REKODI NZURI YA ZANZIBAR YAZIDI KUCHAFUKA KWA MAUAJI...

Kanisa la Minara Miwili lililoko eneo la Shangani, ambalo lilikuwa kituo cha kazi cha Padri Evaristus Mushi.
Padri wa Kanisa Katoliki la Minara Miwili liliopo Mji Mkongwe wa Zanzibar, Evaristus Mushi (56), ameuawa   kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana. 
Mauaji hayo yamefanyika jana saa moja asubuhi, wakati Padri Mushi akijitayarisha kuingia kanisani kuongoza ibada katika Kanisa la Mtoni lililopo nje kidogo ya Mkoa wa Mjini Magharibi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Aziz Juma, amethibitisha kutokea kwa mauaji hayo na kusema  Polisi imeanzisha upepelezi, kutafuta chanzo cha mauaji hayo na kuwakamata wahusika.
“Tumepata taarifa za kifo cha Padri Mushi, Polisi imeanza kufanya msako wa kuwatia mikononi watuhumiwa wa mauaji hayo,” alisema Azizi.
Baadhi ya watu walioshuhudia mauaji hayo, wamedai   Padri Mushi alikuwa anajiandaa kuingia kanisani kuongoza ibada katika Kanisa la Mtoni.
Walidai alipofika katika kanisa hilo, aliegesha gari lake  ndipo walipokuja watu wakiwa na gari na kuanza kumfyatulia risasi na kukimbia.
“Hatufahamu ni watu wa aina gani, tulisikia mlio wa risasi na tukaona gari inakimbia kwa mwendo wa kasi,  kuangalia katika gari ndogo, tukaona damu, kumbe Padri tayari ameuawa,” alisema mtu mmoja jirani na Kanisa hilo.
Hata hivyo, taarifa zingine zilidai kuwa Padri Mushi aliuawa wakati akiendesha gari hilo karibu na Kanisa la Mtoni na si kwamba alishafika na kuegesha gari lake.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyotangazwa katika moja ya redio nchini, watu wasiojulikana wakiwa katika gari ambalo pia halijatambuliwa, walimsimamisha Padri Mushi wakati akiendesha gari lake, alipokaribia Kanisa la Mtoni.
Taarifa hiyo ilisema wakati Padri Mushi akisimama, watu hao walimpiga risasi ya kichwa na gari lake liliserereka na kugonga gari lingine kwa nyuma.
Baadhi ya wasamaria wema, walimkimbiza Padri Mushi   katika Hospitali ya Mnazi Mmoja kwa uchunguzi zaidi, ambapo madaktari walithibitisha kwamba tayari amefariki dunia, kutokana na majeraha ya kupigwa risasi yaliyosababishwa na apoteze damu nyingi.
Majonzi makubwa yalitawala katika Kanisa la Minara Miwili liliopo Shangani Mji Mkongwe, ambapo waumini waliokuwa wakisali, walilazimika kusitisha ibada mara baada ya kupata taarifa ya kifo cha Padri Mushi.
Hilo ni tukio la tatu la kushambuliwa kikatili kwa viongozi wa dini na la pili kwa kiongozi wa Kanisa Katoliki.
Novemba Mwaka jana, Katibu wa Mufti wa Zanzibar, Shehe Fadhil Suleiman Soraga, alimwagiwa tindikali na mtu asiyefahamika iliyomwathiri sehemu kubwa ya mwili wake.
Shehe Soraga alimwagiwa tindikali hiyo karibu na nyumba yake Mwanakwerekwe, saa 12 asubuhi wakati alipokuwa akifanya mazoezi ya viungo muda mfupi baada ya kumaliza swala ya Alfajiri.
Baada ya tukio hilo, Shehe Soraga alisafirishwa hadi Dar es Salaam ambako alilazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Wakati kukiwa na sintofahamu kuhusu shambulio hilo, Desemba mwaka jana  Padri Ambrose Mkenda wa Kanisa Katoliki, mjini Zanzibar, alipigwa risasi na watu wasiojulikana nje ya nyumba yake  saa 1:45 jioni wakati akitokea kanisani.
Mkenda ambaye ni Paroko wa Parokia ya Mpendae, alipigwa risasi begani na shingoni na  baadae alisafirishwa kwa ndege kwenda Dar es Salaam ambako alilazwa katika chumba cha Wagonjwa Wanaohitaji Uangalizi Maalumu (ICU), katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Matukio ya uhalifu wa kutumia sialaha na kemikali kali,  yamekuwa yakijitokeza mara kwa mara katika siku za hivi karibuni, ambapo Polisi imeshakiri kuwepo kwa uingizaji wa silaha katika njia mbali mbali, ikiwemo bandari bubu ziliopo Unguja na Pemba.
Wakati Bandari ya Malindi ndiyo inayotambuliwa rasmi  kwa ajili ya uingizaji wa abiria na mizigo, kuna zaidi ya bandari bubu kumi katika Mkoa wa Mjini Magharibi, zinazotumia kuingiza mizigo na abiria kutoka Tanzania Bara hasa kutoka Bagamoyo na Tanga.

No comments: