WAFANYABIASHARA WADAIWA KUFICHA PETROLI...

Uhaba wa nishati ya mafuta unaoendelea kuikumba mikoa mbalimbali nchini umedaiwa kusababishwa na wafanyabiashara kuficha nishati hiyo wakisubiri bei mpya itakayotangazwa kesho na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Madini (Ewura).
Akizungumza jana, Mkurugenzi wa Mpango Unaoratibu Uagizaji wa Mafuta (PIC), Michael Mjinja alielezea kushangazwa na kuadimika kwa nishati hiyo na kwamba huenda wafanyabiashara wameficha bidhaa hiyo kusubiri bei mpya.
Kauli hiyo pia imeungwa mkono na mfanyabiashara maarufu nchini, Azim Dewji ambaye alidai kuwa kero ambayo Watanzania wanaendelea kupata, imetokana na  wafanyabiashara wengi kushindwa kuuza bidhaa hiyo kutokana na bei ndogo iliyopo na hivyo kukosa faida.
Wakati mafuta yakiadimika katika vituo vya reja reja, Mjinja aliliambia gazeti hili kuwa kuna mafuta mengi na ya kutosha nchini na akashangaa inakuwaje baadhi ya vituo vya mafuta kukosa nishati hiyo.
Alitoa mfano kuwa kuna meli iliyomaliza kupakua mafuta juzi na kufanya kiasi kilichopo kwenye soko la ndani kuwa ni lita milioni 33 za dizeli na lita milioni 31 za petroli na kwamba kuna meli nyingine ambayo imeanza kupakua mafuta ya ndani jana.
“Takwimu hizi ni kwa mujibu wa kampuni zinazonunua mafuta nje walizotoa jana (juzi)  nashangaa kuelezwa kuwa bado kuna upungufu wa mafuta,” alisema Mjinja na kufafanua kuwa jukumu lao ni kuagiza tu nishati hiyo, ila usambazaji wameachiwa Ewura.
Tatizo hilo limekuwa kubwa mikoani, lakini pia kwa jana katika baadhi ya vituo Dar es Salaam havikuwa na nishati hiyo, jambo ambalo linadaiwa kuwa ni wafanyabiashara kuyaficha kusubiri bei mpya kesho.  
Ewura imeweka utaratibu wa kutangaza bei mpya kila Jumatano  ya mwanzo ya  kila mwezi, hali ambayo inafanya wafanyabiashra walio wengi kuficha bidhaa hiyo kusubiri bei mpya.
Dewji alisema ukosefu wa nishati hiyo kwenye vituo vingi vya mafuta umetokana na wafanyabiashara kuona bei ya sasa haiwalipi na hata wanapotaka kuzungumza na Ewura hawafanikiwi.
“Kero yote hii imetokana na jeuri ya Ewura, hawataki kukutana na wafanyabiashara kuzungumzia suala la bei,” alisema Dewji.
Bei elekezi iliyotolewa na Ewura mwanzoni mwa Oktoba, petroli ilishuka kwa Sh 306 kwa lita na Sh 192 kwa lita moja ya dizeli.
Petroli kwa Dar es Salaam inauzwa Sh 1,994 kwa lita badala ya Sh 2, 300 ya Septemba,  dizeli bei yake ilishuka hadi Sh 1,950 kutoka Sh 2,142. Bei ya mafuta ya taa ilibaki Sh 1,993.
Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa Ewura, Titus Kaguo hakutaka kutoa ufafanuzi wowote juu ya suala hilo la mafuta, kwa maelezo kuwa masuala yote yanazungumzwa na Wizara ya Nishati na Madini.
“Hilo suala liko ngazi ya juu, muulizeni Maswi (Eliakim-Katibu Mkuu wa Wizara) ndiye mwenye uwezo wa kuzungumzia masuala hayo,” alisema Kaguo. Maswi alisema atatoa kauli leo kuhusu suala hilo.
Hata hivyo, baadhi ya watu wanahoji, inakuwaje wafanyabiashara hao wasubiri bei mpya bila kujua kama inashuka au kupanda na kuhisi kuwapo watu ndani ya wizara husika kuvujisha ukokotoaji unaofanyika kabla ya kutangazwa.
Lakini wapo pia wanaosema huenda wafanyabiashara hao wanatumia muda mwingi kufuatilia bei ya soko la dunia na wanapoona mwelekeo ni kupanda bei ndipo nao kidogo kidogo wanaanza kuficha nishati hiyo.

No comments: