Majaliwa ya kesi inayomkabili Katibu wa
Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Nchini ,
Shehe Ponda Issa Ponda, ambayo ipo
kwenye hatua ya utetezi itapatikana miezi mitatu ijayo.
Hiyo inatokana na hakimu anayesikiliza kesi
hiyo Hakimu Mwandamizi wa Mahakama hiyo,
Mary Moyo kuanza rasmi likizo ya uzazi
ya miezi mitatu na hivyo Hakimu Mfawidhi wa wilaya ya Morogoro Maua Hamduni
kuiahirisha hadi Aprili 16, mwaka huu
ambapo itatajwa tena mahakamani hapo.
Mtuhumiwa
alifikishwa mahakamani hapo pasipo mawakili wake wa utetezi , ambapo kwa
jana upande wa mashtaka uliongozwa na Wakili wa Serikali, Sunday Hyera.
Kabla ya kuanza kutoa maelezo ya kuahirishwa
kwa kesi, Hakimu huyo alimuuliza Shehe Ponda juu ya kutoonekana kwa
mawakili wake mahakamani hapo na endapo
anazo taarifa zao , naye alijibu
kuwa hakuwa na taarifa zao.
Kesi hiyo kwa sasa ipo katika hatua ya upande wa mashtaka kujibu hoja
zilizotolewa na upande wa utetezi baada ya kufungwa kwa ushahidi ambazo zilidai
kuwa Shehe Ponda hakuwa na kesi ya kujibu.
Kutokana na hatua ilipofikiwa , Hakimu huyo,
alisema pamoja na Hakimu Moyo anayeisikiliza kesi hiyo tangu
mwanzo kuwa katika mapumziko ya likizo ya uzazi ya miezi mitatu, kisheria haiwezekani shauri hilo ikabadilishiwa hakimu
mwingine bali itaendelezwa naye baada ya kumaliza likizo ya uzazi.
Kwa mujibu wa Hakimu huyo, kwa hivi sasa kesi
ya Shehe Ponda itaendelea kutajwa mahakamani hapo hadi hakimu wake atakapoanza
kazi baada ya kumaliza likizo hiyo .
Kufuatia maamuzi ya hakimu huyo, Shehe Ponda
alinyosha kidole mbele ya hakimu huyo na kupewa nafasi ya kuzungumza ambapo
alimwambia hakimu kuwa kwa vile kesi yake itakuwa ikitajwa pekee, anaomba siku
ya kufikishwa mahakamani abakie magereza ili kuondoa usumbufu.
Shehe Ponda alidai kuwa, ingekuwa ni jambo
nzuri siku ya kutajwa kwa kesi yake iitwe fomu yake na kugongwa muhuri wa Mahakama
, wakati akiwa gerezani .
Hata hivyo hakimu huyo alimjibu Shehe Ponda
kuwa, kisheria njia hiyo hairuhusiwi , kwani kinachozingatiwa ni kwa mtuhumiwa
kufikishwa mahakamani na hakimu kumwona kwa macho yake na kuiahirisha kwa
msingi huo na si vinginevyo.
Hakimu huyo alimuuliza Sheikh Ponda kuwa yenye
haoni kuwa ni fursa kuja uraiani kuonana
na kusalimiana na ndugu zake na kujibiwa na Sheikh Ponda kuwa, yeye
amezoea kukaa gerezani hivyo haoni sababu hizo.
Tofauti na siku nyingine inaposikilizwa kesi
hiyo ambapo wafuasi wake hufurika nje ya uzio wa mahakama hiyo , jana,
walijitokeza wachache hawakuzidi watu 10
ambao hawakuweza kufanya jambo
lolote la kusoma Quraan na kufanya
maombi .
Shekhe Ponda alifunguliwa kesi namba 128/2013
katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa wa Morogoro akikabiliwa na mashtaka matatu
ambayo aliyatenda Augosti 10, mwaka 2013 katika eneo la Kiwanja cha Ndege
Manispaa ya Morogoro na alifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Agosti
19 mwaka 2013.
No comments:
Post a Comment