ASKARI ABAMBWA AKIINGIZA KETE 372 ZA HEROINE GEREZA LA KEKO...

Askari Magereza mwenye namba B7942, Brighton Octavian, anashikiliwa na Polisi Temeke, kwa tuhuma za kuingiza dawa za kulevya aina ya Heroine na simu za mkononi katika gereza la Keko.

Askari huyo alikamatwa juzi saa 4, usiku akiwa na kete 372 za Heroine zenye thamani ya Sh milioni 1.5 pamoja na simu mbili za mkononi pamoja na chaji moja.
Chanzo chetu cha habari kilidai jana kwamba askari huyo, ambaye ana miezi mine tu tangu aajiriwe baada ya kumaliza mafunzo, alifunguliwa jalada lenye RB 3105/13, katika kituo cha Polisi Chang’ombe.
Mtoa habari wetu alisema mchezo wa kuingiza simu gerezani ni wa kawaida, na askari Magereza anapoingiza simu, hulipwa na mahabusu au wafungwa mpaka Sh 250,000 ambazo hata hivyo, hakufafanua wanazipataje.
Kamanda wa Polisi wa Temeke, Engelbert Kiondo, alithibitisha kukamatwa kwa askari huyo, na kusema kuwa taarifa zaidi atazitoa leo.
“Ni kweli tunamshikilia mtuhumiwa huyo na taarifa zaidi za tukio hilo nitazitoa nitakapopata jalada kwa kuwa kwa sasa limefungiwa katika ofisi ya Ofisa Upelelezi wa Wilaya,” alisema.
Wakati huo huo, askari watano wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ), kutoka kambi ya Lugalo iliyopo Kawe, wanashikiliwa na Polisi Kinondoni kwa tuhuma za mauaji ya dereva wa Bajaj, Yohana Cyprian (20).
Hata hivyo Kamandaa wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela, alipozungumza na vyombo vya habari jana, alikataa kuwataja majina watuhumiwa hao, kwa madai kwamba bado wanaendelea na upelelezi wa tukio hilo.
Machi 3 mwaka huu, saa 9 alasiri eneo la Mbezi Beach Kwa Mboma, watu hao wanadaiwa kumshambulia dereva huyo sehemu mbalimbali za mwili wake hadi kumuua.
Inadaiwa wanajeshi hao, wanajeshi hao kabla ya kumshambulia dereva huyo, walishiriki katika purukushani katika kijiwe kinachotuhumiwa kutumika kwa uvutaji bangi.
Chanzo cha purukushani hizo, inadaiwa ni baada ya   askari mgambo Revenary Anatory(40), kuwafuata wanajeshi hao, ili wamsaidie kukamata vijana waliokuwepo katika kijiwe hicho.
Mgambo huyo anadaiwa kuwatuhumu vijana hao   kumpora simu mmoja wa wanajeshi, usiku wa jana yake.
Inadaiwa kuwa mara baada ya wanajeshi hao kufika katika eneo hilo, watu waliokuwepo walikimbia na  wanajeshi  hao wakaamua kuwakimbiza na kufanikiwa kumkamata Cyprian.
Aidha, Cyprian mwenyewe anadiwa hakuwepo katika eneo la tukio, wala hakuhusika na uporaji wa simu.
“Hadi sasa tunawashikilia watuhumiwa watano kutokana na tukio hilo, baadhi yao wakiwemo askari wa JWTZ, lakini kwa kuwa upelelezi wa shauri bado unaendelea, na ili kulinda mtiririko wa ushahidi na chanzo cha mauaji, kwa sasa tunahifadhi majina yao,” alisema Kenyela.
Alisema endapo ushahidi utabainisha uhusika wao katika tukio hilo, watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili kwa mujibu wa Katiba ya Jamuhuri ya
Kuhusu watuhumiwa 12 waliodaiwa kuleta vurugu katika Kituo cha Polisi cha Kawe siku hiyo ya tukio, na kusababisha askari watatu kujeruhiwa kwa mawe, Kenyela alisema walitarajiwa kufikishwa mahakamani jana kujibu tuhuma zinazowakabili.
Aidha kwa upande wake Msemaji wa JWTZ Kanali Kapambala Mgawe, alisema licha ya kutokuwa na taarifa rasmi za kukamatwa kwa wanajeshi hao, Jeshi hilo halina kipingamizi cha aina yoyote cha kukamatwa kwao kwa vile Polisi na jeshi wana utaratibu wa kushirikiana pamoja katika matukio mbalimbali.
Kwa mujibu wa Kanali Mgawe, ikithibitika kuwa kweli wanajeshi hao wamehusika na tukio hilo, watachukuliwa hatua za kinidhamu zinazoendena na sheria na taratibu za majeshi ya ulinzi, kwa lengo la kulinda maadili ya jeshi hilo.
Hata hivyo alisema anasubiri taarifa rasmi kutoka Polisi, ili wajue hatua zipi waanze kuzichukua na kujua kiini cha wanajeshi hao kufanya mauaji hayo, aliyosema kuwa ni kinyume taratibu zinazoliongoza jeshi hilo.

No comments: