ASKOFU GWAJIMA APANDISHWA KIZIMBANI KISUTU


Hatimaye Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima (45), amepanda katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, akikabiliwa na mashitaka mawili, ikiwemo la kutumia lugha ya matusi dhidi ya Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam la Kanisa Katoliki, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo.

Mbali na Gwajima, washitakiwa wengine ni Askofu msaidizi wa Kanisa hilo, Yekonia Behagaze (39), Geofrey Mzava (31) ambaye hakuwepo mahakamani hapo na George Milulu (43) mkazi wa Kimara Baruti.
Kesi hiyo ambayo ilianza kutajwa saa 9:30 alasiri hadi saa 11 jioni, ilisikilizwa mbele ya Hakimu Wilfred Dyansobera, ambapo mawakili wa Serikali; Wakili Mwandamizi Joseph Maugo, akisaidiwa na Shadrack Kimaro na Tumaini Kweka,   walisoma mashitaka dhidi ya washitakiwa.
Katika mashitaka ya kwanza yanayomkabili Gwajima, Wakili  Kweka alidai kuwa katika siku isiyofahamika kati ya Machi 16 na 25 mwaka huu, maeneo ya Tanganyika Packers, kiongozi huyo alitumia lugha ya matusi dhidi ya Kardinali Pengo, akieleza kuwa ni mtoto, hana akili katika namna ambayo angeweza kusababisha uvunjifu wa amani.
Mshitakiwa alikana shitaka hilo ambapo suala la dhamana kwa mshitakiwa lilileta mabishano ya kisheria kati ya Wakili wa Serikali Maugo na Wakili wa Gwajima, Peter Kibatala  ambapo upande wa mashitaka ulitaka mshitakiwa awe na wadhamini watakaopatikana wakati mshitakiwa asipokuwepo.
Hata hivyo, Kibatala alidai kuwa mteja wake kwa kuzingatia cheo alicho nacho ni mwaminifu na aliiomba mahakama hiyo, ajidhamini mwenyewe kutokana na muda ambao walipelekwa mahakamani hapo.
Kupitia mabishano hayo, Hakimu Dyansobera alikubaliana na ombi hilo na kumtaka Gwajima asaini hati ya Sh milioni moja.
Akisoma mashitaka ya pili, Wakili Kimaro alidai kuwa Gwajima anakabiliwa na mashitaka ya kushindwa kuhifadhi silaha, ambayo ni kinyume na Sheria ya Silaha za Moto.
Alidai kuwa kati ya Machi 27 na 29 mwaka huu, maeneo ya Hospitali ya TMJ iliyopo Mikocheni A wilayani Kinondoni, akiwa amepewa leseni ya silaha hiyo yenye namba za usajili CAT 5802 na risasi tatu za bastola na risasi 17 za bunduki, aliziacha kwa watu wasio husika bila ya ruhusa.
Kimaro alidai katika siku hiyo washitakiwa Behagaze, Milulu na Mzava walikutwa na bastola bila ya ruhusa na kinyume na taratibu katika Hospitali ya TMJ iliyopo Mikocheni A, Kinondoni.
Mshitakiwa wa tatu alidaiwa kuwa siku hiyo hiyo katika Hospitali ya TMJ, alikutwa na risasi tatu za bastola na 17 za bunduki (shotgun) bila ya kuwa na ruhusa. Mshitakiwa wa nne hakusomewa mashitaka kwa kuwa hakuwepo mahakamani hapo.
Washitakiwa wote walikana mashitaka na kwamba upande wa mashitaka ulidai kuwa upelelezi wa shauri hilo bado unaendelea.
Wakili Kibatala aliomba dhamana kwa washitakiwa hao kwamba wajidhamini wenyewe, lakini Hakimu Dyansobera aliwataka kila mmoja awe na mdhamini mmoja atakayetambulika na Mahakama, atakayesaini dhamana ya Sh milioni moja, ambapo washitakiwa wote walitimiza masharti.
Akizungumza nje ya mahakama, Kibatala alidai kuwa mteja wake alitakiwa kujisalimisha Machi 27 mwaka huu na  alifanya hivyo, lakini mahojiano hayo hayakukamilika, kutokana na matatizo ya kiafya aliyoyapata.
Pia, alidai kuwa mara ya pili aliamriwa apeleke nyaraka 10 za umiliki wa mali zake, ikiwemo helikopta, nyumba na kanisa, ambapo aliamua kuandika barua kuomba vifungu vya sheria, ambavyo alidai kuwa mpaka leo hajapata.
‘’Leo asubuhi nilipigiwa simu na Gwajima akinieleza kuwa amezingirwa na Polisi walioongozwa na Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Kinondoni. Nilipofika nilifanya mazungumzo na Polisi, nikawaambia hakuna sababu ya kuja wengi hivyo, mteja wangu atakuja mwenyewe,’’ alidai.
Baadhi wa waumini waliokuwepo katika viwanja vya mahakama hiyo, walikuwa wakishangilia na kupiga kelele baada ya ‘baba’ yao huyo wa kiroho kuachiwa kwa dhamana.
Gwajima aliondoka mahakamani hapo saa 12:00 jioni kwenye gari namba T 631 AHD aina ya Land Cruiser, huku ikifuatiwa na msafara wa magari ya waumini wake waliokuwa wamepakatana katika magari hayo.
Awali, nyumba ya Gwajima ilizingirwa na Polisi kwa zaidi ya saa saba kuanzia saa 12 alfajiri ya jana hadi saa sita mchana, kwa madai ya kutaka kumkamata, kutokana na kutotokea Polisi kama alivyotakiwa hapo juzi.
Polisi wakiwa na magari ya aina tofauti, walionekana kuzingira nyumba ya askofu huyo iliyopo maeneo ya Tegeta Salasala katika Kata ya Wazo eneo la Kilimahewa, huku nyumba ya mchungaji huyo ikiwa imefungwa geti.
Eneo hilo pia lilizungukwa na wafuasi wa askofu huyo karibu 200, waliokuwa wakisubiri kujua hatma ya kiongozi wao huku wakisali.
Kati ya magari ya Polisi yaliyoonekana katika eneo hilo, kulikuwa na Land Rover Defender zenye namba za usajili T 337AKU na T 475 BNM na mengine aina ya Toyota Land Cruiser yenye namba za usajili PT 1686 na PT 2665 yakiwa na maandishi ya Polisi.
Wakizungumza na mwandishi, baadhi ya waumini wa kanisa hilo walidai wamekuwa na utaratibu wa maombi ya asubuhi siku za Jumatano na Ijumaa, lakini jana walifika kanisani  kama kawaida, lakini hawakumkuta askofu na hakukuwa na  taarifa.
Mchungaji Miriam Eliah alisema waliamua kwenda nyumbani kwake majira hayo ya saa 12 asubuhi, wakakuta mlango umefungwa jambo ambalo si kawaida na walipogonga hawakufunguliwa, lakini walisikia sauti za watoto ndani.
Alisema baadaye waliona gari la Polisi likifika katika maeneo hayo na kushusha polisi na ya pili ikafika na kushusha polisi kisha zikaondoka na baadaye nyingine iliyokuwa na Polisi ikafika maeneo hayo na kubaki karibu na geti la askofu huyo.
Mpaka mchana bado magari ya Polisi yalikuwa yakiendelea kuzunguka karibu na nyumba hiyo, huku baadhi ya viongozi wa kanisa hilo wakiwa katika makundi na vikao wakijadili.
Mwenyekiti wa serikali ya Mtaa wa Wazo anapoishi Gwajima, Richard Njeru, alisema alipata taarifa ya askari kuja kumkamata askofu huyo na aliwaona wakifika saa 12 asubuhi kwa sababu hakufika juzi Polisi kama alivyotakiwa.
Ilipofika majira ya saa sita mchana, magari ya Polisi yaliyokuwepo takriban sita yalianza kuondoka moja moja na gari la mwisho lililondoka muda mfupi baada ya Wakili Kibatala kuwasili saa 6:30 akiwa na teksi.
Wakili huyo alifika katika eneo hilo na kusalimia Polisi kisha kuonana na uongozi wa kanisa hilo waliokuwa wakijadili jambo na baadaye gari la Polisi lililokuwa na polisi wanane liliondoka katika eneo hilo.
Mara baada ya polisi wote kuondoka, waumini wa askofu huyo walisogea katika geti la nyumba ya Gwajima na kuanza kushangilia na kutamka kwa sauti kubwa kuwa ‘majeshi ya bwana ni hatari sana’.
Akizungumza kuhusu kuondoka kwa Polisi hao, Mwenyekiti wa  Baraza la Makanisa ya Kipentekoste Tanzania (CPCT) Wilaya ya Kinondoni na Mchungaji wa Kanisa la EAGT, Emmanuel Mwasota, alisema uongozi wa Polisi umewataka askari waliokuwa maeneo hayo kuondoka na kutaka Askofu Gwajima kwenda mwenyewe katika Kituo cha Polisi cha Kati.
Alisema tatizo lililokuwepo ni mawasiliano, kwani uongozi wa jeshi hilo juzi waliwataka wasiende jana kama ilivyokuwa imetakiwa, kwa kuwa walikuwa wameshajitayarisha kwa kila kitu.
“Tunashangaa leo wamekuja kuzingira nyumba lakini hakuna tatizo kwani baada ya muda askofu atatoka na tutaenda naye polisi kama walivyotuagiza,”alisema
Ilipofika saa 7:32 Kibatala akiongozana na wachungaji wengine wa Kipentekoste akiwemo Katibu Mkuu wa Baraza la Makanisa ya Kipentekoste Tanzania (CPCT), Askofu David Mwasota,  na  aliyekuwa Mbunge wa Bunge Maalum la Katiba, Amon Mpanju, waliingia ndani ya nyumba ya Gwajima.
Baada ya kuingia ndani, nje ya nyumba hiyo magari manne yaliingia katika eneo hilo ambapo alishuka Mtume Onesto Ndegi wa Kanisa la Living Water Center na Mchungaji Vernon Fernandes wa huduma ya Agape na wengineo.
Ilipofika saa 7:27 geti la nyumba ya Askofu Gwajima lilifunguliwa na kutoka gari jeusi lenye namba za usajili T 159, DDH likiendeshwa na mchungaji Hu na pembeni yake amekaa wakili Kibatala.
Pia, katika gari hilo alipanda Askofu Gwajima pamoja na Mpanju na kushangiliwa na waumini wa kanisa hilo na baadaye Wakili Kibatala alizungumza na waandishi wa habari.
“Tunaenda Polisi kuitikia mwito wa kisheria, kwani hatukuwa na taarifa zozote za kisheria za Polisi kuzingira eneo hili na kwa nini walikuja kumkamata, baada ya kufika huko ndiyo tutaelezwa yote,” alisema.

No comments: