YANGA YAWATOA KAMASI AL-AHLY KWAO, YAJIANDAA KUIVAA ESPERANCE...

Wawakilishi wa Tanzania katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika, Yanga SC imedhihirisha kwamba ni Bingwa wa Tanzania baada ya kukataa unyonge wa miaka mingi na kuibana vilivyo Al-Ahly ya Misri katika mechi ya marudiano hatua ya 16 Bora.

Hata hivyo, Yanga imetolewa katika Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kufungwa kwa taabu mabao 2-1 usiku huu katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Borg El Arab mjini Alexandria. Al Ahly inasonga mbele kwa ushindi wa jumla wa 3-2 baada ya awali kulazimisha sare ya 1-1 Uwanja wa Dar es Salaam wiki mbili zilizopita. Aliyewafungisha virago Yanga leo alikuwa ni Abdallah Said aliyefunga bao la pili dakika ya sita ya muda wa nyongeza baada ya kukamilika kwa dakika 90 za kawaida za mchezo akimalizia krosi ya  Walid Soliman kutoka upande wa kushoto.
Al Ahly walitangulia kupata bao katika mchezo wa leo kupitia kwa kiungo Hossam Ghaly aliyeunganisha kwa kichwa kona ya Ahmed Fathi dakika ya 52.
Mshambuliaji wa kimataifa wa Zimbabwe, Donald Dombo Ngoma akaisawazishia Yanga dakika ya 57 kwa kichwa akimalizia krosi nzuri ya beki wa kulia Juma Abdul.
Kwa matokeo hayo, Yanga itamenyana na moja ya timu zilizofuzu Kombe la Shirikisho kuwania nafasi ya kupangwa kwenye makundi.
Kwa Yanga, hii ni mara ya pili kufikia hatua hiyo baada ya mwaka 2007. Mwaka huo Yanga ilifungwa 3-0 na Esperance ya Tunisia katika hatua ya 16 Bora Ligi ya Mabingwa Afrika kabla ya kutoa sare 0-0 Mwanza.
Katika kuwania kucheza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho na ilitolewa na El Merreikh ya Sudan, ikitoa sare ya 0-0 Mwanza na kufungwa 2-0 Khartoum.
Yanga inaweza kukutana tena na Esperance ambayo imeitoa Azam FC ya Tanzania jana kwa jumla ya mabao 4-2, ikishinda 3-0 jana Tunis baada ya kufungwa 2-1 Dar es Salaam katika mchezo wa kwanza.
Kikosi cha Yanga kilikuwa; Deo Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Oscar Joshua, Vincent Bossou, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Thabani Kamusoko, Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Amissi Tambwe/Malimi Busungu dk68, Donald Ngoma na Deus Kaseke/Kevin Yondan dk86.
Al Ahly; Sherif Ekramy; Ahmed Fathi, Rami Rabia, Ahmed Hegazy, Sabri Rahil; Hossan Ashour, Hossam Ghaly, Hussein El Sayed, Moaem Zakaria/Walid Soliman dk64, Ramadan Sobhy na Amr Gamal/ Malick Evouna dk71.

No comments: