SERIKALI YAITOLEA NJE UDA NAULI MPYA MABASI YAENDAYO HARAKA

Serikali imekataa viwango vya nauli mpya vilivyopendekezwa na Kampuni ya Uda Rapid Transit (UDA-RT), itakayotoa huduma ya usafiri wa mabasi yaendayo haraka Dar es Salaam.

Pamoja na kukataa imeweka bayana kuwa viwango hivyo viko juu ambavyo wananchi wengi watashindwa kuvimudu.
Kauli hiyo ya serikali imetolewa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ambaye pia ameagiza wizara zote zinazohusika kukutana haraka iwezekanavyo na kujadili viwango vipya vya nauli vinavyoendana na hali halisi ya maisha ya wananchi.
“… sasa nataka mamlaka zote zilizohusika wakutane na kuja na viwango vipya vya nauli kama huyu mwekezaji ameshindwa aseme, Serikali inaweza kuendesha mradi yenyewe,” alisisitiza Majaliwa.
Wizara na taasisi zilizoagizwa kukutana ni Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi); Wizara ya Ujenzi na ya Uchukuzi;  Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) pamoja na kampuni ya UDA-RT.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam muda mfupi baada ya kurejea akitokea Ruvuma, alikokamilisha ziara yake ya kikazi jana, alisema  viwango hivyo vilivyopendekezwa na vinavyotarajiwa kujadiliwa na Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) havifai na havikubaliki.
Alisema Novemba 25, mwaka jana alitembelea mradi huo wa DART na kumuagiza Katibu Mkuu wa Tamisemi, Mtendaji Mkuu wa DART pamoja na Wakala wa Barabara (Tanroads) kupitia  mfumo mzima wa uendeshaji wa mradi huo, lakini hadi leo hakuna mpango wowote wa biashara uliowasilishwa serikalini na UDA-RT.
Alisema pamoja na hayo, pia kampuni hiyo imeshindwa kuweka bayana gharama za uendeshaji wa mradi huo, uliotakiwa kuanza rasmi Januari 10, mwaka huu.
Majaliwa alisema wakati kampuni hiyo ikishindwa kuweka wazi mpango wake wa kibiashara, alishangaa juzi kusikia imewasilisha viwango vya nauli vilivyopendekeza ambavyo vilikuwa vya gharama ya juu.
“Kwa kukosekana tu gharama halisi za uendeshaji mradi, ni dhahiri kuwa nauli zilizopendekezwa hazina uhalisia,” alisema.
Kampuni hiyo ilipendekeza safari kwenye njia kuu kuwa Sh 1,200 na safari katika njia kuu na pembeni kuwa Sh 1,400 na wanafunzi nusu ya nauli hizo.
“Gharama hizi ni kubwa mno. Mradi huu unalenga kumlinda na kumsaidia mwananchi wa kawaida, wakiwemo watumishi wa umma ambao wengi wao wamejenga pembezoni mwa mji kuweza kusafiri kutoka maeneo ya pembeni hadi katikati ya jiji kwa gharama nafuu na kwa urahisi na si kumkandamiza,” alisema Majaliwa.
 Alisema kipato cha wananchi kwa ujumla wakiwemo watumishi wa umma, bado si kikubwa. Alitoa mfano kwamba, mtumishi anayelipwa mshahara wa  Sh 250,000 kwa mwezi, kwa nauli iliyopendekezwa pamoja na watoto wake, fedha yote inaishia kwenye nauli.
Alisema kwa hali ilivyo, Serikali haiwezi kuridhia viwango hivyo ambavyo ni wazi vitamkandamiza mwananchi badala ya kumsaidia.
“Bado tunayo nafasi ya kuendesha mradi huu, si lazima tuanze Januari 10 kama ilivyopangwa, ni bora tuchelewe na kuanza tukiwa na viwango vya nauli vinavyoridhisha badala ya kuanza na nauli hizi ambazo ni gharama kubwa mno.”
Juzi Sumatra ilikutana na wadau kwa ajili ya kujadili mapendekezo hayo ya nauli, ambayo hata hivyo yalipingwa na wadau wengi wa sekta ya usafiri. Walishauri nauli iwe kati ya Sh 400 na Sh 500 kutimiza malengo ya kusaidia wananchi wa kipato cha kawaida.
Pamoja na hayo wadau hao wakiwemo wananchi na Baraza la Walaji la Sumatra (Sumatra CCC), walihoji sababu za mabasi hayo yanayobeba watu wengi kwa safari moja na yanayotumia barabara zisizo na foleni, yatoze nauli kubwa wakati daladala zinazochukua abiria wachache na kukabiliwa na msongamano mkubwa katika barabara za kawaida, wanatoza nauli za chini.

No comments: