MWANAFUNZI ABAKWA NA KUNYONGWA HADI KIFO MKOANI MARA...

Kamanda Absalom Mwakyoma.
Watu wawili wamekufa katika matukio mawili tofauti, mkoani Mara, akiwemo mwanafunzi mmoja wa shule ya msingi aliyebakwa na kisha kunyongwa.
Inasadikiwa wauaji wake walimnyonga kwa kutumia gauni alilolivaa na kisha kumtupa.
Hayo yalisemwa na Kamanda wa polisi mkoa wa Mara, Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa polisi, Absalom Mwakyoma, akizungumza na waandishi wa habari mjini Musoma.
Kamanda Mwakyoma alisema mwanafunzi aliyebakwa na kuuawa alikuwa anasoma darasa la sita katika shule ya msingi Makoko, iliyoko katika manispaa ya Musoma na maiti yake ilitupwa eneo la Darajani manispaa ya Musoma.
Alisema kuwa uchunguzi wa awali uliofanywa na polisi na daktari inaonesha kuwa mwanafunzi huyo alibakwa kwanza kisha akanyongwa kwa gauni lake alilokuwa amevaa.
Kwa mujibu wa wazazi wa mwanafunzi huyo, alitoweka nyumbani na siku mbili baadae mwili wake uliokotwa katika nyumba ambayo haitumiki. Kamanda Mwakyoma alisema hakuna watu anayeshikiliwa kuhusiana na tukio hilo.
Kamanda Mwakyoma amewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa jeshi hilo, ili watu waliofanya unyama huo waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.
Katika tukio lingine mtu aliyejulikana kwa jina la  Kizwere Ndege (47), amekufa papo hapo baada ya kugongwa na basi la Kampuni ya Bunda Express lenye namba za usajili T.810 eneo la Iramba, wilayani Butiama.
Kamanda Mwakyoma alisema marehemu aliyekuwa akitembea kwa miguu aligongwa na basi hilo lililokuwa likiendeshwa na Mkazi wa Mwanza Ramadhan Karimu na kwamba chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi.

No comments: