UJENZI MAABARA YA EBOLA KUKAMILIKA MWEZI HUU


Tanzania inazidi kupiga hatua katika sekta ya afya, na sasa inatarajia kuachana na usafirishaji wa sampuli za magonjwa ya uambukizi mkali yenye virusi visababishavyo damu kutoka mwilini, ikiwemo ebola na dengue.

Hali hiyo inatokana na kuanza ujenzi wa maabara ya magonjwa hayo, unaotarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi huu.
Maabara ya kwanza ya magonjwa hayo, inajengwa katika Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya, ambapo zaidi ya Sh milioni 109 zimeshatumika.
Maabara hiyo itakayoanza kutumika hivi karibuni, itakuwa imeboreshwa kutoka iliyokuwepo awali ya upimaji maambukizi ya kifua kikuu.
Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Steven Kebwe alisema ukarabati wa maabara hiyo, ulianza Februari mwaka huu na utakamilika mwishoni mwa mwezi huu baada ya mkandarasi kutia saini mkataba na Serikali Februari 6, mwaka huu akipewa wiki nne. Alisema hayo baada ya kutembelea hospitali hiyo na kuzungumza na watumishi hivi karibuni.
Dk Kebwe alisema maabara hiyo inatarajiwa kuanza kutumika kabla ya mwezi Julai mwaka huu, ambapo sekta ya afya itaingia katika mfumo wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) na hivyo kusaidia urahisi wa upatikanaji wa huduma kwa kiwango cha juu.
Alisema kukamilika kwa maabara hiyo, kutapunguza maambukizi ya magonjwa ya milipuko kama vile dengue, ebola na homa ya bonde la ufa.
Pia, maabara hiyo itatumika kufanyia utafiti, kufundishia na vipimo kwa watu walioambukizwa na wasioambukizwa.
Naibu Waziri alisema awali kabla ya kuwa na maabara ya kupima magonjwa hayo, mtu yeyote akiugua ilikuwa inalazimu damu yake kuchukuliwa kisha kupelekwa Afrika Kusini au Nairobi kwa ajili ya vipimo, kutokana na kuwepo kwa maabara yenye uwezo huo na hivyo kuchelewa upatikanaji wa majibu.
Alisema uwepo wa maabara katika Mkoa wa Mbeya, utasaidia kukabiliana na magonjwa ya milipuko yanayotokea katika nchi za jirani, kama Malawi, Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Dk Mpoki Ulisubisya alisema upatikanaji wa maabara hiyo ni hatua kubwa na muhimu ambayo Serikali imeifanya kukabiliana na magonjwa yanayotokana na kutokwa damu mwilini.

No comments: