Jaji Joseph Warioba. |
Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba ameonya vyama vya siasa kwa kushinikiza maslahi yao kwenye mchakato wa uundwaji wa Katiba mpya.
Amesema hatua hiyo itasababisha kupatikana kwa Katiba ya Mapambano itakayohatarisha amani, utulivu na mshikamano wa nchi.
Katika hatua nyingine, Mwenyekiti huyo amesema ni matarajio kwamba wadau watashirikiana na Tume kuhakikisha Katiba itakayoundwa inaheshimiwa na wananchi wote ili kujenga umoja wa kitaifa na si kugawa Watanzania.
Alisema hayo Dar es Salaam jana alipokutana na waandishi wa habari ili kutoa taarifa ya uendeshaji wa mabaraza ya Katiba, ambayo yalijadili na kutolea maoni Rasimu ya Katiba na kuwasilisha kwa Tume hiyo Agosti 31.
Akizungumzia hali ilivyo sasa katika mchakato, Jaji Warioba alisema wakati Tume ilitarajia vyama vya siasa kutumia nafasi ya kabla ya Bunge la Katiba katika kuunganisha wananchi, hali imekuwa tofauti, kwani sasa vyama hivyo vinaendesha siasa majukwaani kwa nia ya kuwagawa.
Alisema kama vyama hivyo vitaendelea kama sasa, kuna uwezekano maoni ya wananchi yaliyo katika sura ya kwanza hadi ya tano ya Rasimu hiyo yakapuuzwa na kuibuliwa kwa matakwa ya vyama vya siasa, jambo litakalohatarisha amani ya nchi.
"Sura ya kwanza hadi ya tano inaeleza nini wananchi wanahitaji kwa Katiba yao. Ukisoma katika maeneo haya utakuta masuala yote kuhusu tunu za nchi, amani, mshikamano, uzalendo na rasilimali.
"Katika maeneo hayo utaona pia maoni ya wananchi kuhusu wabunge kutokuwa mawaziri, wabunge kuwa na kikomo na hata namna wabunge wasiowajibika wanavyoweza kuondolewa na wananchi. Tume ilitarajia vyama kuboresha hayo yaliyosemwa na wananchi na si kutafuta ya kwao."
Mwenyekiti huyo alisema wakati Tume ilipita nchi nzima kukusanya maoni ya wananchi na kuruhusu hata vikundi kutoa maoni kupitia mabaraza ya Katiba kwa kuamini kuwa yatahusu wananchi, lakini kwa bahati mbaya vyama vya siasa vilitumia nafasi hiyo kuingiza matakwa yao kwa maslahi yao, jambo alilosema litasababisha kupatikana Katiba ya Mapambano.
"Hakuna sababu ya kuoneshana mabavu na kuonesha nani ni mshindi kwani inayoundwa ni Katiba ya wananchi na si ya vyama. Ushauri wa Tume ni kwa wanaogawa wananchi wakae meza moja kuangalia namna ya kuboresha kilichopendekezwa na wananchi na si kuendelea kuwagawa," alisisitiza Jaji Warioba.
Akizungumzia ubishani uliotokea bungeni hivi karibuni, pamoja na kusita kuzungumzia akihofia kuingilia shughuli za chombo hicho, aliitaka Serikali kutafakari kwa kina juu ya baadhi ya mambo yaliyoingizwa kwenye Rasimu hiyo, akisema yakitekelezwa yatakinzana na sheria mama.
Alitoa mfano, kwamba wakati sheria mama inaeleza kuwa uhai wa Tume hiyo ni hadi wakati wa kura ya maoni, Bunge liliazimia uhai wa Tume kumalizika pale Rasimu itakapokabidhiwa kwenye Bunge la Katiba, jambo alilosema linakiuka sheria.
"Ukisoma kifungu cha 18 cha sheria, kinasema Tume ya Mabadiliko ya Katiba itatoa elimu kwa wananchi kabla ya kura ya maoni sasa hapa tunajiuliza, itakuwaje elimu itolewe na chombo ambacho tayari kitakuwa kimevunjwa? Hii inaleta mkanganyiko wa kisheria".
Alisema kwa kawaida, Muswada unapowasilishwa bungeni, Waziri husika ndiye huutetea na kuusimamia hadi unapopitishwa na ndiyo maana sheria mama iliangalia hilo kwa kuzingatia kwamba kwa vile Tume ndiyo ilihusika na mchakato huo inatakiwa kusimamia hatua zote hadi wakati wa kura ya maoni, jambo ambalo alisema sasa limepindishwa.
Kuhusu madai kwamba baadhi ya wajumbe wa Tume hiyo wametishia kujiuzulu, Jaji Warioba alikanusha madai hayo, akisema kilichotokea ni wajumbe kusikitishwa na mambo yanavyoendelea na kuhoji umuhimu wa wao na Tume kuendelea kuwapo.
"Kilichotokea ni kwamba wakati wa mijadala yetu ya kawaida, baadhi ya wajumbe walisema sasa kama mambo yanakwenda namna hii, kuna umuhimu gani wa sisi Tume kuwepo?
"Lakini hakuna aliyejiuzulu wote wanaendelea na kazi ipasavyo, hadi pale watakapomaliza majukumu tuliyokabidhiwa," alisema Jaji Warioba.
Kuhusu uendeshaji wa mabaraza ya Katiba, Mwenyekiti huyo alisema Tume ilijigawa katika makundi 14, kila moja likiwa na wajumbe kati ya wawili na watatu na kuzunguka nchi nzima kufanya jumla ya mikutano 179 iliyohudhuriwa na wajumbe 19,337.
"Mikutano hii ilifanyika katika kila halmashauri ya wilaya, ya manispaa na jiji na mkutano mmoja ulichukua wastani wa siku tatu. Kati ya mikutano hii, jumla ya mikutano 166 ilifanyika Bara na 13 Zanzibar."
Alizitaja changamoto zilizojitokeza kuwa ni baadhi ya vyama vya siasa kuingilia uhuru wa wajumbe katika kutoa maoni kuhusu Rasimu ya Katiba kwa baadhi ya maeneo wajumbe kufundishwa cha kusema.
Alisema Tume kwa kushirikiana na Shirikisho la Vyama vya Watu wenye Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA) kwa upande wa Bara na Umoja wa Watu Wenye Ulemavu Zanzibar (UWZ) iliandaa na kuendesha mikutano miwili ya mabaraza Zanzibar Agosti 5 na Dodoma Agosti 15.
Kuhusu Tume inachofanya sasa, Jaji Warioba alisema ni uchambuzi wa maoni ya Mabaraza ya Katiba na kwa kufuata mwongozo iliojiwekea, uchambuzi huo unafanywa kwa kuzingatia uzito wa hoja za wananchi katika maeneo tofauti ya Rasimu.
"Baada ya uchambuzi huu kukamilika, Tume itaandaa ripoti ambayo itajumuisha Rasimu ya Katiba iliyoboreshwa kutokana na maoni ya mabaraza. Ripoti hiyo itawasilishwa kwa Rais wa Tanzania na wa Zanzibar kama Sheria ya Mabadiliko ya Katiba inavyoelekeza.
"Mipango ya Tume ni kukamilisha kazi hii ndani ya muda uliowekwa na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, sura ya 83 kwamba Katiba mpya iwe tayari Aprili mwakani," alisema Jaji Warioba.
No comments:
Post a Comment