UPELELEZI KESI YA LWAKATARE NA MWENZAKE BADO KUKAMILIKA



Upelelezi wa kesi ya kula njama ya kudhuru kwa sumu, inayomkabili Mkurugenzi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Wilfred Lwakatare na mwenzake bado haujakamilika.

Wakili wa Serikali Genes Tesha alidai hayo jana mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Janeth Kaluyenda wakati kesi hiyo ilipotajwa jana.
Hakimu Kaluyenda aliahirisha kesi hiyo hadi Aprili Mosi mwaka huu itakapotajwa tena kwa ajili ya kuangalia kama upelelezi umekamilika.
Lwakatare na Ludovick Joseph wanadaiwa Desemba 28, mwaka juzi katika eneo la King’ong’o, Wilaya ya Kinondoni, kwa pamoja walikula njama za kutoa sumu kwa nia ya kumdhuru Mhariri wa Gazeti la Mwananchi Dennis Msacky.
Katika hatua nyingine, upelelezi wa  kesi ya mauaji ya kutokusudia kutokana na kuporomoka kwa jengo la ghorofa 16, inayowakabili watu 12 bado haujakamilika.
Washitakiwa katika kesi hiyo ni Gabriel Fuime, mfanyabiashara Laza Radha, Diwani katika Manispaa ya Kinondoni, Ibrahim Mohamed (59), vigogo wa Manispaa ya Ilala ambao ni Mhandisi Mkuu, Charles  (48), Mhandisi wa Majengo Godluck Sylivester (35) na Mkurugenzi Mkuu wa Mkaguzi wa Majengo, Willibrod Mugyabuso (42).
Wengine ni Mhandisi Mohamed Abdurkarim (61), Mhandisi Mshauri, Zonazea Oushoshaodaga Hema (59), Msajili Msaidizi AQRB, Albert Mnuo na Ofisa Mkuu Mtekelezaji OQRB, Joseph Ringo (60), Mkadiriaji Ujenzi, Vedasto Ruhale (59), Msanifu Majengo, Michael. Waliowasilisha ombi hilo ni washitakiwa tisa uamuzi unawahusu washitakiwa wote.
Inadaiwa kuwa Machi 29 mwaka jana, katika mtaa wa India Gandhi Ilala, Dar es Salaam bila kukusudia washitakiwa waliwaua watu 27.

No comments: