MAHABUSU WA KIKE ALIA KUKOSA DAWA ZA MTOTO GEREZANI...

Mwanamke anayekabiliwa na shtaka la mauaji ya mtoto wake mlemavu juzi, aliiambia Mahakama kuwa licha ya mtoto wake kuugua na kumpeleka hospitali
ya Magereza, hakupata dawa na kutakiwa kwenda kununua dawa
alizoandikiwa, jambo lililofanya mpaka sasa ashindwe kumpa dawa mtoto huyo.
Mshtakiwa huyo Redience Charles (32), mkazi wa Hombolo Manispaa ya Dodoma alitoa madai hayo mbele ya Hakimu Mkazi Adrian Kilimi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma Mjini, baada ya kupanda kizimbani akiwa na mtoto mdogo mgongoni kusikiliza mwenendo wa kesi yake.
Redience yuko katika gereza la mahabusu la Isanga Manispaa ya Dodoma.
Kauli hiyo aliyotoa ilifuatia swali la Hakimu huyo kumuuliza hali ya mtoto inavyoendelea huko gerezani alipo.
"Mtoto anaumwa, pale gerezani kuna hospitali nikampeleka lakini dawa walizomuandikia pale hakuna nikatakiwa kwenda kununua duka la dawa, sina hela mpaka sasa hajanywa dawa," alisema mama huyo.
Kutokana na kauli hiyo, Hakimu Kilimi alimwelekeza mama huyo kurudi hospitalini hapo ili waone namna ya kumsaidia.
Kesi hiyo ambayo upelelezi wake haujakamilika imepangwa kutajwa tena Februari 18, mwaka huu.
Mwanamke huyo alifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Machi 29, mwaka jana akiwa na mtoto mchanga akikabiliwa na shtaka la mauaji ya mtoto wake mlemavu Karim Salum aliyekuwa na umri wa miaka mitano na kisha kumtumbukiza kwenye choo cha shule.
Mshtakiwa anadaiwa kutenda kosa hilo Machi 7, mwaka jana huko Hombolo Bwawani.
Mtoto aliyeuawa alikuwa ni mlemavu wa viungo na bubu ambapo mwili wake uligundulika kwenye shimo la choo cha Shule ya Msingi Hombolo Bwawani A ukiwa umeharibika vibaya.
Marehemu alikuwa akiishi na mama yake mzazi na baba yake wa kambo Benjamini Chipanha ambapo mshtakiwa huyo amekuwa akieleza kijijini hapo kuwa mtoto wake alikuwa amechukuliwa na wafadhili kwenda kulelewa mkoani Tanga.
Taarifa za awali zilimkariri Diwani wa Hombolo Bwawani, Mussa Kawea zilisema kuwa, mshtakiwa licha ya awali kudai mwanawe amepata mfadhili wa kumlea mkoani Tanga, alijua kuwa mtoto hakuwa kwa mfadhili yeyote.
Kawea alisema Machi 7, mwaka jana walipata taarifa za kupotea kwa mtoto huyo baada ya bibi yake mzaa mama Esther Kuyowona kutoa taarifa ya kutoweka kwa mjukuu wake na kwamba juhudi za kumdodosa mama wa mtoto zilipoonekana kutozaa matunda walitoa taarifa polisi.
Alisema licha ya mama kudai mwanawe yupo Tanga, wananchi walifanya msako na katika pitapita yao walisikia harufu kali katika choo cha shule na hivyo kutoa taarifa tena polisi ambapo baada ya choo kuvunjwa kulikutwa mabaki ya mwili wa mtoto huyo ukiwa umeharibika vibaya na ndipo mshtakiwa huyo alikamatwa na kufikishwa mahakamani kujibu mashtaka yanayomkabili.

No comments: