MGOGORO WAOTA MIZIZI KANISA LA MORAVIAN...


Ujumbe wa Kanisa la Moravian Duniani (Unity Board), umesikitishwa kwa jinsi mgogoro katika Jimbo la Misheni Mashariki unavyoota mizizi siku hadi siku, badala ya kumalizika na umesema hali hiyo inalivuta Kanisa kwenye mavumbi, uchafu na ni aibu.
Mgogoro huo ulioibuka takribani mwaka mmoja sasa, ulianza baina ya viongozi baada ya baadhi ya wajumbe wa Halmashauri Kuu chini ya Makamu Mwenyekiti wa Jimbo hilo, Mchungaji Sauli Kajula kutangaza kumvua madaraka Mwenyekiti wa Jimbo, Mchungaji Clement Fumbo kwa madai ya ufisadi na kukiuka Katiba.
Ujumbe huo ulizitaka pande mbili zinazopingana, ambazo sasa zimegawa hata waumini, kumtazama Mungu aliyewaita katika utume, kufuata Katiba ya Kanisa na kumwomba kwa bidii ili suluhu ipatikane na Kanisa lirejee katika hali ya amani.
Mtendaji Mkuu wa Kanisa la Moravian duniani, Mchungaji Dk Jorgen Boytler alisema hayo juzi, Dar es Salaam, alipozungumza na waumini wa jimbo hilo kutoka sharika mbalimbali katika Usharika wa Tabata, kabla ya kupokea maoni yao ya jinsi ya kumaliza mgogoro huo. Alifuatana na Makamu Mwenyekiti wa Moravian duniani, Mchungaji Nosigwe Buya.
Akieleza namna uongozi wa Moravian duniani unavyosononeshwa na mgogoro huo, Dk Boytler alisema, “Ninawapa salamu kutoka uongozi wa Moravian duniani, wamenituma niwaeleze kuwa jambo hili si la Dar es Salaam pekee bali dunia nzima, Unity inasikitishwa kwa hali hii na inaomba mumtangulize Mungu mbele.
“Kanisa la Moravian lilianzishwa mwaka 1457, wapo watu waliopoteza maisha kwa kazi ngumu ya umisionari wakati ule na kazi yao inapaswa kuwa faida leo, lakini sasa ni kama Kanisa linavutwa kwenye mavumbi na uchafu, ndiyo maana tuko hapa kupokea maoni yenu ya namna ya kumaliza mgogoro huu,” aliongeza Boytler.
Kuhusu uvumi uliosambazwa kuwa barua ya ujumbe huo iliyotumwa Februari 6 ikizuia wachungaji 16 waliotangazwa kufukuzwa na Mchungaji Clement Mwaitebele wa Jimbo la Kusini ambalo ni mlezi wa Jimbo la Mashariki, haikuandikwa na Unity Board bali watu wanaomwunga mkono Fumbo, Dk Boytler alikiri mbele ya waumini hao kuwa ndiye aliyeandika barua hiyo.
Mchungaji Buya alisema kusudi lao kuja nchini ni moja; kupokea maoni ya waumini na kuyafikisha kwa uongozi wa juu wa Kanisa hilo duniani, ili kuchukua hatua, lakini alisisitiza kuwa suluhisho la mgogoro huo liko mikononi mwa waumini wa jimbo hilo.
“Jambo hili ni mwendelezo wa mikutano tuliyokaa mwishoni mwa mwaka jana na mapema mwaka huu, leo (juzi) ni siku ya mwisho kukusanya maoni yenu, hatujaleta dawa ya mgogoro, dawa mnayo ninyi ila wakati haya yanafanyika, tafadhali msipelekane Polisi wala mahakamani, mwekeni Mungu mbele,” alisema Buya.
Wakati mkutano huo ukiendelea Tabata, upande wa Mchungaji Kajula ulikuwa na kongamano la maombi ya amani kwa Taifa na mgogoro huo, katika Ushirika wa Temeke. Ingawa hawakutoa kauli yoyote lakini awali walishaeleza msimamo wa kutoutambua uongozi wa Mchungaji Fumbo.
Akisoma mapendekezo ya waumini kuhusu namna ya kumaliza mgogoro, Mkuu wa Idara ya Mawasiliano na Uhusiano wa Jimbo hilo, Mchungaji Emmaus Mwamakula, aliuomba uongozi huo wa dunia kuchukua uamuzi mgumu katika suala hilo, kwa kuwa waumini wanateseka, wakiwemo baadhi ya wachungaji wanaonyimwa posho kwa kuwa upande wa Mchungaji Fumbo.
“Itakumbukwa, kwamba mgogoro ulianza baada ya baadhi ya wajumbe wa Halmashauri Kuu kuitisha Sinodi batili iliyotangaza kumpindua Mchungaji Fumbo, jambo lililopingwa na mabaraza na waumini wengi, hivi sasa baadhi yao wanaishi kwa vitisho na baadhi ya sharika tumesitisha kupeleka fedha kwenye Sanduku la Umoja,” alisema Mwamakula.
Aliiomba Unity iharakishe kutafuta ufumbuzi wa suala hilo ikiwa ni pamoja na kuharakisha kulifanya kuwa jimbo kamili kwa kuwa zaidi ya sharika 15 kati ya 28 za jimbo na vituo vitano na waumini wengi wako upande wao na hawana imani na malezi ya Jimbo la Kusini kwa kuwa lina maslahi katika mgogoro huo.
Wakati tukienda mitamboni, taarifa kutoka London, Uingereza zilisema Kadinali Keith O'Brien, ambaye ni kiongozi wa juu wa Kanisa Katoliki nchini humo,ametangaza kujizulu uaskofu mkuu kutokana na tuhuma za tabia mbaya na kusema hatashiriki mchakato wa kuchagua mrithi wa Papa Benedict XVI.
Kadinali huyo alisema jana kwamba hatahudhuria mkutano huo wa mchakato, kwa sababu hataki vyombo vya habari  vijielekeze zaidi kwake katika kipindi hicho muhimu mjini Roma, Italia.
Wataalamu walisema uamuzi huo wa kutohudhuria mchakato huo haukutarajiwa; kwa sababu haijapata kutokea huko nyuma Kadinali asishiriki kwa sababu ya kashfa binafsi, kwa mujibu wa mwanahistoria wa Vatican,  Ambrogio Piazzoni, ambaye ni Makamu Msimamizi wa Maktaba ya Vatican.
Vatican ilithibitisha jana, kwamba O’Brien amejiuzulu uaskofu wa Mtakatifu Andrea na Edinburgh. Inakubalika chini ya sheria za kidini kutokana na umri wa O’Brien ambaye Machi 17 atafikisha miaka 75-ambao ni wa kawaida kustaafu uaskofu.
Alisema hana afya mbaya na kwamba alitangaza kujizulu Novemba mwaka jana. Taarifa ya Kanisa ilisema Papa alikubali kujiuzulu huko Februari 18.
“Nikirudi nyuma katika miaka yangu ya utumishi: Kwa mema ambayo niliweza kufanya, namshukuru Mungu. Kwa upungufu uliotokea, naomba radhi kwa wote niliowakosea,” alisema O’Brien. Papa Benedict XVI anatarajia kung’atuka rasmi Februari 28.

No comments: