Serikali imetakiwa ichunguze viongozi wa
madhehebu ya dini ya Kikristo na Kiislamu nchini, ili ijiridhishe na mienendo
ya utume wao wa kuhubiri injili na sala kwa wananchi.
Lengo la uchunguzi huo, limeelezwa kuwa ni
kubaini viongozi wa kiroho wanaokwenda kinyume na maadili ya kazi zao, hususani
wakati huu nchi inapokaribia Uchaguzi
Mkuu, ili kujenga na kuimarisha mshikamano na amani ya nchi kwa wananchi na
Taifa kwa ujumla.
Rai hiyo ilitolewa juzi jijini hapa na Naibu
Kadhi Mkuu Tanzania Bara, Sheke Abubakari Zuberi, wakati akizungumza kwenye
kongamano la amani la ndani mkoani hapa.
Kongamano hilo, lilishirikisha maaskofu na
mashehe, wakuu wa wilaya, wabunge, kamati za ulinzi na usalama na wananchi
kutoka wilaya zote saba za Mkoa wa Mwanza.
“Viongozi wa dini wachunguzwe na Serikali kama
zinavyofanya nchi zingine, maana wao wanaweza kuipotosha amani.
“Kama wapo wanaotuhumiwa kushiriki kwenye
vitendo vya rushwa wanaweza kuiharibu amani ya nchi, kwa sababu wana hamasa
kubwa na wafuasi wengi wanaoweza kuwahamasisha kuvuruga amani ya nchi tuliyo
nayo,” alisema.
Aliwataka viongozi wa dini na wanasiasa,
kujiepusha na vitendo vya ufisadi kwa maelezo kuwa vinawaondolea heshima yao
inayotokana na maadili ya kiroho, hasa
katika kuhudumia waumini wao na kuwaongoza wananchi kwenye maeneo
yao.
Aliwataka wananchi na viongozi wa madhehebu ya
dini, washirikiane pamoja kutoa taarifa za matukio yenye kuhatarisha amani mara
wanapobaini viashiria vya kuhatarisha amani katika nchi, kwa kuwa maskari
waliopo nchini hawawezi kulinda amani ya nchi peke yao.
Aliitaka Serikali ianzishe mtaala maalumu wa
amani, utakaofundishwa katika shule za msingi na sekondari, ili kukuza na
kujenga vijana maadili kwa faida ya nchi na maendeleo yao.
Aliwataka viongozi wa kisiasa, wahubiri amani
bila ya kujali itikadi ya vyama vyao vya siasa na kwa kushirikiana na Serikali,
washiriki kikamilifu kwenye utatuzi wa migogoro inayowakumba wananchi kwa sasa,
ikiwemo ya wakulima na wafugaji.
Alilaani watu wanaoua wenzao wenye ulemavu wa
ngozi kwa madai ya kujipatia utajiri na madaraka, ambapo alisema jambo hilo
linalaaniwa na viongozi wote wa madhehebu ya dini.
Naye Mchungaji Dk William Kopwe, kutoka Jumuiya
ya Kikristo Tanzania (CCT), alisema kuwa amani ya nchi sio kitu cha kuchezea
kiholela, na kuongeza kuwa ni kitu kinachofaa kuheshimiwa na kuenziwa na watu
wa makundi yote katika jamii.
“Suala la amani ya nchi liangaliwe kwa mapana
yake, sio jambo rahisi la kuchezea chezea hivi, na ili ujue amani ni kitu gani,
iweke katika makundi mawili, amani hasi inayotokea kunapokuwepo vurugu na
mifarakano na amani chanya ambayo ni kinyume cha hayo,” alisema.
Awali wali
katika hotuba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo, iliyosomwa kwa niaba
yake na Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Baraka Konisaga, alisema kongamano hilo la
amani ni la kujenga na sio la kubomoa na Serikali inatarajia kuona upendo na
mshikamano wa watu wote katika kulinda amani ya nchi
Alisema baada ya kuhamia jijini Mwanza,
alishukuru kukuta ipo Kamati ya Amani inayojishughulisha na suala zito la amani
na kuitaka kamati hiyo kufika katika ofisi yake wakati wowote watapokuwa na agenda
ya kujadili suala la amani.
No comments:
Post a Comment