BURIANI AZAM FC, YATANDIKWA MABAO 3-0 NA ESPERANCE...

Wawakilishi wa Tanzania Bara kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, Azam FC usiku wa kuamkia leo wameyaaga mashindano hayo baada ya kukubali kipigo cha mabao 3-0 kutoka kwa timu ya Esperance ya Tunisia.

Kwa matokeo hayo, Azam wametolewa kwa jumla ya mabao 4-2 kufuatia ushindi wa mabao 2-1 walioupata kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Azam Complex ulioko Chamazi siku kadhaa zilizopita.
Ikicheza bila nyota wake kadhaa wakiwamo Paschal Serge Wawa, Shomari Kapombe, Jean Baptiste Mugiraneza, Kipre Tchetche na Salum Abubakar, Azam ilishindwa kabisa kufurukuta mbele ya miamba hao wa soka kutoka Tunisia.
Esperance walipata bao lao la kwanza kwa njia mpira wa faulo uliopigwa nje kidogo ya eneo la hatari la Azam na kwenda moja kwa moja huku kipa Aishi Manula akichupa bila mafanikio.
Bao la pili lilifungwa dakika ya 73 kutokana na makosa ya kipa Manula kushindwa kudaka mpira wa krosi na mpira kumfikia mfungaji aliyeudokoa kwa kichwa na kwenda kimiani.
Huku wachezaji wa Azam wakiongozwa na nahodha wao, John Bocco wakihaha kusaka bao la ugenini, wakajikuta wakipachikwa bao la tatu katika dakika ya 81.
Bao hilo lilionekana kuwachanganya zaidi Azam na kujikuta wakiwaachia wapinzani wao kutawala mchezo huo na kufanya watakacho uwanjani.
Kwa ujumla mwamuzi alilimudu vilivyo pambano hilo, huku makosa aliyoyafanya mwamuzi huyo wakati fulani yakiisaidia Azam kupata madhara zaidi.
Beki wa Azam, David Mwantika aliunawa mpira kwenye eneo la hatari akiwa katika harakati ya kuzuia shuti la mshambuliaji wa Esperance.
Leo, wawakilishi wengine wa Tanzania Bara kwenye michuano ya Klabu Bingwa Afrika, Yanga watapeperusha bendera ya nchi kwa kupambana na miamba mingine ya Afrika timu ya Al-Ahly katika mchezo utakaopigwa mjini Alexandria majira ya saa 1 usiku kwa saa za Afrika Mashariki.
Katika mechi ya kwanza iliyopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wiki mbili zilizopita, timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1.
Yanga itahitaji ushindi wowote ama sare yoyote kuanzia mabao 2-2.
Kila la kheri Yanga.

No comments: