Rais Jakaya Kikwete jana ameongoza mamia ya wakazi
wa Dar es Salaam waliojitokeza kuaga mwili wa Mbunge wa Mbinga Magharibi,
Kapteni John Komba aliyefariki Jumamosi jioni katika Hospitali ya TMJ ikielezwa
kuwa kaondoka kama moto wa kiberiti.
Tukio hilo lilifanyika jana Dar es Salaam katika viwanja
vya Karimjee, na kuwakutanisha viongozi mbalimbali wa serikali wakiwemo Makamu
wa Rais, Marais wastaafu akiwemo Benjamin Mkapa (pichani) na Ali Hassan Mwinyi,
mawaziri mbalimbali, manaibu mawaziri, viongozi wa vyama vya upinzani,
mwanasheria mkuu, viongozi wa dini na wabunge.
Katika tukio hilo lililojaa simanzi na vilio vilitawala,
huku baadhi ya nyimbo alizokuwa ameziimba marehemu, Kapteni Komba zikiimbwa na
baadhi ya wasanii wakati wa kuaga.
Akizungumza katika tukio hilo, Mwenyekiti wa Kamati ya
Bunge ya Maendeleo ya Jamii, Said Mtanda alisema msiba wa Kapteni Komba ni pigo
lisilozibika kamwe na siku alipofariki alimpigia simu wakazungumza kwa saa nne
kuhusu safari ya kamati hiyo kuelekea nchini Ethiopia kikazi.
“Tulipanga mambo mengi yakiwemo namna tutakavyotekeleza
majukumu na jinsi ya kwenda Ethiopia… wajumbe wa kamati ilikuwa waondoke Machi
mosi…lakini saa kumi jioni nikapokea ujumbe kuwa Komba amefariki,” alisema
Mtanda na kuongeza kuwa alikuwa amali na rasilimali kwa familia, Chama Cha
Mapinduzi na hata kwa wananchi wake jimboni.
Alisema Kapteni Komba alisimamia haki za wazee na kwamba
Kamati itaendelea kusimamia yote yaliyoasisiwa na Mbunge huyo wa Mbinga ambaye
pia alikuwa Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi
(CCM) Abdulrahman Kinana alisema Kapteni Komba alikuwa muimarishaji na
mkuzaji wa CCM katika maeneo mbalimbali kwa kupitia nyimbo zake.
“Wakati wa msiba wa Nyerere atakumbukwa kwa ujasiri wake
na msimamo wake kwani alitunga nyimbo nyingi zenye kuwaliwaza
Watanzania,”alisema Kinana na kuongeza kuwa vishindo pamoja na sauti yake
vimezimika.
Alisema kifo chake kimeleta pengo kubwa kwa CCM,
wasanii huku daima akikumbukwa kwani wakati wa uhai wake aligusa maisha ya
walio wengi akiwa mwanajeshi, mwalimu, msanii na hata mwanasiasa.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera,Uratibu na
Bunge, Jenista Mhagama alisema serikali itaendelea kutekeleza mipango ya
Maendeleo iliyokuwa ikitekelezwa katika jimbo la Mbinga Magharibi kama
ilivyokuwa imepangwa katika jimbo hilo.
Alisema Komba atakumbukwa kwa ucheshi, msimamo
katika masuala mbalimbali pia mchango wake kupitia vipaji alivyokuwa navyo.
Spika wa Bunge, Anne Makinda alisema kifo cha
Komba kaondoka na moto wa kiberiti, akiondoka na talanta zake,
jambo linalosababisha wengi kutokuamini ambapo Mungu haachi kutoa
mafundisho.
Alisema Kapteni Komba ilikuwa aende nchini Ethiopia na
wenzake na kabla ya mauti kumkuta alikuwa akiandika nyimbo.
“Kifo kitampata kila yeyote…angejua na kupewa hata muda
kidogo angesema wale wote waliomkosea anaomba wamsamehe…na pia sisi tunapaswa
kumsamehe,” alisema Makinda na kuongeza kuwa wakati mwingine watu hutumia
midomo isivyo na ikumbukwe kuwa kila mmoja anatoka kwa Mungu.
Alisema Kapteni Komba alitekeleza wajibu wake kama
binadamu na amekwenda kupeleka hesabu yake ya aliyoyafanya duniani huku CCM
ikiamini kuwa Mungu atawapa Mbunge mwingine katika jimbo hilo.
Kiongozi wa Upinzani Bungeni, aliyewakilishwa na Mbunge
wa Arumeru Mashariki Joshua Nassari alisema pamoja na itikadi zao
bungeni lakini umoja wao ni nguzo kuu.
Alisema kifo ni safari ya kila mmoja, na kila
binadamu anapaswa kutambua kuwa maisha ni mafupi na kujifunza kutenda mema
kuanzia ngazi ya familia na hata kwa taifa.
Mweyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku
alisema Kapteni Komba alikuwa na utendaji ulio bora alifanya hivyo bungeni
akiwa na uwezo wa kusimanga viongozi bila kuwaudhi.
Alisema alikuwa mkweli akistahili kukumbukwa kwa uongozi
alioutoa kupitia kipaji chake cha kuimba na baadaye katika Bunge na zaidi
katika kusaidia CCM.
No comments:
Post a Comment