ASKARI MAGEREZA 'ALIYEINGIZA' HEROIN JELA KUPANDISHWA KIZIMBANI...

Kamanda Godfrey Nzowa akionesha baadhi ya kete za dawa za kulevya zilizokamatwa.
Askari Magereza namba B7942, Brighton Octavian, anayeshikiliwa Polisi Temeke, kwa tuhuma za kuingiza dawa za kulevya gerezani, anatarajiwa kufikishwa mahakamani wakati wowote.

Tayari jalada lake limefikishwa kwa Kamanda wa Kikosi cha Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya, Godfrey Nzowa.
Akizungumza na mwandishi kwa njia ya simu jana, Kamanda Nzowa alisema jalada hilo limefikishwa ofisini kwake kwa hatua zaidi za kisheria.
Alisema kwa sasa wanaendelea na upelelezi, ili kufahamu ni aina gani za dawa na za uzito gani, na hatimaye atafikishwa mahakamani baada ya uchunguzi huo kukamilika.
Octavian anashikiliwa kwa tuhuma za kupatikana na kete 372 za heroin na simu mbili za mkononi alizokuwa akiziingiza katika Gereza la Keko.
Inadaiwa askari huyo alikamatwa saa 4, usiku akiwa na  dawa hizo zenye thamani ya Sh milioni 1.5, simu mbili za mkononi na chaja moja.
Chanzo chetu cha habari kilidai kwamba askari huyo, ambaye ana miezi minne tangu aajiriwe baada ya kumaliza mafunzo, alifunguliwa jalada namba RB 3105/13, katika kituo cha Polisi Chang’ombe.
Mtoa habari alisema mchezo wa kuingiza simu gerezani ni wa kawaida, na anayeingiza simu, hulipwa na mahabusu au wafungwa hata Sh 250,000 ambazo hata hivyo, hakufafanua wanazipataje.

No comments: