AMBAYE HAKUSOMEA UUGUZI AWACHOMA SINDANO WAGONJWA MASASI...

Chumba cha sindano.
Mwanakijiji anayedaiwa kutokua na ujuzi wa uuguzi, anadaiwa kutibu katika zahanati mojawapo wilayani Masasi katika Mkoa wa Mtwara, baada ya kuombwa na muuguzi amsaidie kufanya kazi hiyo.

Anadaiwa kuchoma sindano na kutoa dawa kwa wagonjwa katika Zahanati ya Mbuyuni, Kata ya Chiungutwa licha ya kwamba hakusomea kazi hiyo.
Taarifa hiyo ilitolewa jana katika Kongamano la Kitaifa la Wanawake, lililoandaliwa na  Muungano wa Mashirika ya Kutetea Masuala ya Jinsia, linalofanyika mjini Dodoma.
Mmoja wa washiriki , Kidawa  Hassan alisema muuguzi huyo ambaye ni mwanamke wa mtaani, wanamfahamu miaka mingi na wanashangazwa kumuona akifanya kazi kwenye zahanati.
“Kila mtu anashangaa suala hilo, kwani hana ujuzi wowote na  watu wanafahamu elimu yake ni ya msingi  na kazi zahanati ameanza miezi mitatu iliyopita,” alisema Hassan.
Alisema baada ya wanakijiji kuuliza   alipataje kazi mahali hapo, waliambiwa kuwa alikuwa ameombwa na muuguzi mmoja wa zahanati hiyo, amsaidie kazi za hospitalini hapo.
Alisema  wakazi wa kijiji hicho, wamekuwa wakipata madhara, kwani amekuwa akichoma sindano ambazo zinafanya watu wachechemee.
“Kuna ndugu yangu alishawahi kuchomwa sindano na muuguzi huyo na alipokwenda hospitali kubwa, ikaonekana kuwa alichomwa kwenye sehemu isiyostahili, tunaomba tusaidiwe katika hili kwani wananchi wanapata madhara,” alisema.
Akijibu madai hayo, Mbunge wa Viti Maalumu, Anna Abdallah alieleza kusikitishwa na taarifa hiyo na aliahidi kufuatilia.
“”Hilo ni kosa kubwa kwani afya ya mtu huwezi kuichezea, lakini tutalifikisha suala hilo kwa Mbunge ili liweze kufuatiliwa na kuchukuliwa hatua, kwani ni bora kuacha kutoa huduma kuliko kucheza na uhai wa mtu,” alisema.
Alisema kuwa hilo ni kosa la jinai ambalo mtu anaweza kufungwa, kwani haiwezekani mtu asiye na taaluma kuwekwa kwenye zahanati ili kuweza kusaidia kutoa huduma za afya.
“Lazima suala hilo lifuatiliwe na hatma yake ijulikane” alisema Abdallah.
Hata hivyo, wanawake  hao walitaka taarifa hizo zisizagae,  kwani muuguzi huyo  anaweza kukimbia na kupoteza ushahidi, bali watu waondoke kimya kimya ili waweze kumkamata.

No comments: