WAGANGA 55 MWANZA WAKAMATWA KWA RAMLI CHONGANISHI

Jeshi la Polisi mkoani Mwanza linawashikilia waganga wa kienyeji 55 wanaopiga ramli chonganishi na kusababisha madhara makubwa yakiwemo ya mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi pamoja na vikongwe.

Katika idadi hiyo, mmoja wa waganga hao anadaiwa kukutwa na nywele zinazodhaniwa kuwa ni za mlemavu wa ngozi (albino) pamoja na debe tatu za bangi.
Hayo yalielezwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Valentino Mlowola, wakati
akizungumza na waandishi wa habari kufuatia operesheni za kuwasaka waganga wakienyeji wanaopiga ramli chonganishi ambazo zimekuwa zikiathiri walemavu wa ngozi kwa kauli na matendo yao.
Alisema kati ya hao waliokamatwa 18 ni wanawake na 37 na wanaume ambapo walipokamatwa walikutwa wakiwa na nyara mbalimbali za serikali walizokuwa wakizitumia huku wakizimiliki pasipo halali zikiwemo ngozi za simba.  
Alisema operesheni hiyo ambayo ni endelevu ilianza Machi 6, mwaka huu watuhumiwa hao walikutwa na nyara mbalimbali za serikali zikiwemo ngozi za simba, chui,fisi, swala, kiboko, chatu, nyoka aina ya kifutu, yai la mbuni, nyegere na nungunungu.
Aidha, alisema watuhumiwa hao walikamatwa wakiwa na vifaa mbalimbali vya kupigia ramli chonganishi ambavyo ni simbi, vibuyu, visonzo, sarafu za kale, ungo, ngoma, manyanga, vyungu, mizizi ya miti shamba, mikuki, mishale, shuka nyeupe, nyekundu na nyeusi.

No comments: