MALI ZA HOSPITALI YA AMI ZAKAMATWA KUFIDIA KODI YA PANGO BILIONI 3


Madalali wa Mahakama Kuu jana waliondoa na kukamata mali za Hospitali ya African Medical Investment Ltd (AMI) maarufu kama Trauma Center ya Msasani Jijini Dar es Salaam, baada ya kushindwa kulipa kodi ya pango kwa zaidi ya miezi 26, inayofikia zaidi ya dola za kimarekani milioni 1.6.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mwakilishi wa kampuli ya MEM Auctioneers and General Brokers Limited iliyopewa kazi ya kukamata mali hizo, Elieza Mbwambwa alisema walikuwa wanatekeleza amri ya Mahakama Kuu, Kitengo cha Biashara kilichoamuru mali hizo zikamatwe ili kupigwa mnada kwa ajili ya kulipa deni lao la pango na kisha kuondolewa kwenye jengo na kumkabidhi mmiliki ambaye ni Navtej Singh Bains.
Alitaja mali zilizokamatwa kuwa ni pamoja na magari matatu ya kubebea wagonjwa, vitanda maalum vya kulaza na kuwahudumia wagonjwa, gari ndogo aina ya Mark II, mashine mbalimbali kama kompyuta, printa, microwave, viti, meza, makochi na hata vitambaa na mashuka ya hospitali.
“Japokuwa mahakama ilitoa amri ya kukamatwa mali zote baada ya kikomo cha notisi ya siku 14, ambayo imeisha jana, mdai amefanya ubinadamu wa kutuomba kama madalali wa mahakama, kuondoa na kukamata vitu ambavyo havitumiki na wagonjwa waliolazwa.
“Tumewapa hospitali ya AMI notisi nyingine ya kuwahamisha wagonjwa kabla ya Mei 22 mwaka huu, kisha tutaondoa kila kitu chao na kumkabidhi mwenye jengo, jengo lake. Tulichofanya ni kuorodhesha mali zote ambazo bado zinatumika na wagonjwa hawa. Wagonjwa wapya hawataruhusiwa kupokelewa tena.
“Endapo hawa waliolazwa hawatahamishwa na hospitali, sisi tutafanya utaratibu wa kuwahamishia katika hospitali zingine,” alisema Mbwambwa.   
Alitaja mashine ambazo zimeachwa kwa ajili ya kuwapa huduma wagonjwa kuwa ni City-Scan, X-ray na mashine nyingine ambayo ni muhimu katika kuchunguza maendeleo ya afya ya mgonjwa.
Akizungumza kwa niaba ya uongozi wa hospitali hiyo, Lawrence Ochola alisema bado madaktari wanaendelea kuwahudumia wagonjwa waliolazwa na kwamba hawezi akasema zaidi ya hayo.
Hatua hii ya kufukuzwa kwenye jengo imefikiwa baada ya mabishano ya muda mrefu ya kisheria baina ya AMI na mfanyabiashara ambaye pia ni mmiliki wa jengo hilo, Navtej Singh Bains.
Taarifa zaidi inasema kwamba akaunti za Benki za Hospitali hiyo ya AMI katika Benki ya EXIM zilizoambatanishwa na Mahakama zilikutwa zikiwa zimefungwa na fedha zote zikiwa zimetolewa.
Amri ya kufurushwa kwa AMI ilitolewa wiki Mei 7 mwaka huu na kusainiwa na Makamu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
Hatua hii sasa inafanya kufungwa kwa Hospitali ya AMI, licha ya rufaa zake za kujaribu kuzuia kufukuzwa, huku ikiwaacha wateja wake katika hali ya sintofahamu.
Baadhi ya ndugu na jamaa wa wagonjwa waliolazwa hospitalini hapo walionekana wakifanya taratibu za kuanza kuwahamisha wagonjwa wao, huku uongozi wa hospitali ikionekana kukaa kimya.
Hatua hii ya kufukuzwa kutoka kwenye jengo inatokana na hospitali hiyo kushindwa kutimiza amri ya Mahakama ya Rufaa ya Tanzania iliyoamuru kulipwa kwa dola za kimarekani milioni 1.6 mahakamani pamoja na kodi ya kila mwezi ya kiasi cha dola za kimarekani 64,000 kila kufuatia mgogoro wa kodi ya jengo.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa AMI Plc, Theunis Botha, ambaye pia ni Mkurugenzi na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Hospitali ya AMI Tanzania, aliwasilisha ombi katika Mahakama Kuu ya Tanzania kuwa imefilisika.
Katika shauri hilo la ufilisi lililofunguliwa wiki iliyopita kwa Msajili wa Mahakama Kuu, kampuni hiyo inadai kuwa imekuwa ikikumbana na hasara za mabilioni ya shilingi jambo lililofanya kuwepo kwa madeni yaliyokithiri ambayo kwa sasa yako nje ya uwezo wa kampuni kulipa.
“Mlalamikaji (AMI) anadai alipata hasara halisi ya Dola za kimarekani 1.146 katika mwaka uliomalizika Februari 28, 2013, huku kwa mwaka uliomalizika Februari 28, 2014, mlalamikaji alipata hasara ya Dola za Kimarekani 775,000,” inasomeka sehemu ya hati ya malalamiko.
AMI Tanzania inamilikiwa na Kampuni mama ya AMI Plc ya London ambayo iliondolewa kwenye Soko la Hisa la London Februari 2014 baada ya jaribio la kuuza mali zake zilizopo Maputo, Msumbiji bila kibali kutoka kwa wanahisa.
Inaelezwa kuwa kampuni hiyo ilitakiwa pia kufanya malipo kwa taasisi mbalimbali, zikiwemo Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na watu na kampuni binafsi.
Kwa mujibu wa shauri hilo, ukichukulia thamani ya mali za kampuni na kiasi cha fedha zinazodaiwa na wadai, kulikuwa hakuna njia ya kuweza kupata fedha za kutosha kuwalipa sambamba na kutekeleza majukumu yake.
Pia kuna kumbukumbu zinazoonesha kuwa Lancet Laboratory (T) Ltd iliwasilisha ombi la dharura dhidi ya kufungiwa kwa Hospitali ya AMI ikiwa inaidai hospitali hiyo zaidi ya Sh milioni 150.
Taarifa za ndani zinaeleza kuwa wadai mbalimbali wako njia panda kutokana na deni kubwa la Dola za Kimarekani milioni nne wanaloidai hospitali hiyo. Wadai wakubwa ni pamoja na mmiliki wa jengo Bains, madaktari, wafanyakazi, TRA, wasambazaji wa dawa na wasambazaji wengine.

No comments: