KANISA KATOLIKI LAADHIMISHA MIAKA 150 YA IMANI LIKISIFU UVUMILIVU ZANZIBAR...


Kanisa Katoliki la Minara Miwili, Zanzibar ambalo Padri wake alishambuliwa kwa tindikali hivi karibuni.
Kanisa Katoliki leo linaadhimisha miaka 150 ya Imani Endelevu Katoliki Jimbo la Zanzibar huku likisifu uvumilivu wa kiimani uliokuwapo karne kadhaa na kulaani watu wachache wanaotumiwa kuharibu amani visiwani. 

Viongozi wa kanisa hilo wamesema matukio ya mwishoni mwa mwaka juzi na mapema mwaka jana ya baadhi ya viongozi wa Kanisa kuuawa kwa kupigwa risasi, kujeruhiwa na wengine akiwamo Shehe kumwagiwa tindikali, yalikusudiwa kuvuruga udugu uliodumu kwa amani karne na karne. 
Sambamba na maadhimisho hayo, walisifu hatua ya kiongozi wa Kanisa hilo duniani, Papa Francis juzi kuwaondoa madarakani makardinali wanne waliokuwa wasimamizi wa benki ya Vatican kwa tuhuma za kutakatisha fedha, wakielezea kuwa ni moja ya uwajibikaji katika uongozi na kudhihirisha kuwa katika Kanisa hakuna kubebana. 
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na mwandishi kuhusu maadhimisho hayo, maaskofu wa Kanisa Katoliki nchini walisema kwa miaka mingi, wafuasi wa imani kubwa mbili visiwani humo ni Uislamu na Ukristo, kwa miaka yote kabla ya mwaka jana (2013) walikuwa wakiishi kwa udugu na kuvumiliana. 
Askofu wa Jimbo la Zanzibar, Augustino Shao alisema tangu Ukristo uingie Zanzibar katika karne ya 15 kabla ya kurejea tena miaka 150 iliyopita, kumekuwa na uvumilivu wa kiimani lakini Kanisa la kipindi cha sasa limo katika nyakati za kutindikiwa kwa uvumilivu huo. 
“Haikuwa hivi tangu awali, sasa tumekosa uvumilivu wa kuishi pamoja kwa tofauti za imani zetu, kuona wenye imani nyingine walio wachache hawana haki, wachache wanachafua, lazima katika jumuiya ya wengi, wawepo watu wasijali utu, sisi ni Watanzania lazima tuishi pamoja, makabila, dini na rangi zetu ni viunganishi na tunu,” alisema Askofu Shao na kuongeza: 
“Hakuna dini ya Taifa, changamoto tunazoziona miaka hii tunaziweka katika sehemu ya kutojua, kwamba hakutakaa kuwe na dini ya Taifa, kumkubali mwenzako pamoja na tofauti zake za kiimani, kabila na itikadi za kisiasa inapaswa kuwa utajiri na tunu ya pekee kwetu,” alisema. 
Askofu Shao ambaye ni Askofu wa pili Mtanzania visiwani Zanzibar tangu mfumo wa usimamizi wa Jimbo hilo kuwa chini ya Askofu, alisema kitakachofanyika leo ni Ibada ya Misa ya shukrani kwa Mungu kwa tunu ya imani endelevu visiwani humo itakayoshirikisha maaskofu kutoka majimbo yote nchini, mapadri na waumini kwa ujumla. 
Kwa utaratibu wa kawaida wa Kanisa Katoliki, ibada kama hiyo ya Jubilei, hushirikisha maaskofu wote wa majimbo Katoliki 33 Tanzania Bara, makasisi, watawa wa kiume na wa kike, viongozi wa madhehebu mengine na waumini. 
Askofu Shao alisema maandalizi yanafanywa na waumini wenyewe, lakini pamoja na kwamba kila Mkatoliki anaruhusiwa kuhudhuria, wawakilishi wachache kutoka kila jimbo wamechaguliwa kwa uwakilishi katika sherehe hiyo. 
Alisema matukio ya kiimani yatafanyika na kuelezewa historia ya Kanisa Zanzibar, jambo linalotazamiwa kuleta mwamko mpya wa imani kwa waumini na Kanisa. Maaskofu kadhaa walishawasili Zanzibar juzi na jana, akiwamo Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo. 
Alisema walipeleka mwaliko kwa Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein na kueleza kuwa ingawa hawajapata taarifa kama atakuwapo, wanatarajia atafika au kutuma mwakilishi. 
Askofu wa Jimbo Katoliki Bukoba, Method Kilaini alisema wapo watu wachache wanaokubali kutumiwa na watu wa nje ya nchi kuharibu tunu ya udugu na uvumilivu wa kiimani iliyopo nchini hivyo hawapaswi kuendelea kupata nafasi hiyo. 
“Udugu ulikuwa mkubwa Zanzibar lakini msukosuko ukaingia hivi karibuni baada ya watu wachache, wengi wao wakiwa vijana, kurubuniwa kwa fedha kwa kutaka maisha rahisi waliyoyaficha kwa mgongo wa dini na kufanya vitendo vibaya na vya kinyama na hali sasa ni mbaya,” alisema na kuongeza: 
“Waislamu wa Zanzibar ni watu wazuri, ingawa ni wengi kuliko Wakristo… Waarabu waliingia visiwani miaka 800 kabla ya Wamisionari, lakini walionesha kuvumiliana, wapo watu wachache wanafuata mkumbo kutoka nje na si Zanzibar, huu ni wakati kwa Waislamu, Wakristo na Serikali kuwa kitu kimoja kukomesha hali hii”. 
Askofu Shao alisema wana uhakika wa hali nzuri ya usalama kwa kuwa ni ahadi endelevu ya Serikali tangu yalipotokea matukio ya kuhatarisha amani kwao. 
Matukio yaliyolikumba Kanisa ni pamoja na mauaji ya Padri Evarist Mushi, Februari mwaka jana na kujeruhiwa kwa risasi Padri Ambrose Mkenda, Desemba mwaka juzi. 
“Tuna uhakika wa usalama kwa kuwa ni ahadi endelevu ya Serikali, walisema hawataruhusu yatokee yaliyotokea, tunaona amani inarejea na tuna imani na hilo kwa kuwa hata uongozi umepanguliwa Polisi, ni matumaini yetu ulinzi utaimarishwa,” alisema Askofu Shao. 
Kisiwa cha Zanzibar kilikuwa lango la kuenea kwa Ukristo Afrika Mashariki na Kati. Wakristo wa kwanza kufika ni Wamonaki Waagustino kutoka Ureno mwaka 1499. Baadaye walifukuzwa na Waarabu mwaka 1698. Walikuja Wakapuchini mwaka 1857 na wakakaa kipindi kifupi. 
Kanisa maarufu la Minara Miwili, ambalo ndipo jimboni, lilianza kujengwa mwaka 1867 na kukamilika 1897 ikiwa ni miaka 30 ya ujenzi. Lilikuwa chini ya utawala wa kitume kuanzia mwaka 1964 hadi mwaka 1980 walipolifanya kuwa Jimbo. 
Wakati wa usimamizi wa kitume, mapadri waliosimamia na miaka yao kwenye mabano ni  Joseph Spendi (1966-1968), Adrian Mkoba (1968-1973), Bernard Ngaviliau akiwa kasisi alilisimamia mwaka 1973 hadi 1980 alipoteuliwa kuwa Askofu na Zanzibar kuwa Jimbo kamili. 
Ngaviliau aliliongoza hadi mwaka 1996 na Aprili 27,  1997 Shao alisimikwa Askofu wa Zanzibar hadi leo.. 
Akielezea hatua aliyochukua kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis ya kutimua kazi makadinali wanne waliokuwa wasimamizi wa benki ya Vatican, Askofu Shao alisema hatua hiyo ni nzuri, kwa kuwa inaendana na sera zake za uwajibikaji na wao wameipokea. 
“Sera alizoingia nazo kuongoza Kanisa zinahitaji kuwa na watu watakaomwezesha kufikia pale anapotamani, Kanisa Katoliki lina utaratibu wake katika masuala ya utendani na kwa sera zake sisi tunaona ni sawa ila kuna mambo ambayo hayawezi kubadilishwa kabisa; tunu ya imani na mafundisho ya imani,” alisema Askofu Shao. 
Hata hivyo, alisema makadinali hao si kwamba waliiba ama kuhusika na matukio ya moja kwa moja, lakini kwa kuwa ni viongozi wa ngazi za juu kiutendaji, suala la uwajibikaji ni muhimu. 
Alitolea mfano mawaziri wanne waliojiuzulu nchini si kwamba waliingia porini na kuhusika kubaka wanawake bali waliwajibika kwa kuwa ni watendaji wa ngazi ya juu. 
Mawaziri waliojiuzulu ni pamoja na Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel Nchimbi, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha, Waziri wa Maendeleo ya Mifugo, Dk David Mathayo David na Waziri wa Maliasili na Utalii, Khamis Kagasheki. Rais Jakaya Kikwete anasubiriwa kutangaza Baraza jipya la mawaziri karibuni. 
Askofu Shao alisema katika uongozi wowote, uwe wa kiroho ama kijamii, suala la kuwajibika na mabadiliko ni muhimu yakawepo na kuongeza kuwa nchini Kanisa likiona kuna hali ya kutowajibika, japo huwa inafanyika, si vibaya kuchukua uamuzi kama alivyofanya Papa Francis. 
Katika hilo, Askofu Kilaini alisema ni mfano wa uwajibikaji na katika Kanisa hakuna sera ya kubebana, ingawa wakati kashfa ikitendeka inawezekana hata makadinali hao, baadhi yao hawakuwapo. 
“Inawezekana wakati ule mbaya wa kashfa hii hawakuwapo lakini ndio uwajibikaji wenyewe huo, ni kama mawaziri wanne nchini waliojiuzulu, hawakuhusika moja kwa moja na ubakaji wa wanawake lakini wamewajibika kama viongozi, kikosi cha makadinali wa kumshauri Papa alichokiunda, kina watu wakali sana,” alisema Askofu Kilaini. 
Alisema makadinali hao, akiwamo wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Kadinali Laurent Monsengwo Pasinya, ni viongozi walio tayari kusafisha chochote kisichokuwa sawa ndani ya Kanisa, hivyo hatua hiyo haimaanishi wahusika ni wezi bali uwajibikaji. 
Mwandishi aliandika juzi hatua ya Papa Francis kuwaondoa madarakani makadinali wanne, akiwamo Waziri wa Mambo ya Nje, Kadinali Tarcisio Bertone, Odilo Scherer wa Brazil, Telesphore Toppo wa India na Domenico Calcagno wa Vatican, wote waliteuliwa na Papa Benedict XVI muda mfupi kabla ya kujiuzulu wakiwa na miezi 11 ya uteuzi katika kipindi cha miaka mitano. 
Aliyenusurika katika hatua hiyo ni Kadinali Jean-Louis Tauran, Mkuu wa Baraza la Upapa linalohusika na mijadala ya kidini. 
Benki ya Vatican, nchi ndogo kuliko zote duniani, ilikumbwa na kashfa ya kutakatisha fedha mwaka 2010 baada ya waendesha mashitaka wa Italia kugundua shughuli zenye utata zihusuzo fedha chafu ndani ya benki. Tayari watu wa kushika nafasi zao walishateuliwa. 
Hayo ni mabadiliko makubwa kufanywa na Papa Francis, Mwargentina na Papa wa kwanza kutoka nje ya Ulaya kwa zaidi ya miaka 1,000 tangu alipochaguliwa Machi 13 mwaka jana. 
Aidha, mabadiliko makubwa pia yanatarajiwa kufanyika kuhusu kashfa ya udhalilishaji wa kijinsia dhidi ya watoto yaliyofanywa na baadhi ya makasisi wa Kanisa hilo na hatua tayari zinaanza kuonekana katika usimamizi wa sheria za Kanisa.

No comments: