MAPADRI ZANZIBAR WALILIA ULINZI MADHUBUTI...

Msalaba ukiwekwa kwenye kaburi la Padri Evaristus Mushi, juzi.
Viongozi wa dini ya kikristo visiwani hapa wameomba ulinzi katika taasisi zao huku baadhi yao wakisema  wanaendelea kupokea vitisho wakitakiwa waache kuendelea kutoa huduma kwa waumini wao.
Baadhi ya viongozi hao akiwamo Padri wa Kanisa la Minara Miwili, Cosmas Shayo, wamesema vitisho hivyo vinatolewa kwa njia ya ujumbe wa karatasi na  simu vikitaka waondoke hapa.
Padri Shayo alikiri kupokea ujumbe wa vitisho. “Ndiyo viongozi wote wakuu wa Kanisa la Minara Miwili tunapokea ujumbe wa vitisho kwa njia ya simu unaotutaka kuondoka na kuacha kuendesha ibada hapa,” alisema jana.
Alisema vitisho hivyo pamoja na matukio ya kuuawa Padri Evaristus Mushi, yamekuwa yakiwaweka katika wakati mgumu wa kuishi kwa hofu na wasiwasi mkubwa, pamoja na kuendesha ibada kwa waumini na wafuasi wa madhehebu ya kikristo.
Alisema hadi sasa hakuna ulinzi wowote katika Kanisa hilo kama ambavyo ilitolewa ahadi na viongozi wakuu likiwamo Jeshi la Polisi . “Mimi hapa sijaona askari yeyote, kuanzia Polisi au askari kanzu waliokuja kulinda na kuweka usalama ... Serikali imeahidi na kutuhakikishia ulinzi lakini sijaona askari,” alilalamika.
Lakini Katibu wa Dayosisi ya Kanisa Anglikana Zanzibar,  Francis Wakati alipozungumza na gazeti hili ofisini kwake Mkunazini, alisema wameanza kupokea ulinzi kutoka  Polisi wanaokuja kwa zamu kuanzia asubuhi, mchana na usiku kulinda kanisani hapo.
Wakati alisema kwa muda mrefu waliandika barua Polisi kuomba ulinzi kutokana na matukio mbalimbali zikiwamo fujo za wafuasi wa kikundi cha Uamsho, lakini wamekuwa wakijibiwa, kwamba hali ni shwari.
“Kuanzia juzi (Jumatatu) baada ya tukio la kuuawa Padri Mushi tumeanza kupokea walinzi kutoka Polisi na nilipowauliza, waliniambia wameambiwa waje kulinda Kanisa...wanafunga banda wakati farasi wameshatoka nje,” alisema Wakati.
Mwandishi wa habari alishuhudia gari la Polisi aina ya Land Rover likiingia katika eneo la Kanisa la Mkunazini na kushusha askari polisi wanne kwa ajili ya lindo la mchana hadi usiku saa nne.
Wakati  alikiri kuwapo vitisho dhidi ya viongozi wa Kanisa hilo vikiwataka kusitisha shughuli za ibada visiwani hapa kwa madai kwamba Zanzibar ni ya Kiislamu.
“Vitisho kwetu sisi ni jambo la kawaida, tumevizoea Wakristo wa Zanzibar...tangu kuibuka kwa vurugu za kidini viongozi wetu wamekuwa wakipokea vitisho kwa njia ya simu na vikaratasi vikitutaka sisi ‘makafiri’ tuondoke,” alisema Wakati.
Alisema ipo dhana kubwa miongoni mwa wananchi wa Zanzibar wakitaka visiwa hivyo vitambuliwe rasmi kuwa ni Dola ya kiislamu, wakati Sultani aliyetawala visiwa hivi ndiye aliyetoa idhini ya kugawa ardhi kwa  Wakristo kwa ajili ya ibada; kujengwa makanisa mawili ya kwanza Mkunazini na Minara Miwili yaliyo eneo la Mji Mkongwe.
Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa, akizungumza kwa simu, alisema hadi sasa hakuna mtu aliyekamatwa kuhusu kuuawa kwa Padri Mushi.
Alipoulizwa kuhusu taarifa za kukamatwa kwa watu Kenya kuhusu mauaji hayo, alisema hana taarifa hizo.
“Mimi sina taarifa za kukamatwa kwa watu waliohusika na mauaji ya Padri Mushi huko Kenya ... mimi eneo langu la kufanya kazi ni Zanzibar ndipo ninapowajibika,” alisema.
Wakati huo huo, Kaimu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Nchini, Naibu Kamishna wa Polisi, Issaya Mngulu, amekanusha kuwapo watu waliokamatwa Kenya isipokuwa alisema watu watano wanashikiliwa kwa mauaji hayo.
"Napenda kukanusha kwamba taarifa hiyo si sahihi...nitoe rai kwa vyombo vya habari kujiepusha na utoaji wa taarifa za uongo zinazoweza kuvuruga uchunguzi wa suala hili," alisema akilenga gazeti moja lililoandika habari hizo.
Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Arusha, Josephat Lebulu ataka Polisi na Idara ya Usalama wa Taifa, kukamata wanaosambaza CD za uchochezi dhidi ya Ukristo na Uislamu sambamba na wanaotuma ujumbe mfupi wa maneno kwa baadhi ya viongozi wa dini.
Katika ibada maalumu ya kumwombea marehemu Padri Mushi iliyofanyika juzi katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Theresia mjini Arusha, Askofu Lebulu alihimiza Watanzania kuwa na moyo wa kusamehe na kuomba Taifa lisiingie kwenye machafuko.
Hata hivyo, alisema pamoja na ujumbe unaotumwa, viongozi wa dini hawatarudi nyuma katika imani na kutoa huduma za kiroho kwa waumini wao. Alitaka mapadri, watawa na watoa huduma wengine wa dini wasife moyo akisisitiza ikitokea mauaji kama yaliyotokea Zanzibar, watakuwa wamekufa kwa ajili ya kumtangaza Kristo.
Pia Polisi kupitia kwa Msemaji wake,  Advera Senso imesisitiza kuendelea na operesheni ya kusaka na kuwachukulia hatua wanaochochea vurugu kwa kutumia CD, ujumbe wa simu na mahubiri.
Katika hatua nyingine Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Norman Sigalla amepiga marufuku mahubiri yanayolenga uchochezi katika nyumba za ibada na kuonya wanasiasa wanaotumia migogoro kupata umaarufu.
Kikao cha Kamati ya Ulinzi na Usalama mkoani humo ndicho kimeazimia hayo. Watu wanaodurufu na kusambaza CD au kutuma ujumbe unaochochea migogoro ya kidini wameanza kukamatwa.
“Kama una CD, DVD au mikanda yenye ujumbe wa kuchochea migogoro, hakikisha unaipeleka hata kwa Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wako. Hatuko tayari kuona mkoa wetu unakumbwa na migogoro ya kidini,” alisema.

No comments: