AJIRA LUKUKI ZATANGAZWA SEKTA YA AFYA...

Celina Kombani.
Serikali inatarajia kuajiri watumishi wa afya 5,000 nchini, ambao wataanza kazi Mei Mosi mwaka huu.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Celina Kombani, alisema jana kwamba wiki hii vibali vya ajira za watumishi hao wapya vitatoka.

“Mwakani tutaajiri watumishi wengine wa afya 11,000 na sehemu kubwa ya watumishi hao wapya wa mwaka huu na mwakani itakwenda vijijini,” alisema Kombani.
Alitoa maelezo hayo wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Chunya, Victor Mwambalaswa (CCM), aliyetaka kufahamu ni lini zahanati zilizokamilika kwa muda mrefu, zitapewa watumishi wa afya.
Wakati huo huo katika swali la msingi, Mbunge wa Mufindi Kusini, Menrad Kigola (CCM), alihoji ni lini Serikali itamaliza ujenzi wa vituo vya afya vya Mtwango, Mninga, Mgololo na Bumilayinga katika jimbo lake.  
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Aggrey Mwanri, alisema Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi imeomba idhini ya Sh milioni 420.5 kupitia Mpango wa Maendeleo ya Afya ya Msingi (MMAM), ili kuendeleza ujenzi wa vituo vya afya, zahanati na nyumba za watumishi.
“Hata hivyo leo (jana) nimezungumza na Mkurugenzi wa Halmashauri na hivi vituo alivyotaja mbunge havipo, sasa katika halmashauri yenu angalieni upya vipaumbele vyenu,” alisema Mwanri.
Ujenzi wa vituo vya afya vya Mtwango, Mninga, Mgololo na Bumilayinga, ni miongoni mwa miradi ya afya 21 iliyoibuliwa na wananchi wa Mufindi Kusini, zikiwamo zahanati 17 na vituo vya afya vinne. Sehemu kubwa ya ujenzi umechangiwa na wananchi.

No comments: