WAUAJI WA ALBINO SASA WATANGAZIWA HALI YA HATARI



Rais Jakaya Kikwete amezungumzia hali ya usalama wa nchi, ikiwemo  uvamizi wa vituo vya Polisi,  uporaji wa silaha ulioambatana na vifo vya askari na kusema matukio hayo, baadhi yake yana dalili za ugaidi. 

Akizungumzia hali ya usalama nchini jana katika hotuba yake ya mwisho wa Februari, Rais Kikwete pia amekuja juu  kuhusu mauaji kwa watu wenye albinism na kusema vitendo hivyo vinafedhehesha, kudhalilisha taifa na havivumiliki.
 “Kwa jumla hali ya usalama ni nzuri, hata hivyo kuna matukio ya kiusalama ambayo ningependa kuyazungumzia.  La kwanza ni mashambulizi yenye sifa za ujambazi na mwelekeo wa kigaidi.  Na, la pili ni la mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi,” alisema Kikwete. 
Akizungumzia mauaji ya albino yaliyoanza kuibuka tena mwaka jana na mwaka huu, baada ya hali kuwa tulivu mwaka 2011, Rais Kikwete amekubali kukutana na viongozi na wanachama wa Chama cha Watu Wenye Ulemavu wa Ngozi, kwa lengo la kuwasikiliza na kuangalia jinsi ya kumaliza mauaji ya watu hao, yanayofanywa kwa imani ya ushirikina.
 “Naungana na Chama cha Albino Tanzania kulaani ukatili huu na kutaka watu wote wanaojihusisha na ukatili huu wasakwe, wakamatwe, wafikishwe mahakamani na kupewa adhabu kali inayowastahili wanapopatikana na hatia,” alisema Rais Kikwete.  
 “Nimekubali wiki ijayo kukutana na baadhi ya viongozi na wanachama wa Chama cha Watu Wenye Ulemavu wa Ngozi,  kuwasikiliza maoni yao na kuangalia jinsi ya kumaliza tatizo hili. Kwa kweli, mauaji ya albino ni jambo linalofedhehesha na kudhalilisha taifa letu, ni vitendo visivyovumilika…hatuna budi sote kushikamana na kuhakikisha tunapambana nao kisawasawa na kuwashinda, tusikubali kamwe waturudishe kule kubaya tulikokuwa zamani, alisisitiza Rais Kikwete.    
Rais Kikwete aliongeza  “Nimesikitika na mauaji ya ndugu zetu albino. Ni vitendo vya kinyama ambavyo havitegemewi kufanywa au kutokea katika jamii yeyote.  Naamini ushirikiano wa karibu kati ya serikali na jamii utatuwezesha kutokomeza mauaji ya ndugu zetu wenye ulemavu wa ngozi na kuliondolea taifa letu aibu hii”.
Alisisitiza,  watu wenye ulemavu wa ngozi ni wanadamu kama walivyo wasio na ulemavu huo na wana haki sawa ya kuishi na kupata hifadhi ya maisha yao, kama walivyo wanadamu wengine.  
Alitaka jamii kushikamana kuhakikisha mapambano dhidi ya wahalifu hao yanafanywa na kuwakamata, wafikishwe kwenye vyombo vya sheria, haki itendeke.
 “Niwahakikishie ndugu zangu albino wakati wote serikali inalipa uzito mkubwa suala la kudhibiti na kukomesha mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi , watuhumiwa kadhaa wa mauaji hayo wako waliokwishahukumiwa na wengine bado wanaendelea kusakwa,” alisema Rais Kikwete.
Aliongeza serikali itatumia mbinu na maarifa iliyotumia  kukabili wimbi kubwa la mauaji hayo miaka ya nyuma. Aliomba wananchi kutoa ushirikiano wa kuwafichua watu wanaofanya vitendo vya mauaji na kukata viungo vya watu wenye ulemavu wa ngozi.
 “Kutokomeza kabisa matukio ya mauaji na ukataji wa viungo vya watu wenye ulemavu wa ngozi ni jambo linalowezekana, kikubwa ni watu kuacha imani za ushirikina, eti kiungo cha albino kinaweza kukusaidia, ni imani potofu kabisa, uvuvi, uchimbaji madini, biashara ni vichocheo vya uovu huu,” alisema Rais Kikwete.
Aliomba wananchi  kusaidia kutoa taarifa kuhusu wanunuzi wa viungo hivyo na waganga wanaochochea mahitaji ya viungo vya albino.
Tukio la kwanza liliripotiwa mkoani Geita tangu Aprili 17 mwaka 2006. Watuhumiwa wa mauaji hayo waliuawa na wananchi wenye hasira. Mwaka 2007 kulikuwa na matukio saba na mwaka 2008 matukio ya mauaji ya albino yaliongezeka kutokana na watu 18 waliouawa. 
Kikwete alisema jitihada za serikali zilifanywa kwa kushirikiana na wananchi na hivyo mauaji yalipungua na kuwa tisa mwaka 2009. Mwaka 2010 matukio hayo yalipungua na kuwepo na tukio moja.
Mwaka 2013 mmoja aliuawa na wengine watatu walijeruhiwa. Mwaka 2014 waliuawa albino watatu na wawili walijeruhiwa. Januari mwaka huu, tukio moja mkoani Geita limeripotiwa. 
Matukio ya mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi yametokea katika mikoa 10 kati ya mikoa 30 nchini.  Mikoa hiyo ni  Mwanza wenye matukio 13, Kagera (sita), Tabora (matano), Geita (manne) na Mara matukio manne.
Mikoa mingine ni Kigoma (manne), Simiyu (matatu), Shinyanga (mawili), Arusha (moja) na Mbeya tukio moja.  
Rais alisema katika kipindi cha takribani miezi 12, kumekuwa na matukio ya watu kuvamia vituo vya Polisi, wengine kuchoma  moto na kupora silaha.  “Pia kumekuwepo na matukio ya kuwashambulia Polisi walioko kwenye doria na wengine kuporwa silaha,” alisema. 
Kikwete ambaye amepongeza polisi wakishirikiana na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania kwa kazi kubwa waliyofanya, amesema vyombo vya  usalama vinaendelea kufanya kazi ya uchambuzi wa kila tukio na kulipa nafasi yake stahiki; kwa maana kama ni la ujambazi au ugaidi. 
“Mafanikio tunayaona, kama nilivyoeleza  na kama tulivyosikia kule Tanga hivi karibuni, ni matunda ya ushirikiano huo.  Hata hivyo, nimewataka waendelee kuwasaka watu hawa waovu popote walipo ili wafikishwe mahakamani na kuzirejesha mikononi mwa Polisi silaha zote zilizoporwa,” alisema.  
Rais alitaja maeneo ya matukio husika ni  Newala, Ikwiriri, Kimanzichana, Ushirombo, Songea, Pugu Machinjioni na Tanga ambako jumla ya silaha 36 ziliporwa, askari saba walipoteza maisha na wengine kupata majeraha.
Vituo vya Polisi vilivyovamiwa na silaha kuporwa kwenye mabano ni Newala mkoani Mtwara (3), Ikwiriri wilayani Rufiji (7), Kimanzichana wilayani Mkuranga ni silaha tano ambazo kati yake, mbili ni za polisi na tatu za raia waliokwenda kuzihifadhi.
Uvamizi ulifanyika pia kwenye vituo vya Ushirombo wilayani Bukombe (18), Pugu Machinjioni (1), Tanga (2) na Ruvuma ambako kulikuwepo na matukio mawili ya Polisi kushambuliwa lakini silaha hazikuporwa.
Kwa mujibu wa Rais Kikwete, silaha 18 zilizoporwa Ushirombo zimepatikana na watu 10 wanaotuhumiwa kuhusika na uhalifu huo wamekamatwa.  
Kuhusu tukio la Tanga, Kikwete alisema silaha moja kati ya mbili zilizoporwa imepatikana na watuhumiwa saba wametiwa mbaroni, wanne  kati yao ni waliokuwa wamejificha katika mapango ya Kiomoni wilayani Tanga. 
Kwa upande wa watu wanne wanaotuhumiwa kuhusika na tukio la Ikwiriri, walikamatwa na kwenye tukio la Newala, silaha zote tatu zimepatikana na watu wawili wametiwa nguvuni.  
 “ Upelelezi unaendelea wa kuzipata silaha zilizoporwa ambazo hazijapatikana mpaka sasa kila moja kutoka Kimanzichana, Pugu Machinjioni na Tanga,” alisema.
Aidha, Kikwete alitoa wito kwa wananchi kushirikiana kwa karibu na vyombo vya usalama hususani Jeshi la Polisi  kupata mafanikio zaidi dhidi ya uhalifu kwa kutoa taarifa za kuwapo vitendo viovu au nyendo za watu waovu wanavyokusudia kufanya wahalifu au taarifa za waliokwishafanya uhalifu.  
Kikwete pia alitaka wananchi kuacha kushabikia watu waovu, wala kueneza taarifa zao potofu kwenye mitandao ya kijamii.  
 “ Tutumie mitandao ya kijamii kuponda fikra zao potofu, fikra zao hasi na vitendo vyao viovu pamoja na kuwafichua wao na mambo yao mabaya wayafanyayo,” alisema.
Pia, Kikwete aliwapongeza wananchi waliotoa taarifa zilizowezesha kuzuia uhalifu  kufanyika  au kufanikisha kuwatia mbaroni wahutumiwa wa vitendo vya ujambazi na ugaidi.
Wakati huohuo, Rais Jakaya Kikwete ameagiza Hazina kuhakikisha inaitengea fedha Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC)  kwa kazi ya kuandikisha wapiga kura kwa Mfumo wa Teknolojia ya Utambuzi wa Alama za Vidole ‘Biometric Vote Registration’ (BVR) ikamilike kama ilivyopangwa.
Aidha, ametaka watu kuwa na subira  kuhusu Kura ya Maoni, wazingatie masharti ya Sheria ya Kura ya Maoni na Kanuni zake. 
Akihutubia taifa jana, Kikwete alisema Serikali itatimiza ahadi yake kwa kufanya kila linalowezekana kuwezesha Tume kirasilimali iweze kutimiza jukumu hilo.
Kauli ya Rais imekuja siku chache baada ya vyama vinavyounda Ukawa hivi karibuni kukaririwa katika mkutano na waandishi wa habari, vikisema Nec inakabiliwa na ukosefu wa fedha, utakaoifanya Tume  ishindwe kutekeleza majukumu yake ya uandikishaji wapiga kura kwa ufanisi.
 Ukawa kupitia kwa Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahimu Lipumba vilitaka Serikali kuelekeza nguvu na kuiongezea fedha Nec. 
Vyama hivyo vilisema uhaba huo wa fedha umefanya Tume kuwa na upungufu wa mashine 7,750  na pia kutokuwa na watumishi wa kutosha. 
 “Nimekwishawakumbusha Hazina kuhusu umuhimu wa zoezi hili kufanikiwa kama ilivyopangwa. Nimewataka wahakikishe wanatoa kipaumbele cha kwanza katika mgao wa fedha. Kama haifanyiki, naomba Tume waniambie mimi mwenyewe,” alisema.
Aidha, Kikwete alisema changamoto za kiufundi zilizojitokeza na zile zinazotokana na upya wa mfumo kwa watumiaji, zimefanyiwa kazi na watengenezaji wa vifaa vinavyotumika katika awamu hii ya uandikishaji nchi nzima. 
Alisema, kuanza kutumika kwa teknolojia hii ni kielelezo cha utashi wa Serikali kuwa nchi  iwe na uchaguzi ulio huru, wazi na haki.
Akizungumzia kuanza kwa uboreshaji wa daftari na uandikishaji wapiga kura ulioanzia katika mji wa Makambako, Kikwete alisema wananchi wamejitokeza kwa wingi kuliko ilivyotarajiwa.
Alisema kati ya Februari 23 hadi 25 mwaka huu, Tume ilitegemea kuandikisha wapiga kura 9,541 lakini kutokana na mwamko wa wananchi wameweza kuandikisha wapiga kura 13,042.  
Kikwete alisema kila kituo kilikuwa kinaandikisha kati ya wapiga kura 80 na 150 kwa siku, huku lengo la Tume ni kuandikisha wapiga kura 32,000 katika Halmashauri ya Makambako ambako kwa siku wanatarajia kuandikisha watu 4,320.  
“ Naambiwa kuwa hesabu za juzi na jana wameandikisha hadi wapiga kura 6,000 kwa siku.  Kwa kasi hii na kama mambo yatakwenda kama inavyotarajiwa, lengo litafikiwa na hata kuvukwa.” 
Kikwete aliipongeza Tume kwa hatua waliyofikia katika uandikishaji na kuwa hali hiyo inaondoa hofu iliyoanza kuingia miongoni mwa baadhi ya watu kuwa huenda zoezi hili lisingefanikiwa.  
Kabla ya uzinduzi uliofanywa mwezi uliopita na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda Tume ilifanya majaribio ya uandikishaji wa wapiga kura kwa kutumia mashine za BVR katika kata 10 za halmashauri za Kinondoni, Kilombero na Mlele kazi iliyofanyika kwa mafanikio kwa kuvuka malengo ya uandikishaji.
Kilombero walifikia asilimia 110.9 ya lengo, Mlele asilimia 101 na Kawe ilikuwa ni asilimia 105.67.    
Aidha, Kikwete ametoa wito kwa wananchi kuhakikisha wanakwenda kujiandikisha kwa mujibu wa ratiba ya uandikishaji katika maeneo yao kama itakavyotolewa na Tume.
“Msifanye ajizi maana hakutakuwepo na fursa nyingine ya kujiandikisha kabla ya uchaguzi mkuu baada ya fursa hii kupita.  
Kikwete aliongeza, “Naendelea kusisitiza kuwa watakaojiandikisha wakati huu ndio watakaopiga kura ya maoni kuhusu Katiba Inayopendekezwa na ndio watakaopiga kura katika uchaguzi mkuu, kwani vitambulisho vya zamani havitatumika.
Kikwete pia alitumia fursa hiyo kuwaomba viongozi wa vyama vya siasa, Serikali, dini na asasi za kiraia kuungana na Serikali na Tume katika kuwakumbusha na kuwahamasisha wananchi wakajiandikishe.
 “Naomba tusiwachanganye wananchi kwa kutoa taarifa zisizokuwa za kweli na kuwafanya wakaacha kujiandikisha.”
Alisema, Serikali itafanya kila linalowezekana kuhakikisha kila atakayejitokeza anaandikishwa na kuzipatia ufumbuzi kwa wakati changamoto zitakapojitokeza.
 “ Kupiga kura kuamua kuhusu Katiba Inayopendekezwa au kuchagua Rais, Wabunge na Madiwani ni haki na wajibu wa kila raia. Kuipata haki hiyo na kuweza kutimiza wajibu huo kunategemea kuwa na kitambulisho cha mpiga kura.  Bila ya hivyo haiwezekani.”
Akizungumzia Kura ya Maoni ya Katiba Inayopendekezwa, alisema  Tume pia  itatoa maelekezo kuhusu kampeni ya Kura ya Maoni wakati ukiwadia.  
 “Naomba watu wawe na subira na kuzingatia masharti ya Sheria ya Kura ya Maoni na Kanuni zake.  Tukifanya hivyo, zoezi hili muhimu na la kihistoria litatekelezwa kwa usalama na utulivu.  Watu watafanya uamuzi kwa uhuru, uelewa, amani na usalama.” 
Kikwete alisema utekelezaji  wa mchakato huo wa kura ya maoni, umeshaanza na unaendelea ikiwa ni pamoja kuandikisha wapiga kura na usambazaji wa katiba hiyo.
Alisema hadi mwishoni mwa Februari, vitabu 1,558,805 vilikuwa vimechapishwa na nakala 1,341,300 kusambazwa.  Nakala 1,141,300 zimesambazwa kwenye mikoa 25 ya Tanzania Bara na nakala 200,000 zimegawiwa Zanzibar.  
Alisema kwa upande wa Tanzania Bara kila kata imepewa vitabu 300.  Kwa vile kata zina wastani wa vijiji vitano hii ina maana kwamba kila kijiji kimepata vitabu 60.
Kikwete alisema mpaka sasa asasi za kiraia 495 zimejiandikisha kwa ajili ya kutoa elimu kwa umma, asasi 420 ni za Bara na 75 za Zanzibar.

No comments: