MATOKEO MTIHANI WA DARASA LA SABA SASA YAIVA...

Dk. Shukuru Kawambwa.
Matokeo ya Mtihani wa Kumaliza Elimu ya Msingi Tanzania Bara mwaka huu yamekamilika na yanatarajiwa kutangazwa wakati wowote kuanzia leo.
Matokeo hayo yatakayotangazwa na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa yatakuwa yamewahi kutangazwa kutokana kwa mara ya kwanza kutumia teknolojia mpya ya ‘Optical Mark Reader’ (OMR).
Hayo yalisemwa na Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo alipozungumzia malalamiko kuwa waliahidi kuwa teknolojia hiyo itasaidia kuwahisha matokeo ya mwaka huu.
Pia baadhi ya wazazi walilalamikia kupoteza ada kwa kuwatafutia shule watoto wao ikiwa ni pamoja na  kuchelewa kutafuta shule za watoto kutokana na kutojua kama wamefaulu au hawajafaulu.
“Kuhusu matokeo waambie wazazi wasiwe  na wasiwasi kwani  yatatangazwa siku chache zijazo yaani siku yoyote wiki ijayo na Waziri wa Elimu Shukuru Kawambwa,“ alisema Mulugo.
Alibainisha kuwa matokeo hayo yatakuwa yametangazwa mapema kuliko miaka mingine kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo mitihani hiyo kusahihishwa kwa kompyuta.
Jumla ya wanafunzi 894,881 walisajiliwa  kufanya mtihani huo, wavulana wakiwa   426,285 sawa na asilimia 47.64  na wasichana ni 468,596  sawa na asilimia 52.36.
Aidha, kati ya  wanafunzi hao, wapo wanafunzi 874,379  waliofanya mtihani huo kwa lugha ya Kiswahili na wanafunzi 20,502 watafanya kwa lugha ya Kiingereza ambayo ndiyo waliyoitumia kujifunzia.
Wanafunzi wasioona waliosajiliwa kufanya mtihani ni 92 wakiwemo wavulana 53 na wasichana 39.  Watahiniwa wenye uono hafifu ambao huhitaji maandishi makubwa ni 495, kati yao wavulana ni 238 na wasichana ni 257.
Mtihani huo ulifanyika kwa mara ya kwanza kwa kutumia teknolojia mpya ya ‘OMR’, kwa watahiniwa kutumia fomu maalumu kujibia mtihani na majibu yao yatasahihishwa kwa kutumia kompyuta. Masomo yaliyotahiniwa katika mtihani huo ni Kiswahili,  Kiingereza, Sayansi, Hisabati na Maarifa ya Jamii.

No comments: