni, jirani na nyumbani kwa Mwalimu Julius Nyerere.
Meja Jenerali Makame alijiunga na JKT mwaka 1994, ambako  alishika nyadhifa mbalimbali hadi mwaka 2001, alipostaafu kazi hiyo.
Miongoni mwa nafasi alizowahi kushika ni kuwa Mkuu wa Kikosi cha Ruvu na Mnadhimu wa Mafunzo Makao Makuu ya Jeshi.
Msemaji wa familia, Mshamu Selemani alisema Makame alikuwa akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Lugalo kwa miezi mitatu, kutokana na kusumbuliwa na miguu na maradhi ya kupooza.
Alisema anatarajiwa kuzikwa keshokutwa katika Kijiji cha Mlyawa, Tandahimba mkoani Mtwara saa 7:00 mchana.
Aidha dua ya kumuombea marehemu, itafanyika kesho mchana katika viwanja cha Karimjee na  baadaye mwili utasafirishwa.

No comments: